Jul 01, 2019 01:32 UTC
  • Jumatatu tarehe Mosi Julai 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 27 Shawwal 1440 Hijria sawa na tarehe Mosi Julai 2019.

Miaka 1099 iliyopita mwafaka na leo, alizaliwa malenga wa Kiirani Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. Kipindi cha ujana wake kiliambatana na kumalizika kwa kipindi cha utawala wa Wasaman na mwanzoni mwa zama za utawala wa Waghaznavi. Kwa sababu hiyo malenga huyu Mfarsi alitunga mashairi kadhaa ya kusifu tawala hizo mbili. Fauka ya hayo Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad (saw) na kizazi chake hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Kesa-i Marvazi mbali na kusifika kwa usomaji mashairi, lakini pia alitoa waadhi na hekima kupitia mashairi yake ya Kifarsi. Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameacha tungo kadhaa za mashairi.

Abu Is'haq Kesa-i Marvazi

Siku kama ya leo miaka 231 iliyopita alizaliwa Jean Victor Poncelet mwasisi wa uchambuzi wa maumbo. Victor Poncelet aliyekuwa mtaalamu wa hisabati maarufu wa nchini Ufaransa, alitambulika kuwa mwasisi wa uchambuzi wa maumbo na ambaye alizaliwa tarehe Mosi Julai 1788 Miladia. Aidha Poncelet alikuwa mmoja wa maafisa wa jeshi la Napolione na katika kipindi cha kurejea nyuma jeshi la Ufaransa kutoka Urusi ya zamani, alitekwa na Warusi. Hata hivyo katika kipindi cha kutekwa alijiendeleza kielimu na kufanikiwa kuhitimu elimu yake ya uhandisi. Jean Victor Poncelet alifariki dunia tarehe 22 Disemba 1867.

Jean Victor Poncelet

Siku kama ya leo miaka 152 iliyopita, nchi ya Canada ilijitangazia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Canada iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 Miladia na kuanzia wakati huo kwa zaidi ya karne mbili, Uingereza na Ufaransa zilikuwa zikishindana katika ardhi ya nchi hiyo kwa lengo la kupanua udhibiti wao. Ushindani huo ulipelekea kujiri vita kati ya mataifa hayo ya kikoloni ambapo mwaka 1689 Miladia vita hivyo vilimalizika kwa kushindwa Ufaransa, katika vita hivyo ambavyo vilidumu karibu miaka 75. Kuanzia mwanzoni mwa karne ya 19 taratibu zilianza harakati za kupigania uhuru wa Canada ambapo zilizaa matunda mwaka 1867 Miladia katika siku kama ya leo.

Bendera ya Canada

Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo, sehemu mbili za Somalia ya Uingereza na ya Italia ziliungana na kuunda nchi moja ya Somalia yenye kujitawala. Karne kadhaa nyuma, Somalia iliwahi kujitawala kwa kipindi kifupi. Mwaka 1884 Uingereza iliiweka katika himaya yake sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Miaka mitano baadaye Italia nayo ikakoloni baadhi ya sehemu za Somalia. Harakati za mapambano za Muhammad Abdullah Hassan dhidi ya Waingereza kuanzia mwaka 1901 hadi 1920 hazikusaidia kitu. Mwaka 1950 Umoja wa Mataifa uliitaka Italia iandae mazingira ya kujitawala na kuwa huru Somalia.

Ramani ya Somalia

Katika siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, nchi ndogo ya Burundi ilijitangazia uhuru wake. Ardhi ya Burundi pamoja na Rwanda ilikuwa sehemu ya makoloni ya Mjerumani huko Afrika Mashariki kuanzia mwaka 1899 hadi 1917. Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kushindwa Ujerumani katika vita hivyo, Umoja wa Mataifa uliikabidhi Ubelgiji ardhi ya Burundi na mwaka 1946, yakatambuliwa rasmi mamlaka na utawala wa Ubelgiji kwa nchi hiyo. Mwaka 1962 Burundi ilipata uhuru ikiwa na mfumo wa utawala wa Kifalme. Hata hivyo miaka minne baadaye wapigania jamhuri walimuondoa madarakani mfalme na kuanzisha mfumo wa serikali ya jamhuri. 

Bendara ya Burundi

Na siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, Rwanda ilipata uhuru. Rwanda ina historia inayofanana na jirani yake wa kusini yaani Burundi ambapo kabla ya nchi hizo kujitangazia uhuru zilikuwa zikikoloniwa na Ubelgiji. Baada ya mapambano mtawalia ya wapigania uhuru wa Rwanda, hatimaye mnamo mwaka 1962, nchi hiyo ilipata uhuru na kabila kubwa la Wahutu likashika hatamu za uongozi wa nchi. Mwaka 1973, Meja-Jenerali Juvenal Habyarimana alichukua madarakani baada ya kufanya mapinduzi yasiyo na umwagaji damu. Hata hivyo mwaka 1994 kulitokea mauaji ya kimbari ambapo zaidi ya watu laki 8 waliuawa wengi wao wakiwa ni wa kabila la Kitutsi.

Bendera ya Rwanda