May 27, 2020 03:58 UTC
  • Jumatano, tarehe 27 Mei, 2020

Leo ni Jumatano tarehe 4 Shawwal 1441 Hijiria sawa na tarehe 27 Mei 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1090 iliyopita, sawa na tarehe 4 Shawwal mwaka 351 Hijiria, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Dar Ghotni mmoja wa maulamaa na wataalamu wa lugha wa karne ya Nne Hijria. Dar Ghotni alikuwa mmoja wa maqari na wafasiri watajika wa Qu'rani Tukufu katika zama zake hizo, ambaye alitumia umri wake mwingi kuandika vitabu vya kielimu.

Muhammad bin Hassan Dar Ghotni

Siku kama ya leo miaka 537 iliyopita sawa na tarehe 27 Mei mwaka 1482 Miladia, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82, Luca della Robbia, msanii mkubwa wa uhunzi wa Italia. Akiwa kijana alijifundisha kazi ya ufuaji dhahabu, hata hivyo aliachana na kazi hiyo baadaye na kujihusisha na uhunzi wa sanamu. Katika kipindi hicho alipata kuunda masanamu na athari mbalimbali za kale. Athari kadhaa za Luca della Robbia zipo katika majengo tofauti ya maonyesho ya kale duniani.

Luca della Robbia

Siku kama ya leo miaka 183 iliyopita sawa na tarehe 27 Mei 1837, ulitiwa saini mkataba wa amani kati ya Ufaransa na Amir Abdulqadir wa Algeria kiongozi wa wapigania uhuru wa nchi hiyo. Tangu mwaka 1832 baada ya mashambulizi ya jeshi la Ufaransa nchini Algeria Amir Abdulqadir aliendesha mapambano dhidi ya wavamizi huko Algeria na kusimama kidete dhidi yao kwa miaka kadhaa na kujulikana kama kiongozi wa wanamapambano wa Algeria dhidi ya Ufaransa. Baada ya kufikiwa makubaliano hayo maeneo mengi ya Algeria yaliyokuwa chini ya Ufaransa yalipewa uhuru. Hata hivyo kutokana na ukwamishaji mambo wa mkoloni Mfaransa, tarehe 18 Novemba mwaka 1839 Miladia Amir Abdulqadir alianzisha mapambano ya pili ya kupigania uhuru na akiwa na askari elfu 50 wapanda farasi na watembeao kwa miguu aliwashambulia askari wa Kifaransa. Hatimaye Amir Abdulqadir alishindwa vita na kulazimika kusalimu amri na kufungwa jela. Mwanamapambano huyo aliachiliwa huru kutoka jela mwaka 1853 Miladia na kufariki dunia mjini Damascus tarehe 29 Agosti mwaka 1883 akiwa na umri wa miaka 75.

Amir Abdulqadir

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, sawa na tarehe 27 Mei 1910 Milaia alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 67 Robert Koch, mgunduzi wa vijidudumaradhi aina ya bakteria na tabibu mashuhuri wa Kijerumani aliyegundua chanzo cha maradhi ya kifua kikuu au TB. Daktari Robert Koch alianza kutwalii na kufanya utafiti mkubwa juu ya sababu au vyanzo vya kutokea baadhi ya magonjwa kama vile kipindupindu, kimeta na kifua kifuu, baada ya kuhitimu masomo yake katika taaluma ya tiba. Mwaka 1882 Miladia, Robert Koch alifanikiwa kugundua vijidudumaradhi vinavyoitwa mycobacterium tuberculosis vinavyosababisha kifua kikuu. Ili kukamilisha uchunguzi wake tabibu huyo Mjerumani alisafiri katika nchi za Afrika Kusini, Misri na India na kutwalii magonjwa mengineyo maarufu katika maeneo hayo kama vile Malaria. Mwaka 1905 Robert Koch alitunukiwa Tunzo ya Nobel katika uwanja wa Tiba. 

 

Tags