Jumapili, 6 Oktoba, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 7 Mfunguo Tano Swafar 1441 Hijiria, sawa na tarehe 6 Oktoba 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1391 iliyopita, yaani sawa na tarehe 7 Safar mwaka 50 Hijiria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia mjini Madina. Mtukufu huyo aliishi miaka saba ya mwanzo wa umri wake pamoja na babu yake Mtume Muhammad (saw) ambapo aliweza kunufaika na mafunzo na maarifa ya dini Tukufu ya Kiislamu. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as). Baada ya kufariki dunia Imam Ali (as) Waislamu walimpa baia Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza, ambapo hata hivyo baada tu ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo alikabiliwa na njama pamoja na ukwamishaji mambo wa Muawiyah bin Abi Sufiyan. Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi aliloachiwa na baba yake kwa ajili ya kumkabili Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah. Imam Hassan aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufyan.
Siku kama ya leo katika kalenda ya Wairani, yaani tarehe 7 Swafar, inatambuliwa kwa jina la Salman Farsi kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuchimbwa handaki kando ya mji wa Madina kwa lengo la kuulinda mji huo kutokana na mashambulizi ya Maquraishi. Siku hii imeitwa jina hilo kutokana na jina la sahaba huyo mashuhuri wa Mtume Muhammad (saw) na mmoja wa wafuasi watiifu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, Salman Farsi alikuwa mmoja wa wakulima wa Iran akiitwa kwa jina la 'Ruzbeh' huku utotoni mwake akiwa muumini wa dini ya Uzartoshti. Alipokuwa kijana Salman Farsi alijiunga na dini ya Ukristo ambapo pia alisafiri mjini Sham na kujifunza utawa wa Kikristo. Katika kipindi hicho alipata kuishi katika miji ya Sham, Nusaybin (Uturuki ya leo) na Mosul, Iraq. Hata hivyo baada ya kusikia utabiri wa Wakristo juu ya kudhihiri kwa Mtume wa Mungu katika ardhi za Kiarabu, akaamua kuhamia Hijaz na kufikishwa mjini Madina akiwa kama mtumwa. Akiwa mjini Madina alipata kukutana na Mtume wa Allah (saw) na kumwamini. Baada ya hapo Mtume alimnunua na kumuachia huru na kumwita jina la Salman Farsi. Katika vita mbalimbali sahaba huyo alikuwa mstari wa mbele pamoja na Mtume (saw) sambamba na kutoa ushauri, kama ambavyo pia ndiye aliyetoa pendekezo la kuchimbwa handaki kando ya mji wa Madina wakati wa kujiri vita vya Ahzab. Kufuatia ushauri wa Salman Farsi Waislamu waliweza kuibuka na ushindi na kutoa pigo kubwa kwa washirikina wa Makka. Baada ya kufariki dunia Mtukufu Mtume (saw), Salman Farsi alikuwa kati ya wafuasi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as).
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita sawa na tarehe 6 Oktoba mwaka 1973, vilianza vita vya nne kati ya Waarabu na utawala ghasibu wa Kizayuni. Katika siku hiyo jeshi la Misri lilivishambulia vikosi vya utawala huo haramu katika oparesheni ya kushtukiza katika upande wa pili wa Mfereji wa Suez. Baada ya kuvunja mstari imara wa ulinzi wa Barlow vikosi hivyo vikafanikiwa kuingia katika jangwa la Sinai. Katika vita hivyo vikosi vya Misri na Syria viliyatia hasara kubwa majeshi ya utawala wa Israel na idadi kadhaa ya ndege za kivita za Wazayuni kusambaratishwa. Hata hivyo kutokana na hatua ya Marekani ya kuupatia silaha za kisasa utawala huo wa Kizayuni Waarabu walipoteza baadhi ya ushindi waliokuwa wameupata katika vita hivyo.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, nchi za Kiarabu zinazouza nje mafuta zilianza kutekeleza vikwazo vya mafuta dhidi ya Marekani, Uingereza na makampuni yanayouuzia mafuta utawala wa Kizayuni wa Israel. Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na uungaji mkono mkubwa wa Marekani na Uingereza kwa utawala ghasibu wa Israel katika vita vya Israel dhidi ya Syria na Misri. Hatua hiyo ilipandisha sana bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa na kutoa pigo kubwa kwa nchi hizo za Magharibi. Muda mfupi baadaye nchi za Kiarabu zilikiuka vikwazo hivyo vya mafuta na kuanza tena kuiuzia mafuta Marekani na Uingereza. Vikwazo hivyo vilionyesha kuwa nchi za Kiislamu zina silaha muhimu inayoweza kutumiwa dhidi ya uungaji mkono mkubwa wa nchi za Magharibi kwa utawala katili wa Israel.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, yaani tarehe 6 Oktoba 1981, maafisa kadhaa wa kundi la Kiislamu la "Al-Jihad" walimshambulia na kumuua rais wa wakati huo wa Misri Muhammad Anwar Sadat. Rais huyo aliuawa kwa sababu ya kutia saini makubaliano ya udhalilishaji ya Camp David mnamo mwaka 1978 na utawala ghasibu wa Kizayuni sambamba na kuutambua rasmi utawala huo haramu. Kufuatia hatua hiyo rais huyo alihesabiwa kuwa msaliti wa malengo matukufu ya Waislamu na Waarabu. Kwa upande mwingine hatua hiyo ilipelekea kutengwa Misri na nchi za Kiislamu. Ni kwa ajili hiyo ndipo makundi ya Kiislamu na wanamapambano wa Misri wakaamua kumuua Sadat, ambaye alionekana kuwa msaliti mkubwa kwa kuutambua rasmi utawala huo ghasibu unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu. Aliyetekeleza mauaji hayo alikuwa Khalid Islambuli, mmoja wa maafisa wa jeshi la Misri wakati huo.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya jamii wa Kifaransa kwa jina la Raymond Aron. Aron alizaliwa mwaka 1905. Msomi huyo wa Kifaransa alikuwa akifundisha pia taaluma hiyo ya masuala ya jamii katika Chuo Kikuu cha Sorbonne, Paris kwa miaka kadhaa. Vilevile alikuwa akiandika makala katika majarida ya Le Figaro na Express mjini Paris. Raymond Aron ameandika vitabu vingi na hapa tunaweza kuashiria vitabu vyake vichache alivyovipa majina ya "Kuanza Vita vya Nyuklia, "Mapambano ya Kitabaka" na "Miaka ya Mwishoni mwa Karne".
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Shahrivar 1369 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar-ashi Najafi mmoja wa Marajii na viongozi wa juu wa Kiislamu hapa nchini, akiwa na umri wa miaka 96. Alimu huyo alisoma elimu za fiqihi, usul fiqihi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani, teolojia na misingi ya kimaadili katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Kadhimain na Najaf nchini Iraq. Miongoni mwa athari kubwa zilizoachwa na Ayatullah Mar-ashi Najafi ni maktaba kubwa ya vitabu iliyoko katika mji wa Qum, ambayo inahesabiwa kuwa ya aina yake na ina vitabu zaidi ya laki tatu.