Jun 18, 2019 02:23 UTC
  • Jumanne, Juni 18, 2019

Leo ni Jumanne tarehe 14 Mfunguo Mosi Shawwal 1440 Hijria inayosadifiana na Juni 18 mwaka 2019 Milaadia.

Miaka 22 iliyopita katika siku kama ya leo, Necmettin Erbakan Waziri Mkuu aliyekuwa na misimamo ya Kiislamu wa Uturuki alilazimika kujiuzulu kutokana na mashinikizo ya wanajeshi wa nchi hiyo. Chama cha Erbakan kilipata kura nyingi katika uchaguzi wa Disemba mwaka 1994 na kuunda Baraza la Mawaziri. Lakini wasekulari na makamanda wa jeshi walizuia kutekelezwa malengo ya serikali ya Arbakan. Waziri Mkuu huyo alikuwa akiamini kwamba kuwakandamiza wanaharaki wa Kiislamu nchini Uturuki ni kinyume na demokrasia na alipinga kuimarishwa uhusiano wa nchi hiyo na utawala ghasibu wa Israel. Lakini Baraza la Usalama wa Taifa la Uturuki ambalo lilikuwa na ushawishi mkubwa wa wanajeshi Februari 1997 lilitoa amri ya kumlazimisha Erbakan akabiliane na wanaharakati wa Kiislamu. Miezi minne baadaye waziri mkuu huyo alishtakiwa mahakamani kutokana na misimamo yake ya Kiislamu na kuzuia kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa muda wa miaka mitano.

Necmettin Erbakan

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, yalitiwa saini makubaliano ya pili ya kupunguza silaha za kistratijia yaliyojulikana kwa jina la Salt 2 kati ya Marais Leonid Brezhnev wa Urusi ya zamani na Jimmy Carter wa Marekani. Makubaliano hayo yalikuwa na lengo la kupunguza silaha za nyuklia duniani.

Salt 2

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita inayosadifiana na tarehe 18 Juni 1953 utawala wa kifalme ulisambaratika nchini Misri na kukaasisiwa mfumo wa Jamhuri baada ya Mfalme Farouq wa nchi hiyo kupelekwa uhamishoni. Kufuatia kushindwa Misri katika vita na Israel mwaka 1948 wananchi wa Misri walipoteza imani yao kwa Mfalme Farouq na hivyo hali ya ndani ya Misri kuanza kuharibika. Mwishowe liliundwa shirika la siri ndani ya jeshi lililopinga utawala wa mfalme huyo. Mwaka 1952 shirika hilo lilimlazimisha Mfalme Farouq kujiuzulu kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Muhammad Najib na Jamal. Mwaka mmoja baada ya kutangazwa Jamhuri ya Misri, Jenerali Muhammad Najib aliapishwa kuwa rais wa kwanza wa Misri. Mwaka mmoja baadaye Jamal Abdul Nassir alimuuzulu Muhammad Najib. Abdul Nassir alipata umaarufu mkubwa nchini Misri na duniani kote kwa sababu ya kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mfalme Farouq

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 68, Maxim Gorky, fasihi na mwandishi mashuhuri wa nchini Russia. Alexei Maximovich Peshkov maarufu kwa jna la Gorky, alikuwa mandishi mkubwa aliyezaliwa tarehe 28 Machi 1868 Miladia katika mji wa Gorky nchini Russia. Alianza kusoma kwa bidii elimu ya fasihi hapo mwaka 1895 na kupewa lakabu ya Maxim Gorky ambayo ilikuja kutumika kama jina lake na baadaye kufikia kupata umashuhuri mkubwa katika fani hiyo. Kwa kuzingatia kuwa alitokana na familia masikini, hivyo uandishi wa Maxim Gorky ulijikita sana katika kupiga vita umasikini na ujinga. Ameacha athari mbalimbali kikiwemo kitabu cha Mijeledi Mitatu kinachozungumzia maisha yake.

Maxim Gorky

Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, vilianza vita vya kihistoria vya Waterloo, vita vya mwisho vya Napoleon Banaparte na madola ya Ulaya. Katika vita hivyo majeshi ya serikali za Prussia na Uingereza yalikutana uso kwa uso na majeshi ya Napoleon Banaparte katika eneo lililokuwa likiitwa kwa jina la Waterloo. Katika vita hivyo na kutokana na kunyesha mvua kali na kuharibika njia zilizokuwa zikitumiwa kwa usafirishaji, hivyo zana za kijeshi  zilichelewa kufika uwanja wa vita sambamba na kuchelewa kufika kikosi cha mstari wa mbele cha Wafaransa. Kufuatia hali hiyo, Napoleon Banaparte akawa ameshindwa vibaya katika vita hiyo na hivyo kumfanya akimbie kwa kutumia meli kuelekea kisiwa cha Saint Helena na kufariki dunia miaka kadhaa baadaye kwenye kisiwa hicho.

Vita vya kihistoria vya Waterloo

Siku kama ya leo miaka 222 iliyopita, alifariki dunia kwa kuuawa huko Georgia, Agha Mohammad Khan Qajar, mfalme wa kwanza wa utawala wa Qajar nchini Iran. Agha Mohammad Khan Qajar alikuwa mtawala muovu sana nchini hapa. Baada ya kuangamizwa silsila ya watawala wa Zand, Khan Qajar aliingia madarakani kupitia udanganyifu, ukatili, umwagaji damu mkubwa na jinai zisizo na mfano dhidi ya Wairani huku mwaka 1174 Hijiria Shamsia akivishwa taji la kifalme mjini Tehran na hivyo akawa ameasisi utawala wa kiimla nchini. Katika kipindi cha utawala wake, maeneo tofauti ya Iran yalitangaza kujitenga kutokana na mtawala huyo kukosa weledi wa uongozi, kuendeleza anasa na kutenda jinai nyingi. Hata hivyo miaka miwili baadaye akiongoza jeshi la Iran kuishambulia Caucasus na Georgia, Agha Mohammad Khan Qajar aliuawa na wafanyakazi wake wawili na hivyo maisha yake yenye faili jeusi yakafikia tamati akiwa na umri wa miaka 63.

Agha Mohammad Khan Qajar

Na siku kama ya leo miaka 867 iliyopita alifariki dunia Qutbud-Din Rawandi, faqihi wa karne ya sita Hijria ambaye pia alikuwa mtaalamu wa hadithi na mtaalamu wa elimu ya aqida ya Kiislamu. Kwa miaka mingi alikwenda kwa wasomi wakubwa wa zama zake na kupata utaalamu mkubwa wa elimu za fiq'hi, hadithi na tafsiri ya Qur'ani Tukufu. Zipo athari kadhaa za msomi huyu mkubwa zinazokaribia vitabu 80 na  miongoni mwa kitabu hivyo ni "Tafsirul Qur'an", "Risaalatul-Fuqahaa", tahafutul falasifa, "Aayaatul-Ahkaam" na "Asbaabun-Nuzul."

Qutbud-Din Rawandi

 

Tags