WHO: Mkataba wa majanga wakwama kuidhinishwa
Nchi 194 wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) zimeshindwa kuafikiana juu ya mkataba uliotafutwa kwa muda mrefu wa kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na majanga.
Lengo lililokusudiwa la kile kinachoitwa 'mkataba wa majanga' ni kuidhinishwa wakati wa Kongamano la Afya Duniani mwaka huu, ambalo ndilo chombo kikuu cha maamuzi cha WHO. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Mei.
Duru ya hivi karibuni ya mazungumzo ilianza karibu wiki mbili zilizopita huko Geneva nchini Uswisi na yalielezwa kuwa msukumo wa mwisho wa WHO wa kupata mwafaka juu ya rasimu ya makubaliano iliyoko.
Lakini baada ya miaka miwili ya mazungumzo, wanachama hao wa WHO, walishindwa kuafikiana kuhusu rasimu hiyo kufikia muda wa mwisho wa jana Ijumaa.
Mojawapo ya masuala yenye utata imekuwa ni iwapo na jinsi gani makampuni ya dawa yanapaswa kulazimika kuelezea utaalamu na kuwezesha sehemu ya bidhaa zao kupatikana kwa nchi maskini.
Tedros Adhanom Ghebreyesus Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) alikuwa ameyataka mataifa ya dunia kuridhia makubaliano ya kusaidia kupambana na miripuko ya magonjwa katika siku za usoni, ikiwa ni baada ya athari kubwa za janga la Covid-19.
Inaelezwa kuwa, nchi za dunia zinatakiwa kukamilisha haraka mchakato wa mazungumzo kuhusiana na makubaliano hayo ifikapo tarehe 10 ya mwezi huu wa Mei, kwa minajili ya kuipitisha katika mkutano wa kila mwaka wa Shirika la Afya Duniani (WHO) baadae mwezi huu, lakini vyanzo vinavyohusika vinasema kuwa, bado kuna tofauti kubwa zilizosalia ambazo zinapaswa kumalizwa na kuandaa mazingira ya kufikiwa makubaliano hayo.