Jumatatu, tarehe 3 Juni, 2019
Leo ni Jumatatu tarehe 28 Ramadhani 1440 Hijria sawa na tarehe 3 Juni 2019.
Siku kama ya leo miaka 1168 iliyopita aliaga dunia Abu Ma'ashar Balkhi mmoja wa wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya hadithi wa Kiirani. Alielekea Baghdad mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Katika zama zake Abu Ma'ashar Balkhi alikuwa mnajimu mashuhuri wa Kiislamu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni al-Madkhal al-Kabir na al-Mawalid as-Saghirah.

Siku kama ya leo miaka 517 iliyopita Vasco da Gama mwanabaharia wa Ureno alifanya mauaji ya umati na ya kinyama huko Calicut nchini India. Calicut ambayo hii leo inajulikana kwa jina la Kozhikode ni bandari iliyoko Madras huko kusini mwa India. Hii ndiyo iliyokuwa sehemu ya kwanza kwa Vasco da Gama kutua na kuiteka katika safari yake ya kuelekea India mwaka 1498. Kama walivyokuwa wakoloni wenzake, da Gama alijitambua kuwa ndiye mmiliki halisi wa India. Wakati wafanyabiashara 800 wa Kiarabu walipofika katika eneo hilo kwa lengo la kufanya biashara ya mchele, Vasco da Gama alitoa amri wafanyabiashara hao wakatwe mikono, masikio na pua na kisha wauawe kwa umati baada ya kuteketeza meli zao.
Miaka 352 iliyopita katika siku kama hii ya leo, kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya elimu ya tiba na upasuaji, ilifanyika kazi ya kuhamishia damu kwenye mwili wa mwanadamu. Kazi hiyo ilifanywa na tabibu wa Kifaransa aliyejulikana kwa jina la Jean Baptiste Denis. Kuigizwa damu kwenye miiili yawagonjwa kulizusha mageuzi makubwa katika elimu ya tiba kwani hadi kipindi hicho wagonjwa wengi walikuwa wakifariki dunia kutokana na kuvuja damu kwa wingi au kwa upungufu wa damu. Katika utafiti wake wa kwanza tabibu huyo Mfaransa alitia damu ya mbuzi ndani ya mwili wa mwanadamu lakini baadaye alifanikiwa kuweka damu ya mwanadamu katika mwili wa mwanadamu mwingine.
Miaka 56 iliyopita katika siku kama hii ya leo mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alitoa hotuba kali na ya kihistoria kwa mnasaba wa siku ya Ashuraa dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah. Hotuba hiyo ilitolewa mbele ya mkusanyiko mkubwa wa watu na wanazuoni katika shule ya Faiziyya katika mji wa Qum licha ya marufuku na vitisho vya utawala wa Shah. Katika hotuba hiyo Imam Khomeini alikemea vikali uhalifu uliokuwa ukifanywa na Shah na usaliti wake dhidi ya Waislamu wa Iran.
Na miaka mitatu iliyopita katika siku kama hii ya leo gwiji wa uzani wa juu wa ndondi duniani, Muhammad Ali Clay aliaga dunia. Muhammad Ali ambaye jila lake la awali lilikuwa Cassius Marcellus Clay anatambuliwa kuwa miongoni mwa wanamasumbwi mashuhuri na wakubwa zaidi duuniani. Baada ya kukubali dini tukufu ya Uislamu, Muhammad Ali Clay alijihusisha pia na harakati za kisiasa nchini Marekani na aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 5 jela kutokana na misimamo yake ya kisiasa. Muhammad Ali aliaga dunia tarehe 3 Juni mwaka 2016 baada ya kusumbuliwa na maradhi ya Parkinson's kwa miaka mingi.
