Jumatano tarehe 18 Disemba 2019
Leo ni Jumatano tarehe 21 Rabiuthani 1441 Hijria sawa na Disemba 18 mwaka 2019.
Miaka 105 iliyopita katika siku kama ya leo, Uingereza iliikoloni rasmi Misri. Inafaa kukumbusha kwamba, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Othmania ulikuwa mwitifaki wa madola yaliyokuwa yakiipinga Uingereza yaani Ujerumani na Austria. Uingereza nayo ikiwa na lengo la kukabiliana na kitendo hicho, iliikalia kwa mabavu Misri, ambayo hadi katika kipindi hicho ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Othmania. Harakati za ukombozi za wananchi wa Misri dhidi ya mkoloni Mwingereza zilizaa matunda mwaka 1922, ambapo nchi hiyo ilijitangazia uhuru wake.
Bendera ya Misri
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita msomi wa Ujerumani, Otto Hahn, alifanikiwa kupasua kiini cha atomu, hatua ambayo ilikuwa mwanzo wa zama za atomu. Mtaalamu huyo wa kemia alizaliwa mwaka 1879 huko Frankfurt na kupata shahada ya uzamivu katika taaluma ya kemia. Tangu wakati huo alijishughulisha na utafiti katika taaluma ya fizikia. Baada ya utafiti mkubwa na katika siku kama hii ya leo Otto Hahn alifanikiwa kupasua kiini cha atomu. Hatua hiyo iliibua nishati kubwa ambayo baadaye ilianza kutumika katika vinu na mabomu ya nyuklia. Mwaka 1944 Otto Hahn alitunikiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya kemia.
Otto Hahn
Tarehe 18 Disemba miaka 40 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha makubaliano ya kufuta aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake. Makubaliano hayo yana lengo la kuondoa dhulma zinazofanywa dhidi ya wanawake duniani. Hata hivyo makubaliano hayo, kama yalivyo mengine mengi ya kimataifa, yanatawaliwa na mitazamo ya kimaada ya Magharibi inayosisitiza usawa wa jinsia mbili za mwanamke na mwanaume katika kila kitu. Hii ni katika hali ambayo mwanamke na mwanaume wanatofautiana kimwili na kiroho. Kwa sababu hiyo dini za Mwenyezi Mungu hususan Uislamu zinasisitiza kuwa njia ya kuwakomboa wanawake ni kuwatayarishia mazingira ya uadilifu kwa kutilia maanani uwezo wao wa kimwili na kiroho.
Na siku kama ya leo miaka 40 iliyopita Dakta Muhammad Mufatteh alimu, mwanaharakati na mwanamapambano wa Kiirani aliuawa shahidi na makundi ya kigaidi. Baada ya kumaliza masomo yake ya kimsingi alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum. Sambamba na kusoma masomo ya dini, Muhammad Mufatteh alikuwa akisoma pia katika Chuo Kikuu cha Tehran na kufanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika falsafa yaani PHD. Baada ya kupata shahada hiyo akaanza kufundisha kama mhadhiri huku akiendesha harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini Iran.
Muhammad Mufatteh