Jumanne, Julai 2, 2019
Leo ni Jumanne tarehe 28 Mfunguo Mosi Shawwal 1440 Hijria sawa na Julai Pili mwaka 2019 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 967 iliyopita alizaliwa Sanai Ghaznawi Hakim Abul-Majd Majdud ibn Ādam Sanai Ghaznavi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran mjini Ghazni. Ghaznavi alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala akiwa bado kijana mdogo. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusomea elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kusoma mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Alianzisha pia mfumo wa aina yake katika usomaji wa mashairi. Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho kina muundo wa mashairi na ndani ya kitabu hicho malenga huyo mkubwa ameweka wazi fikra zake za kimaadili na irfani. Vitabu vya 'Elahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq,' ni miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi.
Miaka 94 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Patrice Lumumba mhandisi wa uhuru wa Kongo. Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa. Lumumba aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokita "Kongo, Nchi Yangu."
Tarehe Pili Julai miaka 58 iliyopita aliaga dunia mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway. Alizaliwa mwaka 1899 na kwa muda fulani alikuwa mwandishi huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway alianzisha mbinu ya kuandika riwaya na tungo fupi fupi na alikuwa akitumia lugha nyepesi na inayoeleweka. Mwaka 1954 mwandishi Ernest Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi. Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na For Whom The Bell Tolls".
Na tarehe 11 Tir miaka 37 iliyopita Ayatullah Muhamad Saduqi alimu mkubwa, mwanamapambano na Imamu wa Ijumaa wa mji wa Yazd huko katikati mwa Iran, aliuawa shahidi na vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqiin na kuwa shahidi wa nne aliyeuawa katika mihrabu ya swala katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Ayatullah Muhammad Saduqi alikamilisha masomo yake ya kidini katika Hauza ya mji mtakatifu wa Qum, Iran na kustafidi na bahari kubwa ya elimu kutoka kwa walimu mashuhuri wa kituo hicho cha kielimu kama vile Ayatullah Burujerdi na Ayatullah Khansari.