May 10, 2024 07:25 UTC
  • Uganda: Tunahitaji teknolojia ya Iran kudhibiti maudhui chafu, potofu mitandaoni

Serikali ya Uganda inatafakari kuanza kutumia teknolojia iliyopiga hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kudhibiti maudhui chafu na za upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii.

Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Dakta Chris Baryomunsi, Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Muongozo wa Taifa wa Uganda katika mkutano wake na ujumbe wa ngazi za juu wa Iran mjini Kampala na kusisitiza kuwa: Lengo si kufunga mitandao ya kijamii, bali ni kushajiisha maudhui safi na uwajibikaji mitandaoni.

Amesema kwa ujumla teknolojia ni kitu kizuri, lakini tatizo ni kuwa baadhi ya watu wanatumia vibaya mitandao ya kijamii na kueneza maudhui chafu na za upotoshaji, na zenye taathira hasi hata wa watoto wadogo.

Waziri wa ICT na Muongozo wa Taifa wa Uganda amebainisha kuwa, serikali ya Kampala imekuwa ikitafuta njia ya kudhibiti utumiaji mbaya wa mitandao ya kijamii, na ingependa kustafidi na teknolojia ya Iran kuzuia usambazaji wa habari bandia na za upotoshaji, ponografia na lugha chafu mitandaoni.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Iran aliyeongoza ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu mjini Kampala amesema Tehran ipo tayari kuipa Uganda uzoefu wake katika ustawi wa teknolojia.

Mapema mwezi huu wa Mei, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran alitangaza utayarifu wa taifa hili wa kushirikiana na Uganda katika miradi ya mawasiliano na teknolojia ya habari na uhamishaji wa taaluma hiyo kwa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Issa Zarepour alisema hayo hapa Tehran katika mazungumzo yake na Rukia Isanga Nakadama, Naibu Waziri Mkuu wa Uganda aliyekuwa safarini hapa nchini na kusisitiza kuwa, Iran inajitahidi kuendeleza diplomasia ya kiuchumi katika bara la Afrika.

Tags