Jumatatu tarehe 24 Juni 2019
Leo ni Jumatatu tarehe 20 Shawwal 1440 Hijria sawa na tarehe 24 Juni 2019.
Siku kama ya leo miaka 623 iliyopita mtaalamu wa lugha na mwandishi mashuhuri wa zama hizo Majduddin Abu Tahir Muhammad Yaaqub Firuzabadi aliaga dunia. Firuzabadi alikuwa pia hodari katika taaluma za hadithi na tafsiri ya Qur'ani na ameandika vitabu kadhaa katika taaluma hizo. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni "al Qamus" ambacho ni miongoni mwa kamusi muhimu za lugha ya Kiarabu. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni "Sifrul Saada" na "Tanwirul Miqyas".

Siku kama ya leo miaka 207 iliyopita, Napoleone Bonaparte mtawala wa Ufaransa akiwa na kikosi cha askari 350,000 alianza kufanya mashambulio dhidi ya utawala wa Russia wa Tsar. Miaka mitano kabla ya tukio hilo, nchi mbili hizo zilikuwa zimetiliana saini mkataba wa kutoshambuliana kijeshi. Hata hivyo taratibu uhusiano baina ya tawala mbili hizo ulianza kuharibika, na hivyo kumfanya Bonaparte afikie hatua ya kuandaa jeshi kubwa na kuishambulia Russia na kisha kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Moscow. Hata hivyo hali mbaya ya hewa yaani baridi kali na kutowafikia wanajeshi wa Kifaransa vifaa muhimu na suhula za kivita, kuliwafanya askari hao wakabaliwe na hali ngumu katika medani ya vita. Hali hiyo ilimlazimisha Bonaparte atoe amri ya kurejea nyuma vikosi vyake. Wakati wa kujiri zoezi hilo, askari jeshi wapatao 30,000 wa Kirusi waliwashambulia askari wa Bonaparte na kuwaua wengi miongoni mwao. Akiwa amebakiwa na askari 30,000 tu, Bonaparte aliikimbia Russia na kufanikiwa kuwasili Paris Ufaransa Desemba mwaka 1812.
Katika siku kama ya leo miaka 176 iliyopita, tanuu za feleji maarufu kwa jina la tanuu za Bessemer zilivumbuliwa. Mvumbuzi wa tanuu hizo alikuwa Mwingereza Henry Bessemer. Tanuu hizo zilitumika huko Uingereza kwa mara ya kwanza na leo hii zinatumika katika masuala mbalimbali viwandani.
Tarehe 24 Juni miaka 207 iliyopita, Caracas mji mkuu wa Venezuela ulidhibitiwa na Simon Bolivar ikiwa ni wakati wa mapambano ya mpigania uhuru huyo dhidi ya wakoloni kwa ajili ya kuyakomboa maeneo ya Amerika ya Kusini. Mkoloni Muhispania alishindwa katika vita hivyo vilivyodumu kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja na baada ya ushindi huo Simon Bolivar anayejulikana kama shujaa wa mapambano dhidi ya wakoloni huko Amerika Kusini, aliasisi Shirikisho la Colombia Kubwa. Shirikisho hilo lilijumuisha nchi za Venezuela, Colombia, Panama na Ecuador, na Bolivar alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa shirikisho hilo.