Jumanne tarehe 10 Novemba mwaka 2020
Leo ni Jumanne tarehe 24 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hjiria sawa na Novemba 10 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 3379 lililoutambua uzayuni (Zionism) kuwa ni aina fulani ya ubaguzi wa kizazi. Azimio hilo lilitoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kufichua utambulisho halisi wa utawala huo. Azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliikasirisha sana Israel na waungaji mkono wa utawala huo wa kibaguzi hususan Marekani. Tofauti na mafundisho ya Kiyahudi, fikra za uzayuni ambazo zilianzishwa mwishoni mwa karne ya 19 zinawatambua wafuasi wa dini hiyo kuwa ni ndio kizazi bora zaidi ya wengine wote duniani. Kwa mujibu wa fikra hiyo Wazayuni wa Israel wanawatambua watu wa Palestina kuwa ni kizazi dunia na hakiri zaidi na kwa sababu hiyo wanawakandamiza, kuwaua na kuwafukuza katika makazi na anchi yao.

Tarehe 10 Novemba mwaka 1981 wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Iran, Ufaransa na Iraq zilitiliana saini mkataba wa mauzo ya silaha uliokuwa na thamani ya dola bilioni moja. Mkataba huo ulikuwa moja kati ya mikataba kadhaa ya mauzo ya silaha baina ya Ufaransa na utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq wakati wa mashambulizi ya Iraq dhidi ya Iran. Ufaransa ilikuwa bega kwa bega na utawala wa Saddam Hussein tangu mwanzoni mwa mashambulizi na uvamizi wa Iraq dhidi ya Iran na ilihesabiwa kuwa muuzaji mkubwa wa pili wa silaha kwa utawala wa dikteta Saddam Hussein baada ya Russia. Silaha hizo zilijumuisha ndege za kisasa za kivita, makombora ya aina mbalimbali, vifaru, mizinga na aina nyingine za zana za kivita. Ufaransa pia ilimsaidia Saddam Hussein katika kutengeneza silaha za kemikali. Vilevile iliupatia utawala wa Iraq mkopo wa dola bilioni 5 wakati wa vita vyake dhidi ya Iran na imekataa kulipa deni la dola bilioni moja kwa Iran.
Miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 10 Novemba 1964, Leonid Brezhnev alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha CPSU katika Urusi ya zamani na hivyo kuchukua rasmi jukumu la kukiongoza chama hicho. Brezhnev aliendelea kushikilia cheo hicho cha ukatibu mkuu hadi kifo chake mwaka 1982. Katika kipindi chake cha uongozi, Umoja wa Usovieti ulipata nguvu zaidi kijeshi lakini pia ulikumbwa na matatizo mengi ya kiuchumi. Viongozi wa kikomunisti waliokuja baada yake walisema matatizo aliyoyaacha Leonid Brezhnev ndiyo yaliyopelekea Umoja wa Usovieti kuporomoka na kuvunjika kabisa mwaka 1991.
Miaka 108 iliyopita katika siku kama ya leo, Morocco iliwekwa chini ya himaya ya wakoloni wa Ufaransa na Uhispania. Uislamu uliingia Morocco mwishoni mwa karne ya 7 na nchi hiyo ikapewa jina la Maghrib kutokana na ardhi yake kuwa upande wa magharibi mwa ardhi ya nchi za Kiislamu.
Na miaka 537 iliyopita muwafaka na leo, alizaliwa Martin Luther mpigania mageuzi ya kidini wa Kijerumani. Luther alikuwa padri wakati akiwa kijana. Mitazamo ya Martin Luther kuhusuiana na dini ya Kikristo ilitofautiana na baadhi ya mitazamo ya Papa na viongozi wa ngazi ya juu wa kanisa na kuanzia mwaka 1517, Luther alidhihirisha mapambano na upinzani wake dhidi ya dhulma na ukandamizaji wa kanisa. Martin Luther alipinga waziwazi agizo la Papa wa Kanisa Katoliki kwa kuifasiri Injili kwa lugha ya Kijerumani na akaanzisha harakati ya kiprotestant dhidi ya kanisa hilo.