Jumapili, tarehe 16 Juni, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 12 Shawwal 1440 Hijiria, sawa na tarehe 16 Juni 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1056 iliyopita, yaani sawa na tarehe 12 Shawwal miaka 384 iliyopita, alifariki dunia Ibrahim Bin Hilal Swabi, fasihi na malenga maarufu wa karne ya 14 Hijiria. Alizaliwa mjini Baghdad Iraq, ambapo akiwa kijana alianza kujifunza fani ya mashairi na fasihi na kupata umahiri mkubwa. Mwandishi huyo mashuhuri alitabahari pia katika taaluma ya hisabati, nyota na uhandisi. Ibrahim Bin Hilal Swabi ameacha athari nyingi zenye thamani kubwa kikiwemo kitabu kinachoitwa 'Taajul-Maathur' na 'Risaalat fii Ilmin-Nujuum.'
Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, yaani sawa na tarehe 16 Juni mwaka 1944, wanajeshi wa majini wa Marekani waliaza kushambulia kwa mabomu miji ya Japan sambamba na kuulenga mji wa Fokula ulioko kusini mwa nchi hiyo. Hayo yalijiri wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Aidha mashambulizi hayo yalifanyika kwa lengo la kuilazimisha Tokyo isalimu amri. Katika mashambulizi hayo makumi ya maelfu ya raia wa Japan waliuawa na kujeruhiwa, sambamba na kuangamizwa viwanda na mashamba ya nchi hiyo. Vita hivyo vilipelekea Marekani kushambulia kwa mabomu ya nyuklia miji miwili ya Japan ya Hiroshima na Nagasaki mwezi Oktoba mwaka 1945.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita sawa na tarehe 16 Juni 1963, Valentina Tereshkova mwanamke wa kwanza duniani mwanaanga kutoka Russia, alianza safari yake ya angani kwa kutumia safina ya anga iliyoitwa Vostok-6. Mwanake huyo alitua katika obiti ya ardhi wakati ambao Valery Bykovsky mwanaanga mwingine wa Russia alipokuwa akijishughulisha pia kuzunguka dunia. Safari ya Tereshkova katika anga za juu ilifanyika miaka miwili baada ya safari ya Yuri Gagarin ambayo ilikuwa ya kwanza kufanywa na mwanadamu katika anga hizo. Kwa muda wa masaa 70 na dakika 50 alizokuwa katika anga za juu, Tereshkova alizunguka dunia mara 48.
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita wananchi wa Soweto huko Afrika Kusini walianza harakati za mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa makuburu. Katika kipindi hicho Afrika Kusini ilikuwa ikitawaliwa na wazungu wachache waliodhibiti kila kitu na sheria zilizokuwa dhidi ya binadamu. Juni 16 mwaka 1976 maelfu ya wanafunzi wazalendo walifanya maandamano makubwa kupinga sera za kibaguzi katika sekta ya elimu ambayo yalikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa utawala wa kibaguzi. Mamia ya raia waliuawa na wengine kujeruhiwa.
Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, alifariki dunia Ayatullahil-udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani aalimu na marjaa mkubwa wa Kiislamu baada ya kuugua. Allamah Fadhil Lankarani alizaliwa mnamo mwaka 1310 Hijria Shamsia katika mji wa kidini wa Qum ulioko kusini mwa Tehran na kuanza kujifunza masomo ya dini akiwa kijana mdogo. Aidha alipata kustafidi na masomo ya walimu wakubwa wa zama zake kama vile Ayatullahil Udhma Burujerdi na Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu awarehemu. Ayatullahil Udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani aliweza kufikia daraja ya ijtihad katika kipindi kifupi.