May 22, 2019 03:23 UTC
  • Jumatano, 22 Mei, 2019

Leo ni Jumatano tarehe 16 Ramadhani mwaka 1440 Hijria sawa na tarehe 22 Mei mwaka 2019 Miladia.

Miaka 713 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 16 Ramadhani mwaka 727 Hijria Qamaria, aliaga dunia Ibn Zamlakani, faqihi na msomi wa Hadithi na Fasihi wa Kiislamu, aliyefahamika kama Dimishqi. Msomi huyo alipata kustafidi na hazina ya elimu ya dini na hadithi kutoka kwa maulamaa wa zama hizo. Kutokana na kipaji chake cha elimu, msomi huyo aliruhusiwa kutoa fatua kwa kipindi cha miaka 20, mbali na kufunza masomo mbalimbali ya kidini katika vyuo tofauti, na kuwa kadhi mjini Damascus nchini Syria. Miongoni mwa kazi za msomi huyo ambazo tunaweza kuashiria hapa ni kitabu alichokipa jina "Al Buranul Kaashif An I'ijazil Qurani".

Eb-ne Zamlakani
 

Siku kama ya leo kwa mujibu wa baadhi ya riwaya yaani tarehe 16 Ramadhani mwaka 845 Hijria Qamariya, alifariki dunia Taqiyud-Din Abul-Abbas Maqrizi, msomi na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu. Maqrizi alizaliwa mjini Cairo, Misri na baadaye aliekekea katika miji mikubwa ya Ulimwengu wa Kiislamu kwa  elimu na maarifa ya Kiislamu.  Kwa muda msomi huyo alijishughulisha na mauala ya ukadhi huko Cairo. Alipendelea sana historia na kuandika vitabu tofauti katika uwanja huo. Miongoni mwa athari za Taqiyud-Din Abul-Abbas Maqrizi ni pamoja na kitabu cha 'as-Suluuk Lima'arifatil-Muluuk' ambacho kinazungumzia historia.

Taqiyud-Din Abul-Abbas Maqrizi 

 

Siku kama hii ya leo miaka 134 iliyopita sawa na tarehe 22 mwezi Mei mwaka 1885  aliaga dunia mwandishi na malenga mtajika wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 83 kwa jina la Victor Hugo. Hugo alikuwa mfuasi wa mageuzi kwa maslahi ya wale waliokandamizwa na kudhulumiwa. Alizaliwa mwaka 1802 miladia na  alianza kughani mashairi tangu akiwa kijana. Akiwa na umri usiopindukia miaka 25 Hugo alikuwa mwanachama katika akademia ya Ufaransa na wakati huo huo akawa mbunge katika bunge la Ufaransa. Victor Hugo aliamua kuachana na masuala ya siasa wakati wa utawala wa Napoleon wa Tatu kutokana na kupinga kwake siasa za kibeberu za mtawala huyo na kuelekea uhamishoni kwa miaka 20. 

Victor Hugo, malenga mtajika wa zama hizo za Ufaransa 
 

Miaka 39 iliyopita katika siku kama hii ya leo sawa na tarehe Mosi mwezi Khordad mwaka 1359 Hijria Shamsiya ulianza mzingiro wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Marekani ambayo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ilipoteza maslahi yake haramu nchini Iran ilianza kuiwekea Iran mzingiro wa kiuchumi lengo likiwa ni kuwashinikiza wananchi Waislamu na wanamapambano wa Iran na vile vile kuulazimisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kufikia mapatano. Baada ya uamuzi huo wa serikali ya Marekani; Imamu Khomeini (M.A) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alitangaza kuwa uhai wa uchumi wa nchi mbalimbali hautegemei madola makubwa na kulihutubu taifa la Iran kuwa: Kamwe msiogope vikwazo vya kiuchumi; kama mtatuwekea mzingiro wa kiuchumi basi tutaimarika zaidi na ni kwa maslahi yetu."

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama imara na kimuqawama mbele ya vikwazo
 

Siku kama hii ya leo miaka 33 iliyopita Omar Tilmisani mmoja wa viongozi wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1904 katika eneo la Tilmisan nchini Algeria. Mwaka 1924 Tilmisani alihitimu masomo yake ya shahada katika fani ya sheria na mwaka 1928 akawa mwanachama wa Ikhwanul Muslimin  baada ya kuasisiwa harakati hiyo. Tilmisani ambaye alimpita kwa miaka miwili Hassan al Banna kiongozi wa harakati hiyo anahesabiwa kuwa mmoja wa makada wakongwe wa harakati hiyo. Hatimaye Omar Tilmisani aliaga dunia tarehe 22 Mei 1986 akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kupatwa na maradhi ya ini na figo. 

Omar Tilmisani, aliyekuwa mmoja wa makada wakongwe wa Ikhwanul Muslimin ya Misri