Jan 11, 2020 04:51 UTC
  • Jumamosi, 11 Januari, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 15 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 11 Januari 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1403 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema, ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya. ***

 

Tarehe 15 Jamadil Awwal mwaka 38 Hijria yaani miaka 1403 iliyopita aliuawa shahidi Muhammad bin Abu Bakr ambaye alikuwa miongoni mwa maswahaba waaminifu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kamanda maarufu wa jeshi la Uislamu katika vita dhidi ya jeshi la Muawiya lililokuwa likiongozwa na Amr bin al-As. Mtawala wa kizazi cha Bani Umayyah, Muawiya alituma jeshi la wapiganaji elfu sita nchini Misri kwa ajili ya kupigana na jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lililokuwa na wapiganaji elfu mbili. Jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lilishindwa katika vita hivyo na kiongozi huyo akauawa shahidi kwa kuchomwa moto baada ya kukamatwa mateka. ***

Muhammad bin Abu Bakr

 

Miaka 695 iliyopita katika siku kama ya leo, mji wa Mexico ambao hivi sasa ni mji mkuu wa nchi ya Mexico, uliasisiwa na mmoja wa wafalme wa silsila ya Aztec. Waaztec walikuwa miongoni mwa makabila ya Wahindi Wekundu wa Amerika ya Latini ambao waliwasili huko Mexico katika karne ya 12 na kutawala eneo hilo mwanzoni mwa karne hiyo. ***

Muonekano mpya wa mji wa Mexico

 

Katika siku kama ya leo miaka 211 iliyopita, Mirza Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mamar'ja' mashuhuri wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kuendeleza masomo yake ya kidini na kupata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo kama Sheikh Murtadha Ansari. Bidii yake kwenye masomo ilimuwezesha kukwea haraka daraja za elimu na kuwa mhadhiri na mwanazuoni wa ngazi za juu mjini hapo na katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatua yake ya kuharamisha tumbaku katika kipindi cha utawala wa Nassir Deen Shah kutoka ukoo wa Qajaar. Fatuwa yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Fatuwa hiyo ilichukuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran. Kwa hakika iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni nchini. ***

Mirza Muhammad Hassan Shirazi

 

Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita, toleo la kwanza la gazeti la al Uruwatul Wuthqaa lilichapishwa chini ya uongozi wa Sayyid Jamaluddin Asadabadi maarufu kwa jina la Jamaluddin Afghani na Sheikh Muhammad Abduh mjini Paris, Ufaransa. Sayyid Jamaluddin aliasisi Jumuiya ya al Uruwatul Wuthqaa kwa shabaha ya kutimiza lengo lake la kujenga umoja na mshikamano kati ya mataifa ya Kiislamu na akaanza kuchapisha gazeti kwa kutumia jina hilo hilo.***

Sayyid Jamaluddin Asadabadi

 

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, aliaga dunia Ustadh Abulqassim Sahab, mmoja wa wasomi wakubwa wa elimu ya jiografia na mtafiti mashuhuri wa Kiirani. Alizaliwa mwaka 1266 Hijria Shamsiya katika mji wa Tafresh nchini Iran. Abulqassim Sahab alijifunza fiqih na usul kwa maulamaa wa mji huo na mbali na kupata elimu hiyo alizungumza pia lugha za Kiingereza na Kijerumani. ***

Ustadh Abulqassim Sahab,

 

Miaka 28 iliyopita sawa na tarehe 11 Januari mwaka 1992, Rais Shazli bin Jadid wa Algeria alijiuzulu baada ya Harakati ya Uokovu wa Kiislamu ya Algeria (FIS) kupata mafanikio makubwa katika uga wa kisiasa na matukio ya baadaye nchini humo. Rais Shazli alichaguliwa kuwa rais wa Algeria mwaka 1979 baada ya kifo cha Houari Boumediene, rais wa zamani wa nchi hiyo. Mwaka 1988 Shazli bin Jadid aliahidi kutekeleza marekebisho na kufanya mabadiliko ya katiba ya Algeria, ambapo kwa mujibu wake suala hilo lingetoa mwanya wa kutambuliwa rasmi vyama vya kisiasa. ***

Shazli bin Jadid

 

Na siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, Mustafa Ahmadi Roshan aliuawa shahidi na maajenti wa utawala haramu wa Israel. Ahmadi Roshan alikuwa msomi wa nne wa nyuklia wa Iran kuuawa na magaidi wa Israel na washirika wake. Mbali na kujishughulisha na masuala ya nyuklia, msomi huyo alifanya utafiti mkubwa katika masuala ya elimu na sayansi. Ahmadi Roshan aliuawa yeye na dereva wake mjini Tehran akiwa njiani kueleka kazini kwake. Siku kadhaa baadaye genge la magaidi waliomuua msomi huyo wa nyuklia wa Iran na wenzake lilitiwa nguvuni; na wanachama wake wakakiri kuwa wana uhusiano na utawala haramu wa Israel na kwamba walipewa mafunzo na maajenti wa utawala huo haramu kwa ajili ya kuwaua kigaidi wasomi wa nyuklia wa Iran. ***

Mustafa Ahmadi Roshan