Nov 22, 2020 02:43 UTC
  • Jumapili tarehe 22 Novemba 2020

Leo ni Jumapili tarehe 6 Mfunguo Saba Rabiuthani 1442 Hijria sawa na tarehe 22 Novemba 2020.

Siku kama ya leo miaka 1317 iliyopita, alifariki dunia Hisham Bin Abdul-Malik, kiongozi wa 10 katika silsila ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuwa madarakani kwa karibu kipindi cha miaka 20. Hisham aliyekuwa mtawala dikteta, alizaliwa mwaka 72 Hijria na kushika uongozi wa Waislamu mwaka 105 Hijria. Hisham alikuwa mashuhuri kwa kuwa bahili, katili na dhalimu, ambaye aliwakandamiza Waislamu wa zama zake hususan wafuasi wa Ahlulbait wa Mtume (saw). Mtawala huyo wa Bani Umayyah aliishi katika kipindi cha Imam Muhammad Baqir (as) mmoja wa wajukuu watukufu wa Nabii wa Muhammad (saw) na alimfanyia maudhi mengi mtukufu huyo na baadaye kutoa amri ya kuuawa kwake. Mbali na hapo Hisham alifanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya harakati ya Zaid bin Ali, mjukuu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). Baada ya kuuliwa Zaid, mtawala huyo dhalimu alitoa amri ya kuchomwa moto mwili wa mtukufu huyo. Licha kwamba katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah, Uislamu ulienea maeneo ya mashariki na magharibi mwa dunia, lakini kulishuhudiwa harakati kadhaa za Kiislamu za kupinga dhulma, kutokana na kushadidi dhulma na ukandamizaji wa Hisham bin Abdul-Malik, harakati ambazo zilipelekea kudhoofika kwa dola hilo la Bani Umayyah.

Siku kama ya leo miaka 626 iliyopita alifariki dunia Mir Sayyid Sharif Gorgani, mtaalamu wa fasihi wa Iran huko Shiraz. Gorgani alizaliwa mwaka 740 Hijiria karibu na mji wa Gorgani ya leo, kaskazini mwa nchi hii. Mir Sayyid Sharif Gorgani alihesabika kuwa msomi mkubwa katika zama hizo hususan katika uga wa elimu ya fasihi. Ameacha athari mbalimbali mojawapo ikiwa ni kitabu kiitwacho "Risaalatul-Kubra fil-Mantwiq" na "Sharhu Mawaaqif Qadhi Adhdud-Diin Iji."

Mahali lilipo kaburi la Sharif Gorgani

Siku kama ya leo miaka 590 iliyopita, sawa na tarehe sita Rabiuthani mwaka 852 Hijiria, alizaliwa Ebn-e Eyas, mwanahistoria mashuhuri wa nchini Misri. Ebn e-Eyas alinakili habari mbalimbali za kihistoria kwa mfumo wa nathari nyepesi, mfumo ambao ulikuwa hautumiwi na wanahistoria wengine. Mfumo huo ulikuwa na umuhimu mkubwa kwenye fani ya lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa athari muhimu ya kihistoria za Ebn-e Eyas ni pamoja na kitabu cha "Badaaiuz-Zuhuur fii Waqaaiud-Duhuur" ambacho kinaelezea historia ya Misri tangu karne za nyuma hadi kipindi chake. Aidha alifafanua maisha ya watawala wa Misri, ujenzi na uimarishwaji wake na mambo mbalimbali yaliyowahi kuikumba nchi hiyo katika karne za nyuma.

Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita, alizaliwa Bi. Mary Ann Evans maarufu kwa jina la George Eliot, mwandishi wa riwaya na simulizi wa Uingereza. Akiwa mtoto mdogo Evans alipendelea zaidi kusoma vitabu, na taratibu akaingia katika fani ya uandishi. Aidha akiwa kijana Evans alikuwa na misimamo mikali ya dini ya Kikristo, hata hivyo misimamo hiyo ilipungua baadaye. Akiwa na umri wa miaka 30, aliandika kitabu cha ‘Maisha ya Nabii Issa-as’ huku akiandika vitabu mbalimbali vya riwaya simulizi na kutokea kupata umaarufu mkubwa katika karne ya 19 Miladia.

Mary Ann Evans

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, kufuatia kujiri kwa Vita vya Pili vya Dunia, nchi ya Lebanon ilijipatia uhuru wake. Lebanon ilitoka katika udhibiti wa utawala wa Othmania mnamo mwaka 1918 Miladia na kudhibitiwa baadaye na Ufaransa. Mwaka 1923 Miladia Ufaransa iliikalia nchi hiyo kwa idhini ya Umoja wa Mataifa. Tangu wakati huo Lebanon ikaanza kushuhudia siasa za ukoloni wa Mfaransa vikiwemo vitendo vya ubaguzi na machafuko. Nchi hiyo ilijipatia uhuru wake mwaka 1943.

Bendera ya Lebanon

Katika siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, John F. Kennedy, rais wa wakati huo wa Marekani aliuawa na raia mmoja wa nchi hiyo akiwa ziarani katika mji wa Dallas huko katika jimbo la Texas. Kennedy alizaliwa mwaka 1917 na alikuwa mwakilishi wa bunge la Marekani kwa duru tatu kuanzia mwaka 1946 na duru moja alikuwa mwakilishi wa seneti ya nchi hiyo. Siku kadhaa baadaye Lee Harvey Oswald ambaye alimuua Kennedy naye pia aliuawa na mtu aliyejulikana kwa jina la Jack Ruby na polisi ya Marekani ilidai kuwa mtu huyo vilevile aliaga dunia baadaye akiwa jela kutokana na maradhi ya saratani.

John F. Kennedy

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 242 kuhusu Palestina. Miongoni mwa vipengee vya azimio hilo ni udharura wa kuondoka askari wa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi zote za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu Juni mwaka 1967 katika vita vya Waarabu na Israel, kusimamishwa operesheni za kijeshi na kutatuliwa kadhia ya wakimbizi wa Palestina kwa njia ya uadilifu. Hata hivyo kutokana na himaya ya pande zote ya Marekani na nchi za Magharibi kwa utawala ghasibu wa Israel, utawala huo haramu umekataa kutekeleza azimio hilo.

Bendera ya Palestina