Mar 14, 2019 02:32 UTC
  • Alkhamisi tarehe 14 Machi 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 7 Rajab 1440 Hijria sawa na Machi 14 mwaka 2019.

Katika siku kama ya leo miaka 140 iliyopita, alizaliwa nchini Ujerumani Albert Einstein, msomi mashuhuri wa fizikia na hisabati. Mnamo mwaka 1921 msomi huyo mahiri alipewa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia, baada ya kufanya juhudi kubwa za kiutafiti. Utafiti na nadharia za Einstein katika uwanja wa nyuklia zilikuwa na taathira kubwa duniani. Hata hivyo Einstein alisikitika sana baada ya kugundua kwamba, uchunguzi na utafiti wake umetumiwa na baadhi ya nchi kwa ajili ya kutengeneza silaha hatari za nyuklia. Albert Einstein alifariki dunia mwaka 1955.

Albert Einstein

Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita alifariki dunia Karl Heinrich Max mwanafalsafa wa Kijerumani na mwasisi wa nadharia ya Umaksi. Karl Max aliyezaliwa katika familia ya Kiyahudi alisomea sheria na baadaye historia na falsafa. Kwa muda fulani mwanafalsafa huyo wa Kijerumani alikuwa mkuu wa jarida moja na mwaka 1848 alishirikiana na mwanafalsafa mwenzake wa Kijerumani na kubainisha imani, maoni na mitazamo yake katika kitabu walichokiandika na kukipa jina la "Manifesto ya Ukomonisti." Miaka miwili baadaye Max alibaidishwa kutokana na kujishughulisha na harakati za kisiasa.

Karl Max

Miaka 65 iliyopita katika siku kama hii ya leo yaani mnamo mwaka 1954 tarehe 14 mwezi Machi vilianza vita vya kihistoria na vikubwa vilivyojulikana kwa jina la vita vya" Dien Bien Phu" ambavyo viliainisha mustakbali wa wanajeshi wa kikoloni wa Ufaransa huko Indochina. Katika vita hivyo wapiganaji wa Viet Minh waliokuwa wakipigania uhuru wa Vietnam walikuwa wakipambana na jeshi la kikoloni la Ufaransa lililokuwa katika ngome ya Dien Bien Phu. Hatimaye tarehe 7 mwezi Mei vita hivyo vilimalizika kwa kusalimi amri kamanda wa jeshi al Ufaransa katika ngome imara ya Dien Bien Phu na kupata ushindi wapiganaji wa Viet Minh. Ushindi huo ulihitimisha utawala wa kikoloni wa Ufaransa nchini Vietnam.

Vita vya" Dien Bien Phu"

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita sawa na tarehe 23 Esfand 1340 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abul Qassim Kashani, mwanachuoni na shakhsia maarufu wa kisiasa katika historia ya Iran. Ayatullah Kashani alifanikiwa kupata daraja la ijtihadi akiwa bado barobaro huko Najaf nchini Iraq lakini baadaye alifukuzwa nchini humo kutokana na misimamo yake ya kupinga ukoloni wa Uingereza. Aliporejea nchini Iran, Ayatullah Kashani aliendelea na misimamo yake ya kupambana na ukoloni wa Uingereza na kufungwa jela mara kadhaa. Baada ya kutoka jela wananchi wa Tehran walimchagua kuwa mwakilishi katika Bunge la Taifa.  

Ayatullah Sayyid Abul Qassim Kashani

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita yaani tarehe 14 Machi 1978, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianza kuivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Lebanon kwa kisingizio cha kukabiliana na operesheni iliyofanywa na wanamapambano wa Kipalestina pambizoni mwa Tel Aviv. Katika mashambulio hayo jeshi la Israel liliua raia wengi wasio na hatia wa Lebanon na Palestina na kuikalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Lebanon. Hata hivyo utawala huo ghasibu uliondoka kwa fedheha katika maeneo ya kusini mwa Lebanon mwaka 2000 baada ya kupata kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano shupavu wa Harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah na kuondoka kwenye eneo hilo.

Uvamizi dhidi ya ardhi ya Lebanon