Alkhamisi tarehe 13 Juni mwaka 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 9 Shawwal 1440 Hijria sawa na 13 Juni mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Khordad 1362 Hijria Shamsia, Bi. Nusrat Amin, faqihi na mfasiri mkubwa wa Qurani Tukufu alifariki dunia katika mji wa Esfahan ulioko katikati mwa Iran. Bi. Nusrat Amin aliutumia muda wake wote katika kuishughulikia Qurani Tukufu na kufanikiwa kufasiri kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu katika juzuu 15 na kuandika vitabu vingine vingi. Miongoni ma vitabu vya msomi huyu ni Assair Wassuluuk na Nafahaat Rahmaniyya.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, inayosadifiana na 23 Khordad 1359 Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwa na lengo la kuleta mabadiliko katika vyuo vikuu hapa nchini, alitoa amri ya kuasisiwa Baraza la Mapinduzi la Kiutamaduni. Katika ujumbe wake, Imam Khomeini MA aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuratibu na kuandaa mipango na mitalaa katika kozi mbalimbali za vyuo vikuu inayokwenda sambamba na mafunzo ya utamaduni tajiri wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita sawa na tarehe 13 Juni mwaka 1944, kombora la kwanza la ardhi kwa ardhi la Ujerumani ya Kinazi lililojulikana kwa jina la V-1 lilishambulia ardhi ya Uingereza, katika Vita vya Pili vya Dunia. Kabla ya hapo Ujerumani ilikuwa ikiishambulia ardhi ya Uingereza kwa njia ya anga. Baada ya vita hivyo, nchi nyingine duniani zilitengeneza makombora ya aina hiyo kwa teknolojia ya kisasa zaidi.
Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, mwafaka na tarehe 13 Juni 1921 katika miaka ya mwanzo ya usimamizi wa Uingereza huko Palestina, ilianza harakati kubwa ya kwanza ya wananchi katika ardhi yote ya Palestina dhidi ya Wazayuni. Harakati ya wananchi hao wa Palestina ilibainisha upinzani wao dhidi ya siasa za kikoloni za Uingereza pamoja na uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Wazayuni waliokuwa wakiishi Palestina. Katika fremu ya sera hizo za Uingereza mwaka 1923 kulikuwa na Wazayuni 35 elfu huko Palestina na kabla ya kuundwa utawala bandia wa Israel mwaka 1948 idadi hiyo ilikuwa zaidi ya laki sita.

Tarehe 9 Shawwal miaka 1330 iliyopita, alifariki dunia Ibn Sirin, mtaalamu wa hadithi na fiqihi ambaye pia alikuwa msomi mashuhuri wa karne ya pili Hijiria. Ibn Sirin alizaliwa mjini Basra, kusini mwa Iraq na kuanza kujifunza elimu mbalimbali akiwa kijana mdogo. Alizipa umuhimu mkubwa hadithi za Bwana Mtume Muhammad (swa), huku akihifadhi na kunakili hadithi hizo kwa umakini mkubwa. Ni kutokana na hali hiyo ndipo wataalamu wengi wa hadithi wakazitilia maanani sana hadithi zilizopokelewa na Ibn Sirin. Ni vyema ikafahamika hapa kwamba, Ibn Sirin alibahatika kudiriki maisha ya masahaba 30 wa Mtukufu Mtume Muhammad (swa) na kunufaika na elimu na maarifa yao. Hii leo vitabu mbalimbali na kwa lugha tofauti vimeandikwa kutoka kwa msomi huyo.
