Jun 07, 2019 21:43 UTC
  • Jumamosi, Juni 8, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe Nne Mfunguo Mosi Shawwal 1440 Hijria sawa na tarehe 8 Juni 2019 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel, Mossad, lilifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya kiongozi mwingine wa Kipalestina katika moja ya nchi za kigeni. Siku hiyo maajenti wa Mossad walimuuwa Atef Bseiso mmoja wa viongozi wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Paris, Ufaransa.  Licha ya kwamba hakukuwepo shaka juu ya kuhusika utawala wa Kizayuni katika mauaji hayo, lakini utawala huo ghasibu ulikana kufanya jinai hiyo ya kinyama kwa kuhofia hasira za walimwengu. Hata hivyo miaka saba baadaye, polisi ya Ufaransa ilitangaza kwamba shirika hilo la ujasusi la Israel Mossad ndilo lililopanga na kutekeleza mauaji hayo.

Atef Bseiso

Siku kama ya leo miaka 164 iliyopita, mji wa Lisbon ambao ni mji mkuu wa Ureno uliharibika, kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi na moto uliosababishwa na zilzala hiyo. Karibu wakazi elfu arubaini wa mji huo walipoteza maisha yao na theluthi mbili ya nyumba na taasisi za kiuchumi za mji huo zilibomolewa. Mbali na maafa hayo, karibu meli elfu mbili, boti na ngalawa nyingi zilizokuwa katika bandari za Ureno zilizama. Mtetemeko huo ni moja ya mitetemeko mikubwa zaidi kuwahi kuikumba Ureno.

Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita, alizaliwa Said Nafisi, mwandishi na mtarjumi wa kisasa wa nchini Iran hapa mjini Tehran. Nafisi alikuwa mtoto wa Ali Akbar Nafisi, maarufu kwa jina la Nadhim al-Atwibbai, msomi na mwandishi wa kitabu cha ‘Kamusi ya Nafisi’. Baada ya kumaliza masomo yake ya awali, Ustadh Said Nafisi alikamilisha masomo yake katika taaluma za sheria na elimu ya siasa. Nafisi alijishughulisha na ukufunzi katika taaluma za historia na fasihi huku akiwa mmoja wa wanaharakati wa utamaduni nchini Iran. Mbali na Iran, Ustadh Said Nafisi alikuwa na uanachama katika taasisi mbalimbali za kiutamaduni na katika vyuo vikuu vya nchi kadhaa za Ulaya na Asia.

Said Nafisi

Na miaka 1089 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Muhammad bin Hassan Dar Qutni mmoja wa maulama wa Kiislamu na wataalamu wa lugha wa karne ya 4 Hijria. Dar Qutni alikuwa miongoni mwa wa maqari na wafasiri watajika wa Qu'rani Tukufu katika zama zake hizo. Alitumia sehemu kubwa ya umri wake kuandika vitabu katika taaluma mbalimbali. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni al Muujamul Kabiir, al Maudhi'i fii Maanil Qur'an na al Manasik.

Muhammad bin Hassan Dar Qutni