Jun 04, 2019 23:35 UTC
  • Jumatano, tarehe 5 Juni, 2019

Leo ni Jumatano tarehe Mosi Shawwal 1440 Hijria sawa na Juni 5 mwaka 2019.

Leo tarehe Mosi Shawwal inasadifiana na sikukuu ya Idul-Fitr. Idul Fitri ni miongoni mwa sikukuu kubwa katika dini tukufu ya Kiislamu. Baada ya kukamilisha ibada ya funga, kuomba na kujipinda kwa ibada katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, Waislamu hufanya sherehe katika siku hii kubwa wakimshukuru Mola Manani kwa kuwawezesha kukamilisha ibada huyo. Iddi al Fitr ni kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa ibada na kujisafisha. Katika siku kama hii ya leo ni haramu kufunga saumu yoyote na Waislamu baada ya juhudi za mwezi mzima za kupambana na nafsi na kuchuma matunda ya ucha-Mungu hukusanyika pamoja na kusali Swala ya Iddul Fitr. Kuhusiana na utukufu wa siku hii Mtukufu Mtume (saw) anasema: "Mtu yeyote atakayemuasi Mwenyezi Mungu katika siku ya Idi, basi ni kama mtu aliyemuasi Mwenyezi Mungu siku ya Miadi- yaani Siku ya Kiama." Kwa mnasaba wa siku hii adhimu, Redio Tehran inatoa mkono wa pongezi, heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani.

Siku kama ya leo miaka 1187 iliyopita yaani tarehe Mosi Shawwal mwaka 253 Hijria Qamariya mpokezi mashuhuri wa hadithi wa Ahlusunna, Imam Muhammad Ismail Bukhari aliaga dunia. Abu Abdullah Muhammad Ismail aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Imam Bukhari ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa hadithi wanaoaminiwa na Ahlusunna. Alisafiri sana kwa ajili ya kutafuta hadithi za Mtume (saw). Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni kile cha Jamius Swahih maarufu kama Sahihi Bukhari. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni: Al Adabul Mufrad, Tarikhul Ausat na As Sunan.

Imam Muhammad Ismail Bukhari

Tarehe Mosi Shawwal miaka 871 iliyopita Said Bin Mubarak maarufu kwa jina la Ibn Dahhan, mfasiri, mwanafasihi na malenga wa Kiislamu alifariki dunia. Alizaliwa mjini Baghdad na baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alianza kusoma lugha sambamba na kupokea hadithi kutoka kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake. Mtaalamu huyo mkubwa wa lugha alitilia maanani taaluma ya fasihi hususan katika kusoma mashairi na hivyo kuwa mfano wa kuigwa na wanafunzi wake katika usomaji mashairi.

Miaka 834 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Abu Abdallah Muhammad bin Omar Razi mashuhuri kwa jina la Fakhrurazi msomi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu. Alizaliwa katika mji wa Rey jirani na Tehran na alifanikiwa kwa haraka kujifunza elimu mbalimbali za Kiislamu kama Fiqihi, Tafsiri, Falsafa na Mantiki kutokana na kipaji kikubwa alichokuwa nacho. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vya Fakhrurazi ni al Tafsirul Kabiir, Sherh Nahaj al-Balagha, Nihayat al-Uquul wa Siraj al-Quluub.

Fakhru Razi

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Khordad 1342 Hijria Shamsia sawa na tarehe 5 Juni 1963 Miladia, wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa dhidi ya utawala wa Shah, baada ya kusikia habari ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini MA. Imam alitiwa mbaroni na vibaraka wa utawala wa Shah siku kadhaa nyuma kufuatia hotuba yake ya kihistoria aliyoitoa katika mji wa Qum, ambayo ilifichua njama mbalimbali za utawala wa Shah dhidi ya taifa la Iran. Ni wazi kuwa mapambano ya umwagaji damu na ya kihistoria ya tarehe 15 Khordad, yalikuwa nukta ya kuanza mapinduzi ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah na kufungua njia ya mustakbali wa kisiasa na kijamii nchini.

15 Khordad 1342

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita mwafaka na tarehe 5 Juni 1967, vilianza vita vikubwa vya tatu kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na nchi za Kiarabu. Katika siku kama ya leo kikosi cha anga cha utawala ghasibu wa Israel kilifanya shambulizi la kushtukiza na kuvuka mipaka ya nchi tatu za Misri, Syria na Jordan na kufanya uharibifu mkubwa. Baada ya shambulizi hilo, vikosi vya nchi kavu vya Israel vikiwa na silaha za kisasa na uungaji mkono wa Marekani na Uingereza, vilifanikiwa kuyashinda majeshi ya Misri, Syria na Jordan katika kipindi cha siku sita tu.

Vita vya Waarabu na Israel

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, sawa na tarehe 5 Juni 1972, lilifanyika kongamano la kwanza la mazingira huko Stockholm nchini Sweden. Kongamano hilo liliwashirikisha wawakilishi 1300 kutoka nchi 113 duniani likiwa na kauli mbiu isemayo 'Kuna Ardhi Moja tu'. Miongoni mwa malengo makuu ya kongamano hilo yalikuwa ni kuwekwa mikakati ya kujenga makaazi ya raia kwa kuzingatia ulindaji mazingira, kuainisha na kudhibiti mada haribifu kwa mazingira na kuhifadhi mazingira kwa ajili ya vizazi vya baadaye.