Jumatatu tarehe 17 Agosti mwaka 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 27 Dhulhija 1441 Hijria sawa na Agosti 17 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 750 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Muslihuddeen Saadi Shirazi malenga, mshairi na mwalimu stadi wa tungo za mashairi na nathari wa Kifarsi. Baada ya kukipitisha kipindi cha utoto na kuinukia kwake katika mji alikozaliwa wa Shiraz nchini Iran, akiwa kijana Saadi Shirazi aliamua kwenda katika mji wa Baghdad huko Iraq. Akiwa huko alisoma katika shule ya Nidhamiya na baadaye kufanya safari katika maeneo ya Sham, Hijaz, Roma na katika maeneo mengine. Katika safari zake hizo, malenga huyo mashuhuri alifanikiwa kufahamiana na jamii mbalimbali na kuona mengi yaliyoimarisha kipawa chake cha kutunga mashairi. Saadi Shirazi ni miongoni mwa malenga na washairi wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Saadi Shirazi ameandika vitabu kadhaa, muhimu zaidi ni kile cha tungo cha Bustan na kitabu chake cha nathari cha Golestan.
Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, alifariki dunia Muhammad Ghaffari aliyekuwa na lakabu ya Kamal al-Mulk mchoraji mahiri wa Kiirani. Alisoma katika skuli ya Darul Funun ya Tehran na kupata mafanikio makubwa katika fani ya uchoraji aliyokuwa akiipenda. Kipindi fulani Muhammad Ghaffar alifanya kazi katika utawala wa Nasser Deen Shah Qajar na kufanikiwa kutoa athari zenye thamani kubwa za uchoraji.
Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, wananchi wa Indonesia walianzisha mapambano ya kujikomboa kutoka katika makucha ya mkoloni Mholanzi. Mapambano hayo yaliyoongozwa na Ahmad Sukarno yaliendelea kwa miaka minne huko Indonesia. Baada ya kushadidi mapambano hayo ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Indonesia, Umoja wa Mataifa uliiamuru serikali ya Uholanzi kuuasisi utawala kwa jina la " Umoja wa Indonesia na Uholanzi". Jamhuri ya Indonesia ilivunja umoja huo mwaka 1956 na kutangaza uhuru wa nchi hiyo na Sukarno akawa Rais wa kwanza wa taifa hilo.
Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Gabon iliyoko magharibi mwa Afrika na katika pwani ya bahari ya Atlantiki, ilipata uhuru wake. Wareno walifika huko Gabon kwa mara ya kwanza mwishoni mwa karne ya 15 Miladia. Hata hivyo nafasi ya kijiografia ya Gabon ilizuia kugunduliwa nchi hiyo hadi karne ya 19. Katikati ya karne ya 19 Wafaransa waliwasili Gabon na kuidhinishwa kuitawala nchi hiyo katika mkutano uliofanyika huko Berlin Ujerumani. Hatimaye mwaka 1960 Gabon ilipata uhuru. Kijiografia nchi ya Gabon inapakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kongo, Cameroon na Equatorial Guinea.
Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, Rudolf Hess makamu wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolf Hitler alijiua akiwa jela nchini Uingereza. Hess ambaye alizaliwa mwaka 1894, alikuwa mmoja wa waasisi wa chama cha Kinazi na miongoni mwa viongozi wakuu wa serikali ya Hitler. Rudolf Hess alihukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama ya jinai za kivita ya Nuremberg nchini Ujerumani baada ya nchi hiyo kushindwa katika Vita vya Pili vya Dunia. Hess alijiua akiwa jela mwaka 1987.
Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, baada ya vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran na Iraq, hatimaye Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kusimamishwa vita hivyo kwa mujibu wa moja ya vipengee vya azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la umoja huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, madola yanayopenda kujitanua ambayo yaliona maslahi yao yamo hatarini hapa nchini yalianza kutekeleza njama mbali mbali ili kuuangusha mfumo wa Kiislamu wa Iran. Saddam Hussein kibaraka wa madola ya Magharibi na hasa Marekani, wakati huo akiwa Rais wa Iraq alitumiwa na Washington na kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya taifa la Iran akitumia visingizo visivyo na msingi wowote. Mwanzoni mwa vita hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kutaka kusimamishwa vita hivyo, ingawa cha kusikitisha katika azimio hilo ni kwamba, baraza hilo halikuashiria hata kidogo uchokozi wa majeshi vamizi ya Iraq dhidi ya taifa la Iran.
Na miaka 15 iliyopita katika siku kama ya leo wanajeshi wa utawala haramu wa Israel waliondoka kikamilifu katika eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina baada ya miaka 38 ya kukalia mabavu eneo hilo na kutenda jinai. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, eneo la Ukanda wa Gaza limegeuka na kuwa nembo ya muqawama na kusimama kidete katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Wazayuni wakiwa na lengo la kushinda muqawama wa Kiislamu, wamelishambulia eneo la Gaza mara kadhaa ambapo shambulio la mwisho lilikuwa la mwaka 2014 vilivyodumu kwa muda wa siku 51.