Feb 25, 2019 04:17 UTC
  • Jumatatu, tarehe 25 Februari, 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 19 Jumadithani 1440 Hijria sawa na 25 Februari 2019.

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita Mzayuni mmoja aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada aliwashambulia na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim mjini al Khalil, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi 29 miongoni mwao. Mauaji hayo yalitokea wakati Waislamu hao walipokuwa katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kikatili. Mauaji hayo ambayo yalidhihirisha tena uhasama na chuki za Wazayuni wa Israel dhidi ya Waislamu, yalilaaniwa na Waislamu kote duniani. Ukatili huo ulizusha wimbi kubwa la machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambapo wananchi walizidisha mapambano dhidi ya maghasibu wa Tel Aviv. Israel ilimshika kwa muda na kumuachia huru mhalifu huyo katili kwa kisingizio kwamba alikuwa punguani!

Mji wa al Khalil, Palestina inayokaliwa kwa mabavu

Tarehe 25 Februari miaka 33 iliyopita dikteta wa zamani wa Ufilipino aliyekuwa amejitangaza rais wa maisha, Ferdinand Marcos, alikimbia nchi hiyo akiwa pamoja na familia yake. Marcos alichukua hatamu za uongozi mwaka 1965. Alidumisha utawala wake wa kidikteta na ukandamizaji nchini Ufilipino kwa himaya na uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani. Mwaka 1973 Ferdinand Marcos alijitangaza kuwa rais wa maisha wa Ufilipino. Wakati huo wananchi katika maeneo mbalimbali walikuwa tayari wameanzisha harakati za mapambano ya kisiasa na kijeshi dhidi ya dikteta huyo. Mapambano hayo yalishika kasi zaidi katikati ya mwongo wa 1980, na Februari 25 1986 Marcos alilazimika kukimbia Ufilipino.

Ferdinand Marcos

Katika siku kama hii ya leo miaka 35 iliyopita ndege za kivita za utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein zilishambulia miji ya Saqz, Pol-e Dokhtar na Mahabad. Utawala wa Saddam Hussein uliamua kushambulia makazi ya raia katika miji mbalimbali ya Iran sambamba na ushindi mkubwa wa wapiganaji wa Kiislamu hususan katika operesheni ya jeshi la Iran iliyopewa jina la Khaibar na kipigo cha jeshi la Iraq katika visiwa vya Majnun. Makumi ya raia waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.

Na siku kama ya leo miaka 266 iliyopita tabibu mmoja wa Uingereza aligundua njia ya kutibu maradhi ya Ascorbate. Maradhi hayo husababishwa na upungufu wa vitamini C mwilini na kulegeza fizi za meno na hatimaye meno huanza kudondoka na kutokwa na damu nyingi wakati wa majeraha madogomadogo. Kwa kuwa zamani wafanyakazi wa vikosi vya majini na wahudumu wa meli na mabaharia ambao hawakuwa na uwezo wa kupata matunda na mboga walikuwa wakipatwa kwa wingi na maradhi hayo, ugonjwa huo ulikuja kujulikana kwa jina la ugonjwa wa mabaharia.