Jumapili tarehe 8 Machi 2020
Leo ni Jumapili tarehe 13 Rajab, 1441 Hijiria sawa na tarehe 8 Machi 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1464 iliyopita yaani sawa na tarehe 13 Rajab mwaka wa 23 kabla ya Hijra, kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa katika nyumba tukufu ya al Kaaba, Ali bin Abi Twalib (as), ambaye ni binamu, mkwe na Khalifa wa Mtume Muhammad (saw). Mama wa mtukufu huyo ni Bibi Fatima bint Assad na baba yake ni Abu Talib. Katika kipindi chake cha utotoni, Ali bin Abi Talib alilelewa na kupata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw), na alikuwa mwanaume wa kwanza kuukubali Uislamu. Mwishoni mwa mwaka wa Pili Hijria, Imam Ali (as) alimuoa Bibi Fatimatul Zahra binti ya Mtume Mtukufu (saw). Imam Ali (as) alishiriki kwenye vita vyote bega kwa bega na Mtume Mtukufu (saw) isipokuwa vita vya Tabuk, na alikuwa msaidizi mkubwa wa Mtume katika hali tofauti za shida na matatizo. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji asiye na mithili, lakini Imam Ali bin Abi Talib (as) alikuwa mpole, mwingi wa huruma na mtetezi wa wanyonge. Sambamba na kutoa mkono wa kheri na fanaka kwa mnasaba wa kuzaliwa mtukufu huyo, tunakunukulieni sehemu fupi ya usia wake inayosema: “Ishini na watu kiasi kwamba mkifa watakuhuzunikieni na ikiwa mtakuwa hai watakufanyieni wema.”
Siku kama ya leo miaka 1162 iliyopita yaani sawa na tarehe 13 Rajab mwaka 279 Hijria, alifariki dunia Abu Isa Tirmidhi hafidh wa Qur'ani Tukufu na mpokeaji hadithi mashuhuri wa Kiislamu. Tirmidhi alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa miaka mingi kwa ajili ya kujipatia elimu ya dini na hadithi. Alikuwa miongoni mwa wanafunnzi hodari wa Imam Bukharin na kitabu chake maarufu zaidi ni Swahih Tirmidhi. Kitabu hicho kinahesabiwa kuwa miongoni mwa marejeo muhimu ya hadithi katika madhehebu ya Suni. Aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 70.
Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita sawa na tarehe 18 Esfand mwaka 1275 Hijiria Shamsia aliuawa Sayyid Jamalud-Din Asadabadi, msomi wa kidini, mwananadharia na mmoja wa viongozi wanamapambano wa Kiislamu dhidi ya ukoloni. Alizaliwa katika kijiji cha Asadabadi, Hamadan magharibi mwa Iran na katika kipindi cha masomo yake alibobea katika elimu kama vile falsafa, nyota na historia. Mbali na kufahamu lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kiturki, alizungumza pia lugha za Kingereza, Kifaransa na Kirusi. Sayyid Jamalud-Din Asadabad ni kati ya waasisi wa fikra ya umoja wa Kiislamu na mmoja wa wapinzani wakubwa wa upenyaji wa ukoloni ndani ya nchi za Kiislamu. Mwanafikra huyo na mrekebishaji mkubwa wa Uislamu alianza kufanya safari katika nchi nyingi za Waislamu akiwa na umri wa miaka 18 ambapo alifanya juhudi kubwa za kuwaunganisha. Kupitia kuchapisha gazeti la ‘Urwatul-Wuthqa’ mjini Paris, Ufaransa na ‘Dhiyaaul-Khaafiqin’ mjini London, Uingereza, alijaribu kuyaamsha mataifa ya Waislamu. Mbali na hayo alitoa hotuba za hamasa zenye fikra za kupigania uhuru kati ya watu na ni kwa ajili hiyo ndio maana akachukiwa na wakoloni na tawala za kidikteta. Baada ya kufuatiliwa na maadui huko Ulaya, Sayyid Jamalud-Din Asadabadi aliamua kuelekea Istanbul, mji mkuu wa utawala wa Othmania wakati huo. Hata hivyo Abdul Hamid, Mfalme wa utawala wa Othmania wa wakati huo alimuua shahidi kwa kumpa sumu.
Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, inayosadifiana na 8 Machi 1968 ilianza Harakati ya Ukombozi ya Moro dhidi ya utawala wa dikteta Ferdinand Marcos nchini Ufilipino. Dikteta Marcos alikuwa mshirika na muitifaki mkubwa wa Marekani na katika utawala wake wa kidikteta, maelfu ya Waislamu wa Ufilipino waliuawa au kufungwa jela. Harakati ya Ukombozi ya Moro ilipambana kwa ajili ya kupigania haki za Waislamu, na ilihesabiwa kuwa harakati kubwa zaidi iliyopinga utawala wa Marcos nchini Ufilipino. Baada ya Marcos kuondoka madarakani mwaka 1986, harakati ya Moro ilikubali kutia saini makubaliano ya amani na serikali ya Manila.
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Machi 1985, ulitokea mlipuko mkubwa wa bomu la kutegwa garini mjini Beirut, Lebanon ambapo watu wasiopungua 45 waliuawa na wengine 175 kujeruhiwa. Mlipuko huo ulitokea karibu na msikiti unaotumiwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mlipuko huo ulifuatia mlipuko mwingine mkubwa zaidi uliotokea mwaka 1983, ambapo watu wasiopungua 61 waliuawa kusini mwa bandari ya Tyre, nchini Lebanon.
Na leo tarehe 8 Machi inatambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Mwanamke. Awali siku hii ilianzishwa kama tukio la kisiasa la kisoshalisti lakini baadaye liliingia katika utamaduni wa nchi nyingi duniani. Siku ya Kimataifa ya Mwanamke inayoadhimishwa katika nchi nyingi duniani imepoteza sura yake ya kisiasa na sasa limekuwa tukio linalotumiwa na wanaume kudhihirisha upendo wao kwa wanawake. Mwaka 1977 Umoja wa Mataifa iliitangaza rasmi siku hiyo kama Siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa.