Jun 29, 2019 02:57 UTC
  • Jumamosi tarehe 29 Juni 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 25 Shawwal 1440 Hijria sawa na tarehe 29 Juni 2019.

Siku kama ya leo miaka 1292 iliyopita Imam Ja'far Sadiq mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake, aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala dhalimu wa Kiabbasi Mansur al Dawaniqi. Imam Sadiq alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Muhammad Baqir. Imam Sadiq ambaye kipindi cha uongozi wake kilisadifiana na zama za mapigano makali kati ya watawala wa Kiumawi na Kiabbasi, alitumia fursa hiyo kueneza elimu na maarifa sahihi ya Kiislamu. Alifanikiwa kulea na kutayarisha wasomi hodari katika taaluma mbalimbali kama tiba, kemia, hesabati, nujumu hadithi na kadhalika. Jabir bin Hayyan ambaye anatambuliwa hii leo kuwa ndiye baba wa elimu ya kemia alikuwa mwanafunzi wa Imam Ja'far Saqid (as). Ushawishi wa Imam ulienea kwa kasi katika ulimwengu wa Kiislamu, jambo ambalo halikuwafurahisha watawala wa Kiabbasi. Hatimaye mtawala Mansur al Dawaniqi aliamuru Imam apewe sumu. Mtukufu huyo aliuawa shahidi kwa sumu hiyo katika siku kama ya leo na akazikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita vilianza Vita vya Pili vya Balkan kati ya Bulgaria na umoja wa nchi za Serbia, Ugiriki, Montenegro, Romania na utawala wa Othmania. Karibu mwaka mmoja kabla ya hapo katika Vita vya Kwanza vya Balkan, Bulgaria, Serbia, Ugiriki na Montenegro zilizokuwa sehemu ya utawala wa Othmania, zilianzisha uasi dhidi ya ufalme huo, na kutokana na kudhoofika utawala huo nchi hizo zilifanikiwa kupata uhuru. Kwa msingi huo karibu asilimia 80 ya nchi zilizokuwa chini ya himaya ya Othmania huko Ulaya zikatoka chini ya udhibiti wa dola hilo. Hata hivyo nchi zilizoshinda katika Vita vya Kwanza vya Balkan hazikuweza kufikia makubaliano ya kugawana ardhi zilizokombolewa sababu iliyopelekea kuanza Vita vya Pili vya Balkan. Vita vya Balkan viliandaa mazingira ya kuanza kwa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Vita vya Pili vya Balkan

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita yaani tarehe 29 Juni mwaka 1976, muungano wa visiwa vya Ushelisheli ulipata uhuru wake na kila siku kama hii huadhimishwa katika visiwa hivyo kama siku ya taifa. Hadi kufikia katikati ya karne ya 18, wakati ambao Wareno walikuwa wakiikalia kwa mabavu ardhi hiyo, visiwa vya Ushelisheli vilikuwa havijagunduliwa na havikuwa na wakazi. Mwishoni mwa karne ya 18 wakati ulipopamba moto wa mapinduzi ya Ufaransa, wanajeshi wa Uingereza waliokuwa katika eneo la Afrika waliivamia Ushelisheli. Mapambano ya kuikomboa nchi hiyo yalipamba moto mwaka 1960 na kuendelea, na miaka 16 iliyofuata visiwa vya Ushelisheli vikawa huru na kuasisi mfumo wa Jamhuri. Ushelisheli inaundwa na visiwa kadhaa vilivyoko katika bahari ya Hindi ikipakana na Madagascar.

Visiwa vya Ushelisheli

Tarehe 29 Juni miaka 27 iliyopita aliuawa Mohamed Boudiaf aliyekuwa Mkuu wa Baraza la Serikali ya Algeria. Mohamed Boudiaf alikuwa rais wa nne wa Algeria tangu nchi hiyo ilipopata uhuru. Alijiunga na harakati za siri za kupinga ukoloni wa Ufaransa akiwa bado kijana na kupanda ngazi katika harakati ya wananchi wa Algeria iliyokuwa ikiendesha harakati za siri dhidi ya wakoloni wa Kifaransa. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya wananchi wa Algeria hapo mwaka 1962 Mohamed Boudiaf aliunda serikali ya kisoshalisti akishirikiana na Ahmed Ben Bella. Alikimbilia nje ya nchi kufuatia mapinduzi ya Houari Boumediene dhidi ya serikali Ben Bella na kurejea Algeria baada ya kujiuzulu Chadli Bendjedid na kuunda baraza la uongozi. Kama walivyokuwa viongozi wengi wa baada ya uhuru wa Algeria, Mohamed Boudiaf alikuwa mpinzani mkubwa wa fikra za Kiislamu na baada ya kushika madaraka alivunja harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo iliyokuwa imeshinda uchaguzi wa Bunge na kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo. Hatua hiyo ilisababisha machafuko ya ndani nchini Algeria na tarehe 29 Juni 1992 alipigwa risasi na kuuawa na mmoja wa walinzi wake. 

Mohamed Boudiaf