Jumatatu, tarehe 17 Juni, 2019
Leo ni Jumatatu tarehe 13 Shawwal 1440 Hijria sawa na tarehe 17 Juni 2019.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita inayosadifiana na tarehe 27 Khordad 1358 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, Imam Khomeini (M.A) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuanzishwa Jihad ya Ujenzi wa taifa kwa lengo la kujitawala na kujitosheleza taifa la Iran na kujikwamua na umasikini na matatizo mbalimbali hasa vijijini. Kufuatia amri hiyo, wananchi wa matabaka mbalimbali wakiwemo wanafunzi, wanachuo na vijana wenye imani na wasomi waliungana ili kujenga na kukarabati maeneo yaliyokuwa duni na nyuma kimaendeleo. Jihadi ya ujenzi wa taifa ambayo ni matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu ilibadilisha sura ya maeneo mbalimbali duni nchini kutokana na hatua muhimu zilizochukuliwa za ujenzi wa miundo mbinu. Baadaye jihadi ya ujenzi ilibadilishwa na kuwa wizara na kisha kuunganishwa na wizara ya kilimo na kuwa Wizara ya Jihadi ya Kilimo.

Katika siku kama ya leo miaka 60 iliyopita Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Borujerdi Marjaa Taqlidi aliaga dunia. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Borujerd nchini Iran. Sayyid Hussein Tabatabai Borujerdi alibobea katika elimu za fiqhi, hadithi na tafsiri ya Qur'ani. Kipindi fulani alielekea mjini Najaf Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu na kubakia huko kwa miaka minane. Alikuwa na wanafunzi wengi ambao baadaye wakuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri. Miongoni mwa wanafunzi hao ni Shahid Murtadha Mutahhari, Sayyid Muhammad Hussein Beheshti, Ayatullah Jaafar Sobhani, Ayatullah Fazel Lankarani, Ayatullah Nasser Makarem Shirazi na wengine wengi.
Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita sawa na tarehe 17 Juni 1925, ulitiwa saini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za vijidudu na kemikali mjini Geneva Uswisi. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utumiaji vitani wa aina yoyote ya silaha za vijidudu, gesi zinazoua, sumu za kemikali na nyinginezo kama hizo ulipigwa marufuku. Licha ya kufikiwa makubaliano hayo, lakini baadhi ya nchi bado ziliendelea kutumia silaha hizo zilizopigwa marufuku dunia. Ujerumani ilitumia silaha za kemikali katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Marekani katika vita vya Vietnam na utawala wa zamani wa Iraq ulitumia silaha hizo wakati wa vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran.

Miaka 102 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, Mirza Muhamamad Taqi Shirazi Kiongozi wa Mapinduzi ya Iraq alitoa fatuwa ya jihadi dhidi ya mkoloni Muingereza. Baada ya Uingereza kutangaza vita dhidi ya utawala wa Othmania mwaka 1914 na kukaliwa kwa mabavu mji wa Basra, maulamaa wakubwa wa Najaf walitoa hukumu ya kukabiliana na mkoloni huyo. Miaka ya baadaye ilishuhudia kujitokeza makundi yaliyokuwa yakipinga uwepo wa Uingereza nchini Iraq.
Siku kama ya leo miaka 117 alifariki dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Twaha, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 83. Familia ya msomi huyo mkubwa inatokana na moja ya maulama mashuhuri wa Kiislamu. Sheikh Twaha alizaliwa mjini Najaf, Iraq na kupata elimu kwa mwanazuoni mashuhuri wa zama hizo yaani Sheikh Murtadha Answari, Sheikh Twaha alitabahari katika elimu ya fiq’hi, usulu fiq’hi, hadithi na tafsiri ya Qur’ani Tukufu.

Na katika siku kama ya leo miaka 529 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Zainuddin bin Ali al Shami maarufu kwa jina la Shahidi Thani, mwandishi wa kitabu cha Sherhul Lum'a. Alikuwa fakihi na mwanazuoni mahiri wa Kishia. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali kwa baba yake, Shahidi Thani alijiendeleza kielimu kwa wanazuoni wengine wa zama hizo na kuondokea kuwa mmoja wa wasomi watajika wa Kiislamu. Alifanya safari katika maeneo mbalimbali ya Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kufanya uhakiki. Alifanikiwa pia kulea wanafunzi wengi waliondokea kuwa wasomi mahiri. Zainuddin alitiwa mbaroni na mwaka 966 Hijria akauawa shahidi kufuatia njama zilizofanywa dhidi yake. Kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyo ni Sherh al Lumuatu Dimisqiyyah.
