May 23, 2019 23:16 UTC
  • Ijumaa 24 Mei 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 18 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka 1440 Hijria sawa na tarehe 24 Mei mwaka 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 476 iliyopita, aliaga dunia mnajimu na mwanahesabati mashuhuri wa Poland, Nicolaus Copernicus akiwa na umri wa miaka 70. Alizaliwa mwaka 1473 ambapo awali alijifunza elimu ya nujumu na baadaye tiba, na baada ya kukamilisha masomo alianza kufundisha hesabati huko Roma. Hata hivyo Copernicus aliendelea kudurusu na kufanya utafiti wa elimu ya nujumu na mwaka 1503 alivumbua nadharia ya harakati ya dunia kuzunguka jua na vilevile dunia kujizunguka yenyewe katika kila baada ya masaa 24. Nicolaus Copernicus alifariki dunia tarehe 24 Mei 1543 siku chache tu baada ya kuchapisha kitabu cha On the Revolutions of the Celestial Spheres kinachofafanua nadharia zake. Inafaa kuashirikia hapa kuwa, karne kadhaa kabla ya Corpenicus, mnajimu na msomi maarufu Muirani, Abu Raihan Biruni alikuwa tayari ameshavumbua ukweli kuwa sayari ya dunia huzunguka jua. Katika moja ya vitabu vyake, Corpenicus ameashiria ukweli huo.

Nicolaus Copernicus

@@@@

Siku kama ya leo miaka 197 iliyopita yaani 24 Mei mwaka 1822, nchi ya Ecuador ilipata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania. Ecuador ni moja ya nchi za Amerika ya Kusini ambayo kupitia uongozi wa Simón Bolívar mwanamapinduzi maarufu wa Venezuela, ilifanikiwa kuwa huru na kujiunga na umoja wa Colombia Kubwa. Hata hivyo umoja huo ulisambaratika haraka na kufanya nchi wanachama wa umoja huo ikiwemo Ecuador kuasisi mfumo wa jamhuri.

Bendera ya Ecuador

 

Miaka 37 iliyopita na katika siku kama ya leo, mji wa Khorramshahr wa Iran ulikombolewa na wapiganaji wa Kiislamu na ukaondoka katika uvamizi wa majeshi vamizi ya Iraq. Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo  ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane. Uvamizi dhidi ya mji huo ulijiri mwanzoni mwa vita vya miaka minane vya kulazimishwa vya utawala wa Saddam wa Iraq dhidi ya Iran. Ama wapiganaji shupavu wa Iran waliokuwa wamejihami kwa silaha ya imani ya kumtegemea Mwenyezi Mungu walipambana kishujaa na kufanikiwa kuwapa pigo kubwa wanajeshi vamizi wa Iraq na hatimaye kuukomboa mji wa Khorramshahr na hivyo kuibua hamasa ya aina yake  jambo ambalo liliwashangaza weledi wa mambo ya kijeshi duniani. Siku hii ya kukumbuka kukombolewa mji wa Khorramshahr inajulikana katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuwa, "Siku ya Muqawama na Ushindi". 

Sherehe baada ya kukombolewa mji wa Khorramshahr

Miaka 19 iliyopita katika siku kama ya leo yaani 24 Mei mwaka 2000, vikosi vya utawala dhalimu wa Israel vililazimika kuondoka kwa madhila katika eneo la kusini mwa Lebanon baada ya kulikalia kwa mabavu eneo hilo kwa muda wa miaka 22. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na mapambano ya wananchi wa kusini mwa Lebanon. Mwaka 1982, majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yalishambulia Lebanon na kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut. Hata hivyo kutokana na wananchi hao kuathirika na mafundisho ya kutokubali dhulma hasa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, nchini Lebanon kulianzishwa harakati za mapambano ya Kiislamu dhidi ya majeshi vamizi ya utawala haramu wa Israel. Harakati ya Mapamabno ya Kiislamu ya Hizbullah ilikuwa na nafasi muhimu na ya kuzingatiwa katika kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon kutoka katika makucha ya utawala dhalimu wa Israel.

Bendera ya Hizbullah

Katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, nchi ya Eritrea iliyoko kaskazini mashariki mwa bara la Afrika ilipata uhuru kutoka kwa Ethiopia. Mwaka 1936 Italia iliikalia kwa mabavu Eritrea iliyokuwa ikihesabiwa katika zama hizo kuwa sehemu ya ardhi ya Ethiopia. Mwaka 1953, Italia iliirejeshea Ethiopia ardhi hiyo. Hata hivyo wananchi wengi wa nchi hiyo waliokuwa wakitaka uhuru walianzisha harakati za ukombozi dhidi ya serikali ya Ethiopia. Mwaka 1991, Harakati ya Ukombozi wa Eritrea ikisaidiana na wanamapinduzi wa Ethiopia walihitimisha utawala wa kidikteta wa Mengistu Haile Mariam, na wakakubaliana kuanishwa mustakbali wa Eritrea mwaka 1993 kupitia kura ya maoni. Washiriki wengi wa kura hiyo ya maoni walipiga kura ya kutaka kujitawala Eritrea. 

Bendera ya Eritrea