Jumanne, tarehe 11 Juni, 2019
Leo ni Jumanne tarehe 7 Shawwal 1440 Hijria sawa na 11 Juni 2019.
Siku kama hii ya leo miaka 1437 iliyopita kulipiganwa vita vya Uhud kando kando ya mlima wenye jina hilo kaskazini mwa mji wa Madina, kati ya Waislamu na Washirikina. Baada ya washirikina wa Kiquraishi kushindwa vibaya na Waislamu katika vita vya Badr walianzisha vita hivi vya Uhud kwa kuandaa jeshi la watu 3,000 waliokuwa na zana kamili kwa ajili ya vita hivyo, huku wapiganaji wa Kiislamu wakuwa 700 tu. Kabla ya kuanza kwa vita hivyo, Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w) aliwashauri masahaba zake juu ya namna atakavyopambana na Maquraishi na iliamuliwa kuwa vita hivyo vipiganwe nje ya mji wa Madina. mwanzoni mwa vita hivyo, Waislamu walionekana kushinda, hata hivyo kufuatia kughafilika na baadhi yao kuasi amri ya Mtume (saw) aliyewataka kuendelea kubakia mlimani, Waislanu hao walishuka mlimani kwa tamaa za kupata ngawira hali iliyowafanya washirikina kuwashambulia Waislamu na kudhoofika nguvu na uwezo wao. Waislamu 70 waliuawa shahidi katika vita hivyo akiwemo Hamza ami yake Mtume (s.a.w). Hata hivyo washirikina hawakuweza kupata ushindi wa moja kwa moja na hivyo wakalazimika kurejea Makka.
Miaka 447 iliyopita na katika siku kama ya leo alizaliwa Ben Jonson, mwandishi wa michezo ya kuigiza na muigizaji mashuhuri wa Uingereza katika familia masikini. Alilazimika kufanya kazi za mikono katika sekta ya ujenzi akiwa na baba yake wa kambo ili kujidhaminia karo ya shule. Baada ya kuhitimu masomo ya juu alijiunga na jeshi la nchi hiyo akiwa na miaka 29 lakini bado jambo hilo halikumpa utulivu wa moyo, na hivyo akalazimika kuondoka jeshini. Aliingia kwenye uwanja wa michezo ya kuigiza kama muigizaji na kisha kuanza kuandika michezo hiyo mwenyewe. Aliishi katika zama za Shakespeare, mwandishi mashuhuri wa michazo ya kuigiza wa Uingereza na kushirikiana naye kwa karibu. Katika michezo yake, Ben Jonson alikuwa akiwakejeli mabwenyenye na viongozi wa makanisa jambo lililowakasirisha sana. Kwa vyovyote vile umasikini na matatizo mengine yalimwandama Jonson hadi mwishoni mwa maisha yake hapo mwaka 1637.
Siku kama ya leo miaka 164 iliyopita mwafaka na tarehe 11 Juni mwaka 1855, mwanga wa jua ulitambuliwa kwa kutumiwa njia za taaluma ya uchanganuzi na wigo wa rangi. Jaribio hilo lilifanywa kwa mara ya kwanza katika historia ya utafiti mpya wa fizikia na wanasayansi wawili wa Ujerumani, Kirchhoff na Bunsen. Inafaa kuashiria hapa kwamba, mionzi ya jua katika hewa wakati wa mvua pamoja na kutokea upinde wa mvua wenye rangi mbalimbali, ni tukio la kuvutia ambalo husababishwa na kuchanganuliwa nuru ya jua na matone ya maji mawinguni. Hata hivyo suala hilo mwanzoni lilifafanuliwa na wanasayansi wa Kiislamu kama vile Ibn Sina, Ibn Hisham na Qutbudin Shirazi na baadaye kuthibitishwa na Kirchhoff na Bunsen.

Siku kama hii ya leo miaka 47 iliyopita inayosadifiana na tarehe 7 Shawwal 1393 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul Hussein Sha'rani mfasiri wa Qurani Tukufu inayojulikana kwa jina la 'Manhaj Swadiqiin', akiwa na umri wa miaka 73. Msomi huyo licha ya kubobea katika elimu za kidini alikuwa mahiri katika kuzungumza lugha za kigeni kama vile Kifaransa, Kiingereza na Kiarabu. Licha ya kuonyesha uwezo wake katika tafsiri ya Qurani Tukufu ya Manhaj Swadiqiin yenye juzuu 10 vilevile ameandika kitabu cha Sharh Kifayatil - Usuul.