Nov 25, 2019 02:50 UTC
  • Jumatatu tarehe 25 Novemba 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 27 Rabiul Awwal 1441 Hijria sawa na Nivemba 25 mwaka 2019.

Tarehe 27 Rabiul Awwal miaka 1078 iliyopita alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu Abul Alaa al Maarry katika mji wa Maarrat al-Nu'man nchini Syria. Abul Alaa alifariki dunia mwaka 449 Hijria katika mji huo huo ulioko umbali wa kilomita 33 kusini mwa Halab (Aleppo). Baadaye alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."

Abul Alaa al Maarry

Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita sawa na Novemba 25 mwaka 1880, kijidudu maradhi kinachosababisha maradhi ya Malaria kiligunduliwa na  Charles Luis Alphonse Laveran, tabibu mashuhuri wa Kifaransa. Ugunduzi huo wa kijidudu maradhi cha malaria ulitayarisha uwanja mzuri wa kukabiliana na kuangamiza maradhi hayo. Mnamo mwaka 1907 Dakta Alphonse Laveran alitunukiwa Tuzo ya Nobeli kutokana na utafiti wake katika masuala ya tiba.

Charles Luis Alphonse Laveran

Miaka 69 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 4 Azar mwaka 1329 Hijiria Shamsia, Tume ya Mafuta ya Bunge la Taifa la Iran, ilipinga mkataba ziada wa mafuta kati ya Iran na Uingereza. Mkataba huo ulikuwa na lengo la kuimarisha nafasi ya Uingereza na kuzidisha uwezo wa nchi hiyo kuchimba mafuta huko kusini mwa Iran. Vilevile mkataba huo uliotayarishwa katika kilele cha ushindani wa Marekani na Uingereza wa kupora utajiri wa mafuta wa Iran, ulitambuliwa kuwa ni tishio kwa maslahi ya taifa.

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko alitwaa madaraka ya nchi kupitia mapinduzi ya uwagaji damu. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo aliyeitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jesi la ukatili na mauaji.

Jenerali Mobutu Sese Seko

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 Muhammad Hadi Farzaneh, maarufu kwa jina la Hakim Farzaneh, mtaalamu mkubwa wa elimu ya theolojia na falsafa. Hakim Farzaneh alizaliwa mwaka 1302 Hijiria katika moja ya maeneo ya mji wa Isfahan. Alisoma elimu ya msingi eneo alikozaliwa na kisha kuelekea mjini Isfahan kwa ajili ya kuendelea na masomo yake ambapo alipata kusomea elimu mbalimbali muhimu hususan theolojia na falsafa. Aliweza kuinukia kielimu na kuwa msomi mkubwa kiasi kwamba mwishoni mwa umri wake alikuwa miongoni mwa wataalamu wa taaluma hizo. Baadaye alirejea katika mji alikozaliwa na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji hadi alipofariki dunia.

Hakim Farzaneh

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita Ustadh Jabbar Baghcheban alifariki dunia baada ya miaka mingi ya kutoa huduma kubwa kwa viziwi hapa nchini. Ustadh Baghcheban alizaliwa mwaka 1261 Hijria Shamsia na mwaka 1303 aliasisi shule ya kwanza ya watoto katika mji wa Tabriz magharibi mwa Iran. Shule hiyo ilianza kutoa mafunzo kwa watoto watatu viziwi. Ustadh Jabbar Baghcheban alivumbua mbinu mpya na ya kisasa ya kutoa mafunzo ya kusoma na kuandika kwa watoto viziwi ambayo ingali inatumika hadi hii leo hapa nchini.

Ustadh Jabbar Baghcheban

Siku kama ya leo Miaka 51 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92. Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel. Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim

Na miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Suriname ambayo kijiografia ipo katika Amerika ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa Uholanzi. Mwanzoni mwa karne ya 16 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Uingereza. Mwaka 1954 Suriname ilijipatia utawala wa ndani na miaka 21 baadaye ikajipatia uhuru kamili. Nchi hiyo inapakana na Brazil na Guyana na iko katika pwani ya Bahari ya Atlantic. 

Bendera ya Suriname

 

Tags