Mar 20, 2019 02:30 UTC
  • Jumatano, Machi 20, 2019

Leo ni Jumatano tarehe 13 Rajab 1440 Hijria sawa na tarehe 20 Machi 2019 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1463 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa katika nyumba tukufu ya al Kaaba, Ali bin Abi Twalib AS, ambaye ni binamu, mkwe na Khalifa wa Mtume Muhammad (saw). Mama wa mtukufu huyo ni Bibi Fatima bint Assad na baba yake ni Abu Talib. Katika kipindi chake cha utotoni, Ali bin Abi Talib alilelewa na kupata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu SAW, na alikuwa mwanaume wa kwanza kuukubali Uislamu. Mwishoni mwa mwaka wa Pili Hijria, Imam Ali AS alimuoa Bibi Fatimatul Zahra binti ya Mtume Mtukufu SAW. Imam Ali AS alishiriki kwenye vita vyote bega kwa bega na Mtume Mtukufu SAW isipokuwa vita vya Tabuk, na alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume katika hali zote za shida na matatizo. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji asiye na mithili, lakini Imam Ali bin Abi Talib alikuwa mpole, mwingi wa huruma na mtetezi wa wanyonge.

Miaka 1161 iliyopita katika siku kama ya leo mwaka 279 Hijria, alifariki dunia Abu Isa Tirmidhi hafidh wa Qur'ani Tukufu na mpokeaji hadithi mashuhuri wa Kiislamu. Tirmidhi alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa miaka mingi kwa ajili ya kujipatia elimu ya dini na hadithi. Alikuwa miongoni wma wanafunnzi hodari wa Imam Bukharin na kitabu chake maarufu zaidi Jamiu Tirmidhi. Kitabu hicho kinahesabiwa kuwa miongoni mwa marejeo muhimu ya hadithi katika madhehebu ya Suni.

Tarehe 20 Machi miaka 292 iliyopita, alifariki dunia Isaac Newton mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 84. Alizaliwa mwaka 1643 na kusoma katika Chuo Kikuu cha Cambridge. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy.

Isaac Newton

Miaka 55 iliyopita katika siku kama ya leo, Imam Khomeini mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa hotuba na kuwataka wananchi wa Iran wasifanye sherehe za Nairuzi za mwaka mpya wa Kiirani wa 1342 ili kulalamikia hatua zisizo za kisheria za utawala wa kifalme wa Kipahlavi. Nairuzi ni sherehe za kitaifa za Wairani ambazo hufanywa kila mwanzoni mwa mwaka wa Kiirani. Katika kipindi chote cha mwaka 1341 Hijria Shamsia utawala wa kidikteta wa Shah ulichukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha misingi ya utawala wake na kwa ajili ya kuyaridhisha madola ya kigeni hususan Marekani. Imam Khomeini kwa uono mpana na kutazama mustakbali wa mambo akiwa pamoja na maulama wengine aliitangaza sikukuu ya Nairuzi kuwa mambolezo ya umma ili kubatilisha propaganda za utawala wa Kipahlavi za kuhalalisha hatua zake za hiana. Kwa muktadha huo, wananchi na viongozi wa kidini walifanya vikao vya maombolezo katika pembe mbalimbali za Iran. Ubunifu huu wa Imam Khomeini ulikuwa na taathira kubwa kiasi kwamba, katika siku ya pili ya sikukuu ya Nairuzi maafisa wa utawala wa Shah walishambulia mkusanyiko wa matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini) katika mji wa Qum waliokuwa wakifanya maombolezo na kuwauwa shahidi na kuwajeruhi baadhi yao.