Mar 15, 2016 10:19 UTC
  • Ufeministi, Itikadi na Misingi Yake (24)

Ni wakati mwingine wa kuwaletea sehemu ya 24 ya kipindi cha Ufenimisti, Itikadi na Misingi Yake. Katika kipindi cha wiki iliyopita tulitupia jicho mitazamo ya baadhi ya wasomi wa Magharibi wanaosema kuwa mitazamo ya kifeministi ni hadaa na uongo. Leo tutatupia jicho juhudi za mafenimisti za kulazimisha mitazamo yao katika mikataba na makubaliano ya kimataifa.

Miongoni mwa taathira za ufenministi kama wimbi la kifikra katika ulimwengu wa sasa ni kupasishwa maazimio na mikataba mbalimbali kubwa zaidi ukiwa Mkataba wa Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake.

Inatupasa hapa kuashiria kwamba, hadi kufikia muongo wa 1960 suala la usawa na uhuru wa wanawake lilikuwa halijawekwa katika mikataba ya kimataifa kama suala linalojitegemea. Mwaka 1963 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitaka kamati ya Hadhi ya Mwanamke na Baraza la Uchumi na Masuala ya Kijamii kubuni na kuandika utangulizi wa Mkataba wa Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake na mkataba huo ulipasishwa mwaka 1967.

Mwaka 1975 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitaka kamati ya hadhi ya mwanamke kukamilisha Mkataba wa Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake. Kwa msingi huo mwaka huo umetambuliwa kuwa ni mwaka wa kimataifa wa Mwanamke na tarehe 8 Machi imetambuliwa kuwa ni siku ya Kimataifa ya Mwanamke. Vilevile kipindi cha kuanzia mwaka 1976 hadi 1985 kimetambuliwa kuwa ni muongo wa mataifa kwa ajili ya wanawake. Hatimaye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 18 Disemba mwaka 1979 lilipasisha Mkataba wa Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake kwa lengo la kuweka sheria na kanuni sawa zinazohusiana na masuala ya wanawake katika nchi mbalimbali na kukamilisha usawa baina ya mwanamke na mwanaume.

Mkataba wa Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake una utangulizi na vifungu 30. Katika kifungu chake cha kwanza kumetajwa kuwa 'kutokomeza ubaguzi dhidi ya wanawake' ni kufuta aina zote za ubaguzi, tofauti na vizuizi kwa mujibu wa jinsia. Kifungu cha pili hadi 16 vya mkataba huo pia vinasisitiza usawa katika kila kitu baina ya wanawake na wanaume. Nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Mataifa hazijakubali mkataba huo. Kwa msingi huo nchi nyingi za Waislamu zimejiepusha kujiunga na mkataba huo kutokana na vipengee vyake kupingana na sheria za Uislamu na hata baadhi ya nchi zisizo za Waislamu kama Marekani ambazo zimetia saini mtakaba huo hadi sasa hazijajiunga nao.

Mkataba wa Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake unakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na kwamba unatawaliwa na roho na mitazamo ya kifeministi na umezusha mijadala mingi katika duru mbalimbali za kidini na kimataifa. Baadhi ya wanadharia wanasema kuwa kuporomoka kwa misingi ya familia na kufifia na kunyauka maadili katika jamii mbalimbali hususan zile zilizoanza kutekeleza mada za mkataba huo ni ishara za kufeli kwake. Hii ni kutokana na kwamba miongoni mwa vigezo vinavyotawala mkataba huo ni suala la usawa wa aina zote na mfanano kamili wa kisheria baina ya mwanamke na mwanaume. Vigezo hivi kimsingi vimepuuza nafasi ya mke na mama ya mwanamke na kuwa sababu ya kutetereka misingi na nguzo za familia, kupanda juu umri wa kuoa na kuolewa, kupungua umri wa mahusiano haramu na kadhalika.

Vilevile sifa nyingine za mkataba huo ni kuweka mbele sheria na kanuni kavu sambamba na kupuuza na kutupilia mbali masuala ya kidini, kimaadili na kiutamaduni. Kwa mfano tu mkataba huo haukuzungumzia lolote au kutunga sheria ya aina yoyote kuhusu ufuska na utovu wa maadili katika maingiliano haramu.

Tumesema kuwa baadhi ya vipengee vya mkataba huo vinapingana na sheria za Kiislamu, maadili na sheria za nchi mbalimbali. Kwa msingi huo nchi nyingi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu hazikujiunga na mkataba huo au zimeukubali kwa masharti. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imekataa baadhi ya vipengee vyake hususan kipengee nambari moja hadi 16 vya mkataba huo. Hii ni kutokana na kwamba, vipengee hivyo vinapingana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu, sheria za Kiislamu na Katiba ya Iran. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu imempa mwanamke nafasi aali na ya juu kutokana na hadhi yake na nafasi yake kubwa katika fikra na mfumo wa Uislamu. Katiba hiyo imezingatia sana haki za wanawake za kushirikishwa katika masuala ya utawala na shughuli za kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa mujibu wa misngi na sheria za Uislamu. Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu inasisitiza kuwa mwanamke si wenzo bali ana nafasi aali na tukufu kwa kuzingatia wadhifa wake mkubwa wa mama na nafasi yake adhimu katika familia.

Hivyo basi inaeleweka kwamba, upinzani wa nchi za Kiislamu dhidi ya Mkataba wa Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake zaidi ni kwa sababu ya vipengee vyake kupingana na itikadi na maslahi ya kitaifa na kidini ya nchi hizo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wakati nchi yoyote inapotaka kujiunga na mkataba wowote huchunguza na kutaka kujua kwamba, je, una maslahi ya kwa taifa na nchi husika au la? Je unapingana na itikadi, maadili na thamani za nchi na taifa hilo? Ni wazi kuwa, baadhi ya vipengee vya mkataba huo vinapingana waziwazi na mfumo wa kifikra na itikadi zinazotawala katika nchi nyingi za Kiislamu. Hata hivyo kutokana na kuwa misingi ya kifikra inayotawala nchi za Magharibi na baadhi ya jumuiya za kimataifa imetokana na fikra za kiliberali, mada kuu za mkataba huo zimekubaliwa na nchi hizo.

Miongoni mwa dosari na kasoro kubwa za Mkataba wa Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake ni kwamba unateteresha misingi na nguzo za familia. Mkataba huo unawatambua mwanamke na mwanaume kuwa ni viumbe wanaojitegemea kila mmoja na kwamba kila mmoja wao hamuhitajii mwenzake. Mtazamo huu unaondoa au kupunguza majukumu na nyadhifa za kila mmoja wao mkabala ya mwenzake na kudhoofisha misingi na nguzo za familia.

Vilevile inatupasa kutambua kuwa, asili ya kuwatambua mwanaume na mwanamke kuwa ni sawa na wanafanana katika kila kitu na kupuuza tofauti zao za kijinsia na kimaumbile imetolewa katika utamaduni wa kisekulari na mitazamo ya humanism ya Magharibi inayotanguliza matakwa ya binadamu kuliko dini na sheria za Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo kwa kuwa wanadharia wa fikra ya usawa baina ya mwanamke na mwanaume wa Magharibi wamekosea katika kutambua hakika ya viumbe hao wawili na nafasi na mchango wao halisi katika mfumo wa maumbile, hawakuweza kulinda na kuchunga uadilifu baina ya jinsia hizo mbili.

Ukweli ni kuwa mwanamke katika nchi za Magharibi amedhurika zaidi na kaulimbiu na nara ya kufanana jinsia mbili za kike na kiume. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwa kutumia kisingizio cha usawa baina ya mwanamke na mwanaume, majukumu ya nyumbani yamegawanywa kwa usawa baina ya mwanamke na mwanaume bila ya kujali na kutilia maanani sifa za kinafsi na kimaumbile za kila mmoja wao. Suala hilo limewalazimisha wanawake kuhujumu masoko ya kazi na ajira kwa ajili ya kupata hadhi ya kijamii, suala ambalo kwa upande wake limewafanya wanawake wapate sulubu na mashaka makubwa ya kimwili na kinafsi kuliko hata wanaume.

Tutaendelea na maudhui hii katika kipindi cha wiki ijayo.

Tags