Sep 22, 2019 23:59 UTC
  • Jumatatu tarehe 23 Septemba 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 23 Muharram 1441 Hijria sawa na Septemba 23 mwaka 2019.

Miaka 344 iliyopita katika siku kama ya leo, Valentin Conrart mwandishi na mwanafasihi wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 72. Alizaliwa mwaka 1603 katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na fasihi ya lugha na kwa msingi huo ndio maana alipokuwa katika rika la ujana, Valentin Conrart akawa na mapenzi na taaluma ya fasihi ya lugha na taratibu akaanza kujihusisha na fani ya uandishi.

Siku kama ya leo miaka 232 iliyopita aliaga dunia Allamah Mulla Muhammad Mahdi Naraqi, mwanazuoni na msomi mkubwa wa Kiislamu. Baada ya kuhitimu masomo ya awali nchini Iran, Mahdi Naraqi alielekea Najaf nchini Iraq kwa lengo la kuzidisha elimu na alipata elimu kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Baada ya hapo Allamah Mulla Mahdi Naraqi alianza kufanya utafiti, kufundisha na kuandika vitabu. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Allamah Naraqi ni "Jaamiul Sa'adat" na " Anisul Muwahhidin".

Allamah Mulla Muhammad Mahdi Naraqi

Katika siku kama ya leo miaka 117 iliyopita sawa na tarehe Mosi Mehr 1281 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ruhullah al Musawi Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu, aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi, Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul Karim Hairi na Muhammad Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa ya kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa. Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.

Imam Ruhullah al Musawi Khomeini

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita sawa na Septemba 23 mwaka 1932, Saudi Arabia iliasisiwa na Abdulaziz bin Saud akawa mfalme wa nchi hiyo. Bara Arabu au Hijaz ni mahali alipotokea Mtume wa Uislamu Muhammad S.A.W. Saudi Arabia ilijitoa chini ya udhibiti wa utawala wa Abassiya mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria na hadi karne kadhaa badaye, nchi hiyo iliendelea kuwa na ukosefu wa amani. Jitihada za al Saud za kutaka kuiongoza Saudia zilianza katikati mwa karne ya 18 na kushika kasi zaidi mwanzoni mwa karne ya 20. 

Bendera ya Saudia

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, aliaga dunia Sigmund Freud daktari wa magonjwa ya akili raia wa Austria. Sigmund alizaliwa mwaka 1856. Daktari huyo alifanya utafiti na kuchunguza matatizo mbalimbali ya kiakili yanayomkumba binadamu na kutoa maoni na nadharia mpya kuhusu chanzo cha magonjwa ya akili. Kwa sababu hiyo anahesabiwa kuwa mwasisi wa elimu ya uchunguzi wa kisaikolojia au Psychoanalysis.

Sigmund Freud

Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita Haram takatifu ya Maimamu al Hadi na Hassan al-Askari katika mji wa Samarra nchini Iraq, ziliharibiwa vibaya kwenye mashambulizi kadhaa ya miripuko ya mabomu yaliyofanywa na makundi ya kigaidi na kusababisha hasara kubwa za mali na watu. Maimamu hao ni wajukuu wa Mtume Bwana Mtume Muhammad SAW na walikuwa na nafasi kubwa ya kielimu na wacha-Mungu wangu katika zama zao. Kitendo cha kuharibiwa eneo hilo kiliwakasirisha mno Waislamu duniani hususan wafuasi wa Ahlul Bait wa Mtume (saw). Shambulio hilo lilifanyika kwa lengo la kuzusha ufa katika safu za Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni nchini Iraq.

Shambulizi dhidi ya haram ya Maimamu al Hadi na Hassan al-Askari