Jun 11, 2019 22:33 UTC
  • Jumatano tarehe 12 Juni mwaka 2019

Leo ni Jumatano tarehe 8 Shawwal 1440 Hijria inayosadifiana na Juni 12 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita inayosadifiana na 12 Juni 1991, ulifanyika uchaguzi wa kwanza wa Rais wa Shirikisho la Russia. Baada ya kusambaratika Urusi ya zamani, Russia kama zilivyokuwa nchi nyingine zilizokuwa zikiunda Umoja wa Kisovieti zilijipatia uhuru wake. Boris Yeltsin aliiongoza nchi hiyo kwa vipindi viwili, hadi mwezi Disemba 1999, alipoamua kung'atuka madarakani.

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 12 Juni 1964, Nelson Mandela kiongozi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini alihukumiwa kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya uhaini dhidi ya mfumo na utawala wa ubaguzi wa rangi, Apartheid nchini humo. Mandela alihukumiwa adhabu hiyo pamoja na wenzake saba akiwemo Walter Sisulu aliyekuwa Katibu Mkuu wa zamani wa chama cha African National Congress kilichokuwa kimepigwa marufuku nchini humo. 

Tarehe 12 Juni 1914, kwa mara ya kwanza kabisa yalifanyika majaribio ya kutumia nishati ya joto la jua pambizoni mwa Cairo mji mkuu wa Misri. Mbunifu na mtekelezaji wa mpango huo alikuwa mwanafizikia wa Kijerumani, ambaye aliweza kukusanya miale ya jua na kufanikiwa kuwasha mashine ya mvuke yenye kutumia 'horse power' 50.

Miaka 116 iliyopita katika siku kama ya leo ambayo ni sawa na tarehe 8 Shawwal mwaka 1324 Hijria toleo la kwanza la gazeti la 'Majlis' lichapishwa nchini Iran. Gazeti hilo lilianzishwa na mtu aliyejulikana kwa jina la Mirza Sayyid Muhammad Sadiq Tabatabai. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mazungumzo yote ya Majlisi ya Ushauri ya Iran yaani Bunge.

Gazeti la Majlis

Tarehe 12 Juni miaka 479 iliyopita nchi ya Chile iliyoko magharibi mwa Amerika ya Kusini ilitekwa na wakoloni wa Hispania. Kabla ya hapo Wahindi Wekundu wa Chile walikuwa wamevunja hujuma na mashambulio kadhaa ya Wahispania waliokusudia kuteka na kukalia kwa mabavu ardhi yao. Hata hivyo, hata baada ya kutekwa nchi yao, Wahindi Wekundu hao waliendeleza mapambano dhidi ya wakoloni hadi pale José Francisco de San Martín jenerali wa Argentina alipowasili mwaka 1817 na kuanzisha mashambulio ya kuzikomboa nchi zote zilizokuwa chini ya ukoloni wa Hispania Kusini mwa Amerika, ikiwemo Chile. Kwa msingi huo, Chile akakombolewa na kutangaza uhuru wake mwaka 1818.