Mar 15, 2016 10:25 UTC
  • Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (22)

Katika vipindi vilivyotangulia tulinukuu maneno ya baadhi ya wataalamu waliosema kuwa japokuwa ufeministi umekuwa na baadhi ya matunda katika uwanja wa kutetea haki za wanawake kama kuwashirikisha katika masuala ya kisiasa na kijamii lakini ukweli ni kuwa mafanikio hayo bado ni machache sana ikilinganishwa na hasara na madhara yaliyosababishwa na fikra za kifeministi kwa wanawake. Kipindi cheti leo kitatupia jicho athari mbaya za ufeministi.

Miongoni mwa athari mbaya za ufeministi ni kuongezeka kwa vitendo vya kubakwa wanawake na ukatili dhidi ya watu wa jinsia hiyo katika nchi za Magharibi. Mahudhurio makubwa na yasiyo na mpaka ya wanawake katika jamii kama unavyohimiza ufeministi, na kuenea kwa utamaduni wa uhuru wa maingiliano ya ngono vimetayarisha mazingira ya maingiliano yasiyo ya kisheria ya kingono baina ya wanaume na wanawake. Kwa mfano tu uchunguzi uliofanywa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon umebaini kuwa, asilimia 61 kati ya wanawake elfu 47 wanaohudumu katika jeshi la Marekani wamefanyiwa unyanyasaji wa kingono. Kashfa hiyo inaonesha athari mbaya za wito wa kuwepo usawa wa aina zote baina ya wanawake na wanaume na mijumuiko isiyo na mpaka kati ya jinsia hizo mbili.

Kubadilishwa kwa vigezo na nafasi za kila mmoja kati ya wanawake na wanaume ni miongoni mwa matokeo ya mitazamo ya ufeministi katika nchi za Magharibi. Hapana shaka kuwa harakati eti ya kutetea haki za wanawake ya ufeministi na wanafikra wanaounga mkono fikra za harakati hiyo wamezusha hali ya mparaganyiko na ukosefu wa nidhamu katika utamaduni wa kazi na harakati za jinsia hizo mbili za wanadamu. Jambo hilo limekuwa sababu ya kutokomezwa sifa za mwenendo wa kawaida wa mwanadamu kwa kadiri kwamba kila siku idadi kubwa ya wanawake huvutiwa na mienendo ya kupenda kuhujumu na ya kikatili ambayo kwa kawaida huonekana zaidi baina ya wanaume. Wakati huo huo wanaume vijana wanaonekana wakijielekeza zaidi kwenye masuala ya kianakike kama masuala ya mitindo, kuremba mwili, kujikwatua na kadhalika. Mwandishi Phyllis Schlafly wa huko Magharibi amekosoa vikali jambo hilo na kusisitiza kuwa: Njia pekee ya kumuwezesha mwanamke kupata nguvu yake halisi ni kutumia sifa chanya za ukamilifu na wala si kujivika utambulisho bandia wa kianaume unaoainishwa na mafeministi.

Miongoni mwa taathira mbaya za ufeministi ni kuzusha mpambano baina ya mwanamke na mwanaume. Kupuuzwa kwa tofauti za kila mmoja kati ya jinsia ya kike na ya kiume ambazo zinawafanya wawili hao wakamilishane kumekuwa sababu ya mafeministi kumpa mwanaume taswira ya kiumbe katili na kinachopenda kudhibiti jinsia nyingine ambacho kuna udharura wa mwanamke kupambana nacho ili kutetea haki zake za kihistoria. Suala hilo pia limemchochea mwanaume kuchukua hatua kama hiyo na kukabiliana na jinsia ya kike.

Mwandishi Christina Hoff Sommers wa Marekani anasema: Fikra za mafeministi zimeleta tashwishi katika fikra za watu na zimewafanya wanawake na wanaume kuwa askari wenye taasubi na chuki kwa ajili ya vita vya kijinsia kutokana na kueneza chuki baina ya jinsia hizo mbili. Mtazamo huu wapenzi wasikilizaji unatofautiana sana na wa Kiislamu unaotambua maisha ya mume na mke kuwa ni sawa na vazi zuri na la kupendeza linalositiri na kuficha aibu na nakisi za kila mmoja wao. Aya ya 187 ya Suratul Baqara inasema: “Wao (yaani wake zenu) ni vazi lenu na nyinyi ni vazi lao…” Katika fikra za Kiislamu kila mmoja kati ya wawili hao yaani mke na mume, ana nafasi muhimu katika kuongoza familia.

Kubadilishwa kwa mfumo wa masuala ya kiroho na kimaadili ndani ya familia ni miongoni mwa taathira mbaya za ufeministi katika jamii za Magharibi. Sisitizo kupita kiasi juu ya masuala ya haki za kijamii, kisiasa na kiraia na kupewa kipaumbele masuala ya uchumi sambamba na kutupilia mbali maadili, kudunisha taasisi ya familia na kudharau wadhifa wa mama na mke ndani ya familia, vimesababisha hasara kubwa isiyoweza kufidika. Miongoni mwa matokeo mabaya ya kubadilika kwa mfumo wa maadili na kuyumba kwa familia ni kupungua kwa ndoa na kukithiri talaka, kudhoofika kwa misingi ya familia ya athari zake mbaya katika jamii na vilevile kukithiri ufuska na uasherati.

Donald Brenzly ambaye ni mhadhiri wa taaluma na tiba ya magonjwa ya akili katika Chuo Kikuu cha Kansas huko Marekani anasema: “Kila kitu kinachosababisha kudhoofika familia hatimaye hudhoofisha pia jamii”. Kuhusu hali ya sasa ya jamii ya Magharibi, mtaalamu huyo anaandika kwamba: Thamani za kiutamaduni, ada na maadili vinafifia siku baada ya siku. Utumiaji wa dawa za kulevya, ukatili, vitendo vya jinai, usaliti na kujiua baina ya vijana, mimba za haramu, kutoa mimba na kadhalika vimeenea sana..”

Kuwavua wanaume na kina baba majukumu ya kukimu na kudhamini mahitaji ya familia na kuwasukuma wanawake makazini kumemfanya mwanamke kuwa maskini zaidi kutokana na uwezo wake mdogo wa kimwili kwa ujumla ukilinganishwa na wa mwanaume. Mbali na hayo tunapaswa pia kutilia maanani matatizo yanayomkubwa mwanamke katika mazingira ya kazi na madhara yanayompata kutokana na uwezo wake mdogo wa kimwili na kutoweza kufanya kazi nzito na kudunishwa na wafanyakazi wenzake wa kiume.

Vilevile makundi ya kisiasa yamekuwa yakitumia vibaya mitazamo ya kifeministi, suala ambalo limesababisha matatizo mengi katika jamii. Harakati ya mafeministi kama zilivyo harakati nyingine zinazotaka kufanya mageuzi, imetumiwa vibaya na madola makubwa. Katika nchi za Magharibi mafeministi wamekuwa chombo kinachotumiwa na vyama vya siasa kwa ajili ya malengo yao. Vyama hivyo vinatumia maandamano ya wanawake katika propaganda zao na wagombea wa vyama hivyo wamekuwa wakitoa ahadi kemkem kwa wanawake kwa lengo la kujaza masanduku yao ya kura na si kwa sababu ya kutetea haki za wanawake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mitazamo ya vyama vingi vya siasa vya Magharibi ni mitazamo ya kibepari inayojali na kutanguliza mbele maslahi ya kiuchumi. Katika upande mwingine madola ya kibeberu yanatumia fikra za kifeministi katika siasa zao za nje kama wenzo wa kuzishinikiza nchi mbalimbali hususan za Kiislamu. 

Tags