Alkhamisi tarehe 8 Agosti 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 6 Dhulhuja 1440 Hijria sawa na tarehe 8 Agosti 2019.
Siku kama ya leo miaka 2352 iliyopita sawa na tarehe 8 Agosti 333 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, ilianza kazi ya ujenzi wa mji wa Alexandria nchini Misri, ambao leo hii unahesabiwa kuwa moja kati ya bandari muhimu kusini mwa Bahari ya Mediterranean. Ujenzi huo ulifanyika kwa amri ya Alexander Macedon huko kaskazini mwa Misri.
Siku kama ya leo miaka 1182 iliyopita, yaani sawa na tarehe 6 Dhul-Hijjah mwaka 258 Hijiria, alizaliwa Abu Ali Muhammad ibn Hammam, mmoja wa maulama mashuhuri wa Iran. Ibn Hammam alikuwa akiishi mjini Baghdad, Iraq ambapo alifanikiwa kusoma elimu ya hadithi kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake. Aidha msomi huyo alikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao walijifunza toka kwake elimu ya hadithi na elimu nyingine za Kiislamu. Msomi huyo ameacha vitabu kadhaa katika uga wa hadithi.

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, mamia ya mahujaji wa Iran na wengine kutoka nchi tofauti waliokuwa wameenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu mjini Makka na wakiwa katika hali ya kutekeleza ibada ya faradhi ya kujitenga na mushrikina, waliuawa shahidi na vibaraka wa utawala wa Saudi Arabia. Ni vyema kukumbusha kuwa, mahujaji wa Iran kwa miaka yote huwa wanatekeleza ibada hiyo kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo mbali na kuwasisitizia Waislamu kuungana, hutangaza kujitenga na maadui wa Uislamu hususan Marekani na utawala haramu wa Israel. Ibada hiyo ambayo hufanyika kwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, huwa na taathira kubwa katika msimu wa Hija. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Imam Khomein mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akasisitizia sana umuhimu wa ibada ya kujitenga na mushrikina na maadui wa dini ya Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita mwafaka na tarehe 17 Mordad 1371 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Alhaj Sayyid Abul Qassim al Mussawi al Khoui, faqihi na marjaa mkubwa wa Kiislamu duniani, akiwa na umri wa miaka 96. Mwanachuoni huyo mashuhuri alizaliwa katika mji wa Khoui ulioko kaskazini magharibi mwa Iran na akiwa katika umri wa ubarobaro, alifuatana na baba yake mjini Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu. Katika zama za umarjaa wake, Ayatullahil Udhma al Khoui alitoa fatwa inayosisitiza udharura wa kuilinda Palestina na kuikomboa Quds Tukufu kutoka mikononi mwa Wazayuni maghasibu. Alimu huyo mkubwa ameacha vitabu vingi vikiwemo 'Jawaahirul Usuul', 'Muntakhabu Rasaail', 'al Bayaan Fii Tafsiiril Qurani' na "Misbahul Faqaha".
Miaka 21 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 8 Agosti 1998, wanamgambo wa kundi la Taliban nchini Afghanistan waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Mazar Sharif ulioko kaskazini mwa nchi hiyo. Baada ya kukaliwa kwa mabavu mji huo, wanamgambo wa Taleban waliushambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji huo na kuwauwa shahidi wanadiplomasia 8 wa Kiirani na mwandishi mmoja wa habari. Kundi la Taliban liliasisiwa mwaka 1994 kwa ufadhili na usaidizi wa Marekani na Pakistan na kufanikiwa kuikalia sehemu kubwa ya ardhi ya Afghanistan.