Jul 05, 2020 06:05 UTC
  • Jumapili, 5 Julai, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 13 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1441 Hijria ambayo inalingana na tarehe 5 Julai 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 675 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Qutub Deen bin Muhammad bin Muhammad Razi. Alizaliwa huko Varamin katika moja ya viunga vya mji wa Rey na kwa kuwa alikulia huko aliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Razi. Qutub Deen alikuwa mmoja wa wanafunzi wakubwa wa Allamah Hilli. Alimu huyo alikuwa mwanazuoni mashuhuri na aliyekuwa na nafasi kubwa katika kueneza mafundisho ya Kiislamu. ***

Qutub Deen bin Muhammad Razi

 

Katika siku kama ya leo miaka 209 iliyopita, nchi ya Venezuela ilijitangazia uhuru wake na kwa ajili hiyo, tarehe 5 Julai, hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Tangu mwanzoni mwa karne ya 16 Miladia, na kwa kipindi cha karne tatu Venezuela ilikuwa chini ya ukoloni wa Uhispania. Katika kipindi cha ukoloni huo, raia wa nchi hiyo walipatwa na matatizo mengi, kiasi kwamba makumi ya maelfu ya Wahindi Wekundu ambao ni raia asili wa taifa hilo waliuawa na mahala pao kuchukuliwa na Wahispania. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, mapambano ya wananchi yalianza chini ya uongozi wa Francisco Miranda na kuzaa matunda katika siku kama ya leo mwaka 1811. ***

Bendera ya Venezuela

 

Miaka 187 iliyopita,  alifariki dunia Joseph Nicéphore Niépce, mvumbuzi wa kamera wa nchini Ufaransa. Niépce alifanikiwa kusajili kwa mara ya kwanza uvumbuzi huo mnamo mwaka 1826 baada ya kufanya majaribio kadhaa ya kielimu katika uwanja huo. Uvumbuzi wake ulikuwana nafasi muhimu katika uga wa kamera na upigaji picha.***

Joseph Nicéphore Niépce,

 

Katika siku kama ya leo miaka 58 iliyopita,  wananchi wa Algeria walipata uhuru wao dhidi ya wavamizi wa Ufaransa, kufuatia kujiri mapambano makali na ya muda mrefu na wavamizi hao. Ufaransa iliikalia kwa mabavu Algeria kwa kutegemea jeshi lake kubwa mnamo mwaka 1830. Kwa kipindi cha miaka 130 ya kukoloniwa taifa hilo, raia wa Algeria waliasisi harakati kadhaa za kupigania uhuru zilizokuwa zikiongozwa na Amir Abdulqadir al Jazairi, ambazo hata hivyo zilikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa jeshi la Ufaransa. Hata hivyo harakati hizo zilishika kasi zaidi na kuzaa matunda baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia na kujipatia uhuru wake katika siku kama ya leo. ***

Algeria

 

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, Jenerali Muhammad Zia-ul-Haq alifanya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya Zulfiqar Ali Bhutto huko nchini Pakistan. Muhammad Zia-ul-Haq alitwaa madaraka yote ya waziri mkuu na rais wa Jamhuri ya Pakistan na mbali na kuwanyonga Zulfiqar Bhutto na wapinzani wake wengine, alivunja mabunge ya nchi hiyo na kusimamisha shughuli zote za vyama vya siasa nchini Pakistan. Zia-ul-Haq aliuawa katika ajali ya ndege akiwa na maafisa kadhaa wa jeshi la Pakistan, na utawala wake ukakomea hapo. ***

Jenerali Muhammad Zia-ul-Haq

 

Na miaka 34 iliyopita, aliaga dunia Sayyid Javad Khamenei, baba wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Alizaliwa katika mji wa Khamenei karibu na Tabriz huko Azerbaijan Mashariki na akaondokea kuwa alimu na fakihi kupitia malezi ya baba yake. Akiwa katika rika la ujana, Sayyid Javad Khamenei alifanya safari katika maeneo matakatifu na akauchagua mji mtakatifu wa Mash’had kuwa makazi yake ya kudumu. Akiwa mjini Mash’had alisoma masomo ya Hawza kwa Ayatullah Aghazadeh Khorasani na al Haj Hussein Qumi na kukwea daraja za kielimu. Aidha akiwa na nia ya kujiendeza zaidi kielimu alifanya safari huko Najaf Iraq na kufanikiwa kusoma kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah Mirza Naini na Abul-Hassan Isfahani. Hatimaye Sayyid Javad Khamenei aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 91 na kuzikwa jirani na haram ya Imam Ridha AS mjini Mash'had. ***

Sayyid Javad Khamenei