Mar 10, 2019 01:15 UTC
  • Jumapili tarehe 10, Machi, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 3 Rajab 1440 Hijria, sawa na tarehe 10 Machi, 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1186 iliyopita, yaani tarehe 3 Rajab mwaka 254 Hijria, Imam Ali Naqi al-Hadi (as), mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Imam Ali Naqi al-Hadi (as) alizaliwa mwaka 212 Hijiria katika mji mtakatifu wa Madina. Alikua na kulelewa na baba yake, yaani Imam Jawad (as). Imam Ali al-Hadi alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake. Aidha Imam Ali al Hadi alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufundisha, kulea wanafunzi na kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Uislamu. Mapenzi ya watu kwa Imam Hadi kwa upande mmoja na elimu aliyokuwa nayo kwa upande wa pili, ni mambo yaliyowafanya watawala wa wakati huo wa ukoo wa Bani Abbas waingiwe na husuda, na ndio maana wakapanga njama ya kumuua shahidi Imam huyo na kuitekeleza katika siku kama ya leo.

Siku kama ya leo miaka 1052 iliyopita alifariki dunia Abul-Wafa Muhammad Bin Yahya Buzjani, mwanahisabati, mtaalamu wa nyota na mmoja wa wasomi wakubwa wa Iran na wa ulimwengu wa Kiislamu. Buzjani alizaliwa mwaka 328 Hijiria karibu na mji wa Nishapur au Nishabur, kaskazini mashariki mwa Iran na kutokea kuwa mwanahisabati na mtaalamu mkubwa wa nyota wa zama zake. Athari zake ziliendelea kutumiwa na makadhi na wanahistoria wa baada yake. Kwa kuzingatia kuwa Abul-Wafa Muhammad Bin Yahya Buzjani aliishi kipindi kimoja na Abū Rayān Biruni, msomi mkubwa wa zama zake, hivyo alikuwa akibadilishana naye mawazo katika elimu hizo. Msomi huyo ameacha nyuma athari tofauti. Kitabu cha 'A'amal al-Handasah' na 'Taarikh Ilmul-Hisab' ni moja ya vitabu vya Abul-Wafa Muhammad Bin Yahya Buzjani.

Abul-Wafa Muhammad Bin Yahya Buzjani

Siku kama ya leo miaka 971 iliyopita, alifariki dunia Abul-Hassan Twahir Bin Ahmad Ibn Babshad Misri, mmoja wa wasomi wakubwa wa elimu ya fasihi wa karne ya tano Hijiria. Awali alijishughulisha na biashara, huku akiachana na kazi hiyo na kuanza kutafuta elimu na hivyo akaelekea nchini Iraq kimasomo. Baada ya kuhitimu masomo yake nchini Iraq alirejea Misri na kujishughulisha na masuala ya kiutamaduni na kijamii nchini humo. Baada ya muda fulani aliamua kujitenga na watu na kufariki dunia katika siku kama ya leo.

Abul-Hassan Twahir Bin Ahmad Ibn Babshad Misri

Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita, yaani tarehe 10 Machi mwaka 1876 Miladia, mvumbuzi wa Kimarekani Alexander Graham Bell alivumbua simu na siku hiyo hiyo akafanya mazungumzo ya kwanza ya majaribio ya simu na msaidizi wake Thomas Watson. Uvumbuzi huo wa simu ulileta mabadiliko makubwa katika vyombo vya mawasiliano. Bell alifaidika na uzoefu na majaribio ya wahakiki na wavumbizi wengine katika kutengeneza chombo hicho cha mawasiliano ya haraka. Baada ya hapo chombo cha simu kiliboreshwa na kufikia kiwango cha sasa kwa kukamilishwa kazi iliyofanywa na Alexander Graham Bell.

Alexander Graham Bell

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ndege za kivita za Marekani zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji mkuu wa Japan, Tokyo. Mashambulizi hayo makubwa yalizishirikisha mamia ya ndege kubwa za kurusha mabomu za Marekani zilizomimina mabomu kwa mara kadhaa katika mji mkuu wa Japan. Mamia ya raia wa nchi hiyo waliuawa katika mashambulizi hayo.

Mashamblizi makali katika mji wa Tokyo, Japan

Na siku kama ya leo miaka 34 iliyopita alifariki dunia Konstantin Ustinovich Chernenko, kiongozi wa zamani wa Urusi ya Zamani. Alizaliwa tarehe 24 Septemba mwaka 1911 Miladia katika familia ya kawaida na ya kijijini maeneo ya Siberia ambapo baada ya kuhitimu masomo yake na akiwa na umri wa miaka 18 alijiunga na idara ya vijana ya chama cha Ukomonisti, huku akiwa mwanachama rasmi miaka miwili baadaye. Kwa kipindi cha miaka 20 alikuwa mjumbe wa ngazi ya juu wa ofisi ya kisiasa wa chama cha Ukomonisti wa Urusi ya zamani na baada ya hapo akateuliwa kuwa katibu Mkuu. Aidha katika kipindi chote cha utawala wa Leonid Ilyich Brezhnev alikuwa akiandamana na Konstantin Ustinovich Chernenko na ni kwa ajili hiyo ndipo Wamagharibi wakamwita Chernenko kuwa ni kivuli cha Brezhnev. Baadaye alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo na kufanikiwa kuongoza kwa kipindi cha miezi 13 na kufariki dunia katika siku kama ya leo mwaka 1985 akiwa na umri wa miaka 74. Ni baada ya kufariki dunia ndipo akachaguliwa Mikhail Sergeyevich Gorbachev, kiongozi wa mwisho wa Urusi ya zamani.

Konstantin Ustinovich Chernenko