Ijumaa, tarehe 8 Machi, 2019
Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Rajab 1440 Hijria, sawa na Machi 8, 2019.
Leo ni tarehe Mosi Rajab, mwezi uliojaa rehema na fadhila tele. Mwezi huu na miezi miwili inayofuata yaani Sha’aban na Ramadhan ni kipindi muhimu kwa ajili ya kujisafisha mwanadamu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kuhusiana na mwezi huu wa Rajab, Mtume Muhammad (SAW) amesema: “Mwezi wa Rajab ni mwezi mkubwa wa Mwenyezi Mungu…kupigana vita na makafiri ndani ya mwezi huu ni haramu. Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, Sha’aban ni mwezi wangu na Ramadhan ni mwezi wa umma wangu.” Kufunga Saumu katika mwezi huu kumesisitizwa sana na kuna thawabu nyingi. Baadhi ya hadithi zimesisitiza sana kufunga Saumu na kuomba maghfira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mwezi huu. Katika mwezi huu kuna matukio mawili muhimu. Tukio la kwanza ni kuzaliwa Imam Ali (as) tarehe 13 ya mwezi huu na tukio la pili ni kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad (saw) tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab.

Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu kutoka katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa.

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, inayosadifiana na 8 Machi 1968 ilianza Harakati ya Ukombozi ya Moro dhidi ya utawala wa dikteta Ferdinand Marcos nchini Ufilipino. Dikteta Marcos alikuwa mshirika na muitifaki mkubwa wa Marekani na katika utawala wake wa kidikteta, maelfu ya Waislamu wa Ufilipino waliuawa au kufungwa jela. Harakati ya Ukombozi ya Moro ilipambana kwa ajili ya kupigania haki za Waislamu, na ilihesabiwa kuwa harakati kubwa zaidi iliyopinga utawala wa Marcos nchini Ufilipino. Baada ya Marcos kuondoka madarakani mwaka 1986, harakati ya Moro ilikubali kutia saini makubaliano ya amani na serikali ya Manila.
Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Machi 1985, ulitokea mlipuko mkubwa wa bomu la kutegwa garini mjini Beirut, Lebanon ambapo watu wasiopungua 45 waliuawa na wengine 175 kujeruhiwa. Mlipuko huo ulitokea karibu na msikiti unaotumiwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mlipuko huo ulifuatilia mlipuko mwengine mkubwa zaidi uliotokea mwaka 1983, ambapo watu wasiopungua 61 waliuawa kusini mwa bandari ya Tyre, nchini Lebanon.
Leo tarehe 8 Machi inatambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Mwanamke. Awali siku hii ilianzishwa kama tukio la kisiasa la kisoshalisti lakini baadaye liliingia katika utamaduni wa nchi nyingi duniani. Siku ya Kimataifa ya Mwanamke inayoadhimishwa katika nchi nyingi duniani imepoteza sura yake ya kisiasa na sasa limekuwa tukio linalotumiwa na wanaume kudhihirisha upendo wao kwa wanawake. Mwaka 1977 Umoja wa Mataifa iliitangaza rasmi siku hiyo kama Siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa.