Ijumaa, Juni 14, 2019
Leo ni Ijumaa tarehe 10 Mfunguo Mosi Shawwal 1440 Hijria sawa na tarehe 14 Juni mwaka 2019 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 283 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa kwa jina la Charles Augustin de Coulomb. Msomi huyo alianza kufundisha masomo katika taaluma za umeme na sumaku baada ya kuhitimu masomo yake na kuandika vitabu vingi katika uwanja huo. Mbali na kufundisha, mwanafizikia Augustin de Coulomb aliendelea pia kufanya utafiti na hatimaye akafanikiwa kubuni kanuni katika sayansi ya fizikia iliyojulikana kwa jina Lake. De Coulomb aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 70.
Siku kama ya leo miaka 199 iliyopita, wanajeshi wa Misri wakiongozwa na Kamanda Muhammad Ali Pasha waliishambulia Sudan na kulikalia kwa mabavu eneo kubwa la ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Wakati huo huo Waingereza pia walilishambulia eneo la kusini mwa Sudan na kulikalia kwa mabavu. Hata hivyo wananchi wa Sudan wakiongozwa na Mahdi Sudani, mwaka 1881 walianzisha harakati ya ukombozi dhidi ya uvamizi wa Misri na Uingereza, na mwaka 1885 wakafanikiwa kutoa pigo kubwa kwa vikosi vamizi vya Misri na Uingereza na kukomboa sehemu kubwa ya ardhi ya nchi yao.
Siku kama ya leo miaka 189 iliyopita, wanajeshi wa Ufaransa waliwasili katika pwani ya Algeria huko kaskazini mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa oparesheni za kijeshi za Ufaransa zilizokuwa na lengo la kuikalia kwa mabavu na kuikoloni Algeria. Hata hivyo uvamizi huo wa kikoloni ulikabiliwa na mapambano makubwa ya wananchi dhidi ya maghasibu wa Kifaransa. Mapambano hayo ya kupigania ukombozi ya wananchi wa Algeria dhidi ya ukoloni wa Ufaransa yalipamba moto baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia. Hatimaye mwaka 1962 rais wa wakati huo wa Ufaransa alilazimika kuipatia Algeria uhuru kamili, kufuatia mashinikizo ya mapambano ya wananchi wa Algeria na upinzani wa fikra za waliowengi ndani ya Ufaransa kwenyewe na kimataifa.
Tarehe 24 Khordad miaka 38 iliyopita wawakilishi 120 wa Majlisi ya Ushaudi ya Kiislamu ya Iran (Bunge) waliwasilisha muswada wa kutokuwa na imani na Bani Sadr aliyekuwa rais wa wakati huo wa Iran. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kusambaratika mapambano ya wananchi dhidi ya wavamizi wa chama cha Baath kutoka Iraq katika hujuma iliyofanywa dhidi ya ardhi ya Iran kutokana na kukosa misaada ya dharura kutoka kwa Bani Sadr aliyekuwa Kamanda na Amri jeshi Mkuu, na vilevile hitilafu zilizojitokeza baina ya Rais wa nchi na mihimili mingine miwili ya dola.
Na siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, alifariki dunia Jorge Luis Borges, mwandishi mkubwa wa Amerika ya Latini. Luis alizaliwa mwaka 1899 nchini Argentina na kutokana na kutalii sana athari za wasomi wakubwa kama Edgar Allan Poe, Charles Dickens na Cervantes akafanikiwa kuinukia na kuwa hodari katika uwanja huo. Mwishoni mwa masomo yake, Jorge Luis Borges alijielekeza zaidi katika kazi ya uandishi na kuwa miongoni mwa waandishi mashuhuri wa visa na hekaya za kuchekesha huko Amerika ya Latini. Hata hivyo kutokana na upofu hakuweza kukamisha kazi zake. Luis ameandika vitabu vingi ambavyo vinapatikana katika maktaba mbalimbali za dunia.