Jumamosi, 03 Agosti, 2019
Leo ni Jumamosi tarehe Mosi Mfunguo Tatu Dhulhija 1440 Hijria mwafaka na tarehe 3 Agosti 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Bibi Fatima Zahra binti ya Mtume SAW alianza maisha mapya baada ya kufunga ndoa na Imam Ali bin Abi Talib AS. Bibi Fatima alikuwa mwanamke mwema, mtukufu na kigezo bora cha Waislamu. Masahaba mashuhuri walijitokeza kumposa binti huyo wa Mtume. Hata hivyo, Mtume alikuwa akimjibu kila aliyekwenda kumposa binti yake huyo kwamba, suala la ndoa yake liko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Baada ya kufunga ndoa, watukufu hao walianza maisha yao ya kawaida kabisa yaliyojaa huruma, upendo na masuala ya kiroho na kimaanawi. Familia hiyo imeitunuku dunia shakhsia adhimu na wa kupigiwa mfano kama Imam Hassan, Imam Hussein na Bibi Zainab (as). ***
Miaka 854 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa msomi na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu, Ibn Abil Hadid katika eneo la Madain, Iraq ya sasa. Abu Hamid Abdul Majid bin Muhammad Madaini maarufu kama Ibn Abil Hadid Muutazili alikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa wa Muutazila, mtaalamu wa elimu za usuli, falsafa, teolojia na malenga. Kitabu chake mashuhuri cha Sherhe ya Nahjul Balagha ni kielelezo cha mapenzi ya Ibnu Abil Hadid kwa Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) na familia ya Mtume Muhammad (saw) kwa ujumla. Kitabu hicho ni miongoni mwa vitabu muhimu sana katika nyanja za fasihi, historia na teolojia na kimekuwa marejeo ya wanazuoni wengi kwa miaka mingi. Athari nyingine za Ibn Abil Hadid ni pamoja na Al 'Abqariyul Hisaan, Al Qasaidul Sab'ul 'Alawiyaat (القصائد السبع العلویات) na Sherhul Muhassal. Ibn Abil Hadid alifariki dunia mwaka 656 Hijria akiwa na umri wa miaka 70. ***
Miaka 527 iliyopita katika siku kama ya leo, ilianza safari kubwa zaidi ya uvumbuzi ya baharia wa Kiitalia Christopher Columbus. Christopher Columbus alipewa jukumu la kuvumbua njia mpya ya kuelekea India katika makubaliano yaliyofikiwa kati yake na mfalme na malkia wa Uhispania wa wakati huo. Kwa sababu hiyo Christopher Columbus aliondoka katika bandari ya Paulus huko Uhispania akiwa na meli tatu na mabaharia 120 na hatimaye walifika katika nchi kavu baada ya kuwa baharini kwa siku 33. Wakati huo Columbus na wenzake walidhani kuwa wamewasili India lakini walikuwa wamevumbua bara America bila ya wao kujua. ***
Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, meli ya kwanza ilipita katika Kanali ya Panama na kwa utaratibu huo, kanali hiyo ikawa imefunguliwa. Wahandisi wa Kifaransa ndio walioanza kujenga mfereji huo wa Panama na baadaye Wamarekani wakaikamilisha kazi hiyo. Kujengwa mfereji huo wenye kilomita 68, kuliunganisha bahari mbili za Pacifi na Atlantic. ***
Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Niger iliyoko magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru kutoka kwa Ufaransa. Kuanzia karne ya 18 Niger ilianza kuwa chini ya Ufaransa, na ulipofika mwaka 1922 Paris ilianzisha kambi za kijeshi nchini humo. Niger inapakana na Libya, Chad, Mali na Benin. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, katika hatua yake nyingine ya kigaidi utawala wa Kizayuni wa Israel uliwauwa Izzuddin Qalq mjumbe wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na naibu wake huko Paris, Ufaransa. Shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD katika miongo miwili ya 70 na 80 liliwauwa kigaidi viongozi wengi wa PLO ili kuidhoofisha harakati hiyo na kuilazimisha kuanzisha mazungumzo eti ya mapatano kati ya Wapalestina na Israel. ***