May 30, 2019 00:05 UTC
  • Alkhamisi, Mei 30, 2019

Leo ni Akhamisi tarehe 24 Ramadhani 1440 Hijria sawa na tarehe 30 Mei 2019 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 730 iliyopita alifariki dunia Qutbuddin Shirazi, tabibu, mwanahesabati, mwanafikizia na mwanafalsafa wa Kiirani katika mji wa Tabrizi huko kaskazini magharibi mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi. Alibobea pia katika elimu za mantiki na irfani. Alifanya hima kubwa kutafuta elimu ya tiba na alihudumu kwa miaka mingi kama tabibu katika hospitali ya Shiraz, kusini mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa mtu wa kwanza kufanya uchunguzi kuhusu upinde wa mvua na kupata tafsiri ya kisayansi kuhusu suala hilo. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika taaluma mbalimbali.

Qutbuddin Shirazi

 

Siku kama ya leo miaka 72  iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai, mmoja wa maulamaa na wataalamu wa elimu ya irfani. Sayyid Muhammad Tabatabai alizaliwa mjini Tabrizi kaskazini mwa Iran, mwaka 1325 Hijiria. Akiwa na miaka 19 alielekea mjini Najaf, Iraq akiwa na kaka yake mkubwa Allamah Muhammad Hassein Tabatabai na kupata kusoma elimu ya dini mjini hapo. Baada ya kutabahari katika elimu ya Kiislamu alirejea eneo alikozaliwa la Tabriz na kujishughulisha na kuwalea wanafunzi.

Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai Tabrizi

 

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita muwafaka na tarehe 30 Mei 1918, yalimalizika mapigano makubwa ya Marne yaliyotokea wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia kati ya jeshi la Ujerumani na vikosi waitifaki vilivyozijumuisha Marekani, Uingereza na Ufaransa. Vita hivyo vya siku tano vilijiri katika eneo karibu na Mto Maren ulioko kaskazini mashariki mwa Ufaransa ambapo majeshi ya Ujerumani yalijipatia ushindi na kuwashikilia mateka wanajeshi elfu hamsini na tano wa majeshi ya waitifaki.

Vita vya Marne

 

Siku kama ya leo 93 miaka iliyopita, alifariki dunia Ali Akbar Khan Nafisi aliyejulikana kama Naadhimul Atwiba, daktari na mtaalamu wa lugha wa Kiirani, katika mji wa Tehran. Baada ya kumaliza masomo yake ya mwanzo alianza kujifunza masomo ya kidini na pia udaktari katika chuo cha Darul Funun cha Tehran. Baadhi ya vitabu vilivyoandikwa na Naadhimul Atwiba katika uwanja wa tiba vimetarjumiwa katika lugha za kigeni. Ali Akbar Khan Nafisi ambaye pia alikuwa mtaalamu wa lugha alifanya jitihada nyingi katika kukusanya maneno ya lugha ya Kifarsi na kuandika kamusi inayoitwa 'Kamusi ya Nafisi.'

Naadhimul Atwiba

 

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita inayosadifiana na tarehe 30 Mei 1981, aliuawa Zia ur Rahman Rais wa Bangladesh baada ya kupigwa risasi katika mji wa Chittagong ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo. Rais Zia ur Rahman aliuawa baada ya kuchungulia dirishani kwenye nyumba ya wageni ya serikali katika mji huo. Watu wanane waliuawa kwenye shambulio hilo, wakiwemo wasaidizi na walinzi wa rais huyo.

Zia ur Rahman

 

Na siku kama ya leo miaka 27 iliyopita Dakta Jalal Samimi mtafiti na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ufundi cha San'at Sharif cha mjini Tehran alifanikiwa kugundua vyanzo vitano vya mionzi ya Gamma katika mzunguko wa kundi la sayari na nyota au Milky Way Gallaxy, baada ya kufanya utafiti na majaribio kwa miaka 20 katika uwanja huo. Inafaa kukumbusha hapa kuwa Dakta Samimi alizaliwa mwaka 1319 Hijiria Shamsia katika mji wa Zabol kusini mashariki mwa Iran na kuhitimu daraja ya udaktari katika somo la Fizikia. Dakta Jalal Samimi alifanikiwa katika ugunduzi huo muhimu baada ya kutwalii na kufanya uchunguzi wa kina na majaribio mengi kuhusiana na Nuclear Emulsion.

Nuclear Emulsion

 

Na siku kama ya leo miaka 241 iliyopita sawa na tarehe 30 Mei 1778, Francois- Marie Arouet maarufu kwa jina la Voltaire, mwanafalsafa na mwandishi wa Kifaransa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 84. Katika maisha yake, Voltaire aliwahi kuwekwa mahabusu mara mbili na kubaidishwa kwa muda wa miaka mitatu nchini Uingereza. Kitendo hicho kilimkasirisha sana Voltaire na kumfanya kuwa dhidi ya utawala wa Ufaransa.

Francois- Marie Arouet