Jumanne, tarehe 10 Septemba, 2019
Leo ni Jumanne tarehe 10 Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria mwafaka na tarehe 10 Septemba mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya. Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya. Baada ya kupambana kishujaa, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi katika siku kama ya leo.
Miaka 105 iliyopita yaani tarehe 10 Septemba mwaka 1914 kulitokea vita baina ya majeshi ya Ujerumani na Russia kando kando ya ziwa la Mazury. Vita hivyo vilianza kufuatia kuzuka Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kujiunga Russia na kambi ya nchi waitifaki. Katika vita hivyo vya Mazury, Wajerumani wakiongozwa na kamanda Paul Von Hindenburg walifanikiwa kupata ushindi na kuwauwa takribani wanajeshi 20,000 wa Russia na kuwateka nyara wengine 45,000. Hatimaye mwaka 1917 baada ya kutokea mapinduzi nchini Russia, nchi hiyo ilijiondoa katika VitaVikuu vya Kwanza vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulitokea katika eneo la Orleansville kusini magharibi mwa Algeria. Janga hilo la mtetemeko wa ardhi lilisababisha mji mmoja uliokuwa na wakazi 30,000 kuangamia na watu 10,000 kupoteza maisha yao. Fauka ya hayo, makumi ya maelfu ya wananchi wa kusini magharibi mwa Algeria walibaki bila ya makazi. Mtetemeko huo vilevile ulitoa pigo kubwa kwa miundo mbinu ya uchumi wa nchi hiyo.
Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita yaani tarehe 19 Shaharivar aliaga dunia Sayyid Mahmoud Talaqani kiongozi wa kidini, mwanaharakati wa Kiirani, mwanamapambano na mfasiri wa Qur'ani Tukufu. Ayatullah Talaqani alikuwa akifuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa ya Iran tangu akiwa kijana mdogo. Kipindi fulani alitiwa nguvuni na kufungwa jela miaka miwili na utawala wa Kitaghuti wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliteuliwa na Imam Khomeini kuwa Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Imam wa Swala ya Ijumaa ya Tehran.
Na Tarehe 10 Septemba mwaka 1990 Samuel Kanyon Doe aliyekuwa rais wa jamhuri ya Liberia aliuawa na kundi la waasi. Doe alishika madaraka ya nchi mwaka 1980 akiwa sajenti mwenye umri wa miaka 29 tu baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akitumia umaskini, kupanda kwa gharama za maisha na hali mbaya ya wananchi. Hata hivyo utawala wa kidikteta wa Samuel Doe haukufanikiwa kupunguza machungu na mashaka ya Waliberia bali kinyume chake alipanua zaidi hitilafu za kikabila na kuzidisha matatizo ya kiuchumi na kijamii. Vilevile alitayarisha uwanja wa kuporwa zaidi utajiri wa madili ya almasi ya nchi hiyo kupitia njia ya kupanua zaidi uhusiano wa Liberia na Marekani na utawala haramu wa Israel. Mauaji ya Samuel Doe yalifuatiwa na vita vya ndani nchini Liberia ambavyo viliendelea kwa kipindi cha miaka 15 na kusababisha vifo vya watu karibu laki mbili na nusu.