Mar 30, 2019 02:17 UTC
  • Jumamosi, Machi 30, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 23 Rajab 1440 Hijria mwafaka na tarehe 30 Machi 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 273 iliyopita, alizaliwa Francisco José de Goya mchoraji mashuhuri wa nchini Uhispania. mwanasanaa huyo alizaliwa katika mji wa Fuendetodos huko Uhispania. Francisco José de Goya alikuwa mabaki ya mwisho ya waalimu wakongwe barani Ulaya. ***

Francisco José de Goya

Katika siku kama ya leo miaka 166 iliyopita, alizaliwa Vincent van Gogh mchoraji mahiri wa Kiholanzi. Vincent van Gogh alizaliwa katika mji wa The Hague na akiwa katika rika la ujana alijishughulisha na kazi mbalimbali. Alipofikisha umri wa miaka 30 aliondokea kuwa na mapenzi makubwa na sanaa ya uchoraji. Kwa vmsingi huo akaanza kujifunza sanaa hiyo.  ***

Vincent van Gogh

Miaka 152 iliyopita katika siku kama ya leo,  Russia iliiuzia Marekani ardhi yenye utajiri ya Alaska inayopatikana huko kaskazini magharibi mwa Canada na katika pwani ya bahari za Pacific na Arctic kwa thamani ya dola milioni saba na laki mbili kutokana na mahitaji ya kifedha iliyokuwanayo. Alaska ina ukubwa wa kilomita mraba zaidi ya milioni moja huku likiwa jimbo la 49 la Marekani. Jimbo la Alaska pia lina thamani kubwa za kiuchumi kutokana na kuwa na maliasili nyingi za madini, hususan mafuta na dhahabu pamoja na mapato yanayotokana na uvuvi wa samaki. ***

Alaska

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, alifariki dunia mwanachuoni mkubwa wa Iran, Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Borujerdi, mmoja wa wasomi mashuhuri wa Iran. Baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alielekea mjini Najaf Iraq na kupata kusoma kwa walimu wakubwa wa kidini wa mji huo, kisha akarejea nchini Iran. Ayatullah Burujerdi kwa kushirikiana na wanachuoni wengine wakubwa wa Kiislamu alianzisha Umoja wa Ukurubisho wa Madhehebu ya Kiislamu. Ayatullah Borujerdi licha ya kuandika vitabu kadhaa, alijenga misikiti kadhaa ndani na nje ya Iran, ukiwemo Msikiti wa Hamburg nchini Ujerumani. ***

Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Borujerdi

Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, maandamano makubwa kwa jina la "Yaumul Ardh" au Siku ya Ardhi yalifanyika huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Ni vyema kukumbusha hapa kwamba, tarehe 18 Oktoba mwaka 1975 Miladia, mkutano wa kutetea ardhi ulifanyika katika eneo la Jalil kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika azimio la kwanza la mkutano huo, washiriki walielezea kusikitishwa kwao na hatua ya utawala wa Kizayuni ya kupora ardhi za raia wa Kiarabu wa Palestina na kulaani vikali hatua hiyo. Mkutano wa Jalil ulisisitiza kuwa, siasa za utawala wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu zinakiuka haki za wananchi Waislamu wa Palestina katika ardhi zao na kwamba, utawala wa Kizayuni umepuuza wazi hati ya haki za binadamu na misingi ya demokrasia na usawa. ***

Na miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kuanguka utawala wa kifalme wa Shah, lilianza kufanyika zoezi la kura ya maoni ya nchi nzima kwa ajili ya kuainisha mfumo wa utawala nchini Iran. Kura hiyo ya maoni ya kihistoria iliyopokewa kwa wingi na wananchi wa Iran, ilifanyika kwa siku mbili. Kura hiyo ilimalizika kwa kupigiwa wingi wa kura ya ndiyo wa asilimia 98.2 kwa utawala wa Mfumo wa Kiislamu. ***