Dec 22, 2019 01:12 UTC
  • Jumapili, Disemba 22, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 25 Mfungo Saba Rabiuth-Thani 1441 Hijria, sawa na tarehe 22 Disemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 2165 iliyopita, duru ya tatu na ya mwisho ya vita vya kihistoria na vya umwagaji damu kati ya tawala za kifalme za Carthage na Roma ilimalizika kwa kupata ushindi Waroma na kuanguka utawala wa Wacartharge. Vita vya falme hizo mbili vilijulikana kwa jina mashuhuri la vita vya Punic. Utawala wa kifalme wa Carthage ulikuwa moja kati ya tamaduni kongwe huko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya bahari ya Mediterrania.

Wakati wa vita hivyo vya kihistoria

Siku kama ya leo miaka 1153 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya riwaya za kihistoria, yaani sawa na tarehe 25 Rabiuth-Thani 288 Hijria, alifariki dunia Thabit Ibn Qurrah Swaabi, mtaalamu wa hisabati, mnajimu na tabibu mashuhuri wa kipindi cha utawala wa Bani Abbas. Ibn Qurrah alizaliwa mwaka 221 Hijiria mjini Harran (Mesopotamia) nchini Iraq ya leo. Alijifunza lugha za Kigiriki, Kisyriac na Kiarabu ambapo alikuwa na uwezo mkubwa wa kuzifahamu lugha hizo. Aidha alielekea mjini Baghdad, Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu ambapo akiwa hapo alitokea kuwa shakhsia mwenye nadharia katika uwanja wa hisabati na elimu ya nyota kupitia maelekezo ya Muhammad Bin Musa, ambaye naye alikuwa mtaalamu wa hisabati mashuhuri wa Waislamu zama hizo. Thabit Ibn Qurrah Swaabi ameacha athari nyingi katika nyuga za tiba, hisabati na elimu ya nyota kwa lugha za Kigiriki. Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Adh-Dhakhiratu fii ilmi al-Twib' na 'Kitabul Mafruudhaat.'

Thabit Ibn Qurrah Swaabi, mtaalamu wa hisabati, mnajimu na tabibu

Siku kama ya leo miaka 380 iliyopita alizaliwa Jean Racine malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kifaransa. Racine alianza kazi ya uandishi katika uwanja huo baada ya kusoma kwa muda fulani na kuhitimu umri wa miaka 18. Hata hivyo muda fulani baadaye alianza kukosoa kazi hiyo baada ya kuandika mchezo wa tanzia alioupa jina la Andromaque na kupata umashuhuri. Alianza kuakisi matukio ya mfalme wa wakati huo wa Ufaransa. Jean Racine alifariki dunia mwaka 1699 Miladia.

Jean Racine

Siku kama ya leo miaka 326 iliyopita, ulitokea mtetemeko mkubwa wa ardhi katika kisiwa cha Sicily kusini mwa Italia. Kufuatia zilzala hiyo, miji mitatu mikubwa ya kisiwa hicho ilibomolewa na kusababisha hasara kubwa kwa miji mingine yakiwemo makao makuu ya kisiwa hicho yaani Palermo. Mtetemeko huo wa ardhi unahesabiwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Italia. Zaidi ya watu 80,000 walipoteza maisha yao katika janga hilo la kimaumbile.

Tetemeko hilo

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, Ufaransa na Uingereza zilihitimisha udhibiti wao wa siku 50 wa bandari ya Port Said nchini Misri na kutoa majeshi yao katika bandari hiyo. Inafaa kuashiria hapa kwamba, baada ya utawala haramu wa Israel kufanya mashambulio katika jangwa la Sinai, mashambulio ya pamoja ya anga ya Uingereza na Ufaransa dhidi ya Misri nayo yalianza. Mashambulio hayo, yalisababisha hasara kubwa katika Kanali ya Suez. Sababu ya kufanywa mashambulio hayo ambayo baadaye yalikuja kujulikana kama Vita vya Kanali ya Suel, ni hatua ya Rais Gamal Abdul-Nassir wa Misri kutangaza kutaifisha kanali hiyo. Umoja wa Mataifa uliiunga mkono Misri wakati wa mashambulio hayo na kwa utaratibu huo tawala tatu hizo, yaani Uingereza, Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel zikaondoa majeshi yao katika ardhi ya nchi hiyo.

Bandari ya Port Said nchini Misri

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita yaani tarehe 22 Disemba mwaka 1989 Miladia, uongozi wa Nicolae Ceausescu, Rais na Mkuu wa chama cha Kikomonisti cha Romania uliangushwa na siku tatu baadaye kiongozi huyo pamoja na mkewe wakanyongwa. Mke wa Ceausescu alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri wa serikali ya Romania. Rais huyo wa zamani wa Romania ya kidikteta aliasisi chama hicho cha Kikomonisti kama walivyofanya watawala wengine wa nchi za Kisoshalisti za Ulaya.

Nicolae Ceausescu

 

Tags