Dec 03, 2025 04:40 UTC
  • Jumatano, 03 Disemba, 2025

Leo ni Jumatano tarehe 12 Mfunguo Tisa Jamadithani 1447 Hijria mwafaka na tarehe 3 Disemba, 2025.

Siku kama ya leo miaka 804 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia Abul Hassan Ali bin Abdu Samad Hamdani, mtambuzi wa lugha, fakihi na mfasiri wa Qur'ani katika karne ya 7 Hijria. 

Alizaliwa huko Sakha nchini Misri na akaondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu ya Sakhawi. Akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu, Abul Hassan Ali bin Abdu Samad alielekea Sham na kuishi Damascus katika Syria ya leo. 

Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu mbalimbali katika elimu za Tajweed, teolojia na Hadithi. Baadhi tu ya vitabu vyake mashuhuri ni al Jawahir na Sifrus Sa'ada. 

Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, alizaliwa Dakta Rajendra Prasad, mwanasiasa na mwanafilosofia wa India huko katika mojawapo ya vijiji vya jimbo la Bihar.

Rajendra Prasad aliweza kuendelea na masomo na kufikia daraja ya udaktari, licha ya hali duni ya kifedha ya familia yake. Alishirikiana na wananchi wa India katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yao.

Prasad vilevile alikuwa bega kwa bega na Mahatma Gandhi katika mapambano ya kisiasa dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na kwa mara kadhaa aliteuliwa kuongoza chama cha Congress ya Kitaifa ya India.

Rajendra Prasad aliteuliwa kuwa Rais wa kwanza wa India baada ya uhuru na kuasisiwa mfumo wa jamhuri nchini humo mwaka 1950.

Rajendra Prasad

Katika siku kama ya leo miaka 46 iliyopita katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipasishwa kwa wingi wa kura za wananchi.

Katiba hiyo inasisitiza juu ya kuzingatiwa thamani za Kiislamu, uadilifu wa kijamii na kuheshimiwa haki za binadamu. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, katika mwaka 1368 Hijria Shamsia, kipengee cha ziada kiliongezwa kwenye katiba hiyo, baada ya kupasishwa na Baraza la Wataalamu linalomteuwa Kiongozi Mkuu wa Iran na kuidhinishwa pia na wananchi.

Kwa mujibu wa kipengee hicho cha nyongeza, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ina vipengee 14 na vifungu 177. 

Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 3 mwezi Disemba mwaka 1984, kulitokea janga kubwa la kuvuja gesi ya kemikali katika kiwanda kimoja cha Marekani katika mji wa Bhopal huko katikati mwa India.

Kiwanda hicho kilikuwa kikimilikiwa na kampuni ya Kimarekani iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Union Carbide. Uzembe wa maafisa wa kiwanda hicho na kutozingatiwa viwango vya usalama kulipelekea kuvuja kwa gesi ya sumu ya sianidi (cyanide) kutoka katika kiwanda hicho na kuenea katika hewa.

Wakazi wasio na hatia wa mji wa Bhopal wasiopungua 2500 walipoteza maisha yao na mamia ya wengine pia kujeruhiwa katika janga hilo. 

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, kombora la kwanza la balestiki lililotengenezwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilifanyiwa majaribio kwa mafanikio wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika kipindi hicho ambapo Iran ilikuwa chini ya vikwazo vikali vya nchi za Magharibi huku ikipigana na adui kulinda ardhi yake, awamu ya kwanza ya majaribio ya kombora hilo ilifanyika kwa mafanikio na uzalishaji wake ukaanza wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.   

Na tarehe 3 Disemba imetangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa ni siku ya Kimataifa ya Walemavu.

Lengo la hatua hiyo ni kuboresha nafasi ya watu wenye ulemavu katika jamii za kibinadamu

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu nusu bilioni duniani ni walemavu. Vilevile watu wenye ulemavu ni moja ya kumi ya wakazi wa nchi nyingi duniani. 

Inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya walemavu wanaishi katika nchi zinazoendelea, kwa sababu ulemavu mwingi unasababishwa na utapiamlo, umaskini, ukosefu wa huduma za afya na elimu na mambo mengine ambayo ni matokeo ya kubakia nyuma kimaendeleo.