Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)
Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi na misingi yake. Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa, kutokana na mitazamo yao ya kuchupa mipaka, mafemenisti si tu kwamba hawakuweza kufidia madhara yanayowapata wanawake bali pia wamewazidishia masaibu na mashaka kama kuwaweka mbali zaidi watu wa jinsi hiyo na nafasi yao asili na halisi yaani nafasi ya kuwa mama, mwanamke na mke.
Tulisema kuwa Uislamu umepinga mitazamo hiyo inayochupa mipaka kulia na kushoto kuhusu nafasi na hadhi ya mwanamke na kumpa hadi na nafasi anayostahili. Katika kipindi hiki tutaendela kuzungumzia nafasi aali ya mwanamke katika Uislamu.
Dini ya Uislamu kama mlivyosikia imejiepusha kabisa na misimamo ya kuchupa mipaka kuhusu nafasi ya mwanamke na kumpa hadhi ya juu. Dini hiyo inasisitiza kuwa tofauti za kimaumbile zilizopo baina ya mwanamke na mwanaume ni dharura kwa ajili ya kufikia ukamilifu wa jinsia hizo mbili na kwamba licha ya tofauti hizo za kimwili watu wa jinsia hizo mbili wako sawa katika ubinadamu japo kuwa kila mmoja wao ana mchango na wadhifa tofauti katika baadhi ya mambo kutokana na muundo makhsusi wa kimwili, kinafsi na kihisia kila mmoja wao. Mwanafalsafa wa Kiislamu wa Iran Shahid Murtadha Mutahhari anasema: Mwanamke na mwanaume ni nyota mbili katika obiti na mizingo miwili tofauti na kila nyota inapaswa kupita na kufanya harakati katika njia yake. Sharti kuu la saada na ufanisi wa kila mmoja wao na jamii ya mwanadamu kwa ujumla ni kwa kila mmoja kati ya jinsia hizo mbili kupita kwenye obiti ya njia yake. Uhuru na usawa unakuwa na faida wakati kila mmoja hao hataondoka katika njia yake ya kimaumbile..", mwisho wa kunukuu.
Katika kipindi hicho ambapo jamii nyingi za wanadamu hususan jamii ya kijadi ya Bara Arab zilikuwa zikikanyaga haki ya mwanzo na ya kimsingi kabisa za mwanadamu yaani haki ya kuishi, Uislamu ulikuja na kuhuisha nafasi na hadhi ya mwanamke kwa mafundisho yake ya mbinguni na kupiga hatua kubwa katika kutimiza haki za watu wa jinsia hiyo.
Kwa mujibu wa mtazamo wa Uislamu, thamani na utukufu wa mwanamke na mwanaume uko sawa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Katika upande huu hakuna mbora kuliko mwenzake na tofauti za kisheria zilizopo baina ya wawili hao ni jambo la dharura kutokana na tofauti za kimuundo na kimwili. Kwa msingi huo mafeministi wamefanya dhulma kubwa dhidi ya mwanamke kwa kuamini usawa kamili wa kisheria baina ya jinsia hizo mbili bila ya kutilia maanani maumbile ya mwanamke na mwanaume. Inatupasa kueleza hapa kuwa, kila moja kati ya Uislamu na ufeministi inataka kutimizwa haki za wanawake lakini licha ya lengo hilo la pamoja, mifumo hiyo miwili inatofautiana kikamilifu katika chanzo na mbinu za kutimiza haki za wanawake. Uislamu unatafuta na kuchukua haki za wanawake katika maneno ya Mwenyezi Mungu Muumba wa mwanaume na mwanamke na ufeministi unatafuta haki hizo katika maneno ya wanadamu. Jambo linalotakikana katika Uislamu si kutimizwa haki makhsusi za mwanaume au haki makhsusi za mwanamke, bali haki za kibinadamu ili chini ya kivuli chake upatikane uhusiano bora zaidi. Katika uhusiano huo hakuna dhalimu au anayedhulumiwa, kwani kila mmoja wao anakuwa katika nafasi yake na kwa msingi huo anatumia haki zake.
Taswira inayotolewa na Uislamu kuhusu mwanamke ni taswira ya mwanadamu kamili katika pande zote za kibinadamu sawa kabisa na mwanaume. Katika fikra za Uislamu wanawake kama walivyo wanaume, wana uwezo wa kiakili na wa kutafakari na vilevile kufanya amali njema. Kinyume na dhana za watu wa kale ambao walikuwa wakisema kuwa amali na matendo mema ya mwanamke hayakubaliwi na Mwenyezi Mungu, katika Uislamu hakuna tofauti baina ya mwanamke na mwanaume katika suala hilo, na kigezo cha kutakabaliwa amali za mja awe mwanamke au mwanaume, ni kuwa mtu mwema na imani ya mtendaji. Katika Qur'ani imani na amali njema si makhsusi kwa mwanaume tu au mwanamke tu, bali Mwenyezi Mungu anakubali amali na matendo mema ya kila mmoja wao. Aya ya 97 ya Suratul Nahl inasema: Mwenye kutenda mema, mwanaume au mwanamke, naye akawa muumini, tutamhuisha maisha mema na tutawapa ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya." Kwa msingi huo malipo ya Mwenyezi Mungu na kuwa karibu yake hakuhusu jinsia makhsusi bali kunafungamana na imani na amali ya mja, na wanawake kama walivyo wanaume, wanapata thawabu na malipo ya amali na matendo yao mema.
Katika upande mwingine katika Qur'ani Tukufu Mwenyezi Mungu SW anasema kuwa lengo la mwisho la kuumbwa mwanadamu ni kumwabudu Yeye na thamani na utukufu wa mwanadamu sawa awe mwanamke au mwanaume, unatokana na kiwango cha uja na ibada zake. Uja na ibada hizo zenye ikhlasi humvika mwanadamu vazi fakhari na utukufu na kumfikisha katika daraja ya kuwa khalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi. Vilevile sifa kuu ya Mtume Muhammad (saw) ni kuwa mja wa Allah na njia hii ya kuwa mja mwema ndiyo inayoipa ukamilifu roho ya mwanadamu. Kwa msingi huo kwa kuwa wanawake wana roho nyepesi na laini zaidi kuliko wanaume, wanaweza kufikia makamu na nasi hiyo ya uja kwa wepesi zaidi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, miongoni mwa masharti ya ukamilifu wa mwanadamu ni kuwa na roho laini na nyepesi. Mwenyezi Mungu SW anasema kuwa hakuna tofauti kati ya wanadamu katika upande wa kibinadamu. Uchunguzi kuhusu historia ya wanawake vigezo na ruwaza njema kama Bibi Fatimatu Zahra Bibi Maryam (as) ambao walikuwa mfano wa kuigwa katika ikhlasi na uchamungu unatufikisha kwenye hakika kwamba, ibada na uchamungu havifuati jinsia ya mtu na kwamba wanawake wanaweza kufikia daraja za juu za ukamilifu wa kiroho.
Miongoni mwa mambo ambayo hayafuati jinsia ya mtu ni suala la kutafuta na kupata elimu na maarifa. Suala la kutafuta elimu limetiliwa mkazo sana katika Uislamu unaowahutubu mwanamke na mwanaume kwa kiwango sawa, na kamwe dini hiyo kubwa na adhimu haiioni jinsia ya mtu kuwa ni kikwazo katika njia ya kutafuta elimu. Mfasiri mkubwa wa Qur'ani wa zama hizi Allamah Muhammad Tabatabai anasema katika tafsiri ya al Mizan baada ya kuzungumzia historia ya kusikitisha ya wanawake kwamba: Katika dini ya Uislamu mwanamke anashirikiana na mwanaume katika hukumu zote za kiibada na sheria za kijamii, na katika kila jambo ambapo mwanaume amepewa uhuru na kujitawala kama katika masuala ya urithi, kutafuta mali na pato, katika miamala ya aina mbalimbali, kufafuta elimu, kulinda haki na kadhalika, mwanamke pia anajitegemea isipokuwa katika masuala yanayopingana na tabia ya maumbile yake.
Uislamu umewalazimisha wanadamu wote, mwanamke na mwanaume, kutafuta elimu na ujuzi, na Mtume wetu Muhammad (saw) anasema: Kutafuta elimu ni wajibu kwa kila Mwislamu mwanaume na mwanamke. Mwenyezi Mungu mtukufu pia anawakemea majahili na watu wasio na elimu, na aya nyingi za Qur'ani Tukufu zinawahimiza wanadamu wote bila ya kujali jinsia zao, kujipamba kwa elimu na maarifa. Aya ya 11 ya Suratul Mujadila inasema: Mwenyezi Mungu atawainua daraja walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu...". Kwa utaratibu huo wanawake kama walivyo wenzao wanaume, wanaweza kukwea daraja za juu za elimu na maarifa na kutoa uzoefu wao kwa jamii ya mwanadamu.