Jumapili, 29 Novemba, 2020
Leo ni Jumapili tarehe 13 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1442 Hijria sawa na tarehe 29 Novemba 2020 Miladia
Siku kama ya leo miaka 1223 iliyopita yaani tarehe 13 Rabiuthani mwaka 218 Hijria aliaga dunia Ibn Hisham msomi na mwanazuoni mkubwa wa Kiarabu. Ibn Hisham alizaliwa Basra nchini Iraq na alibobea katika elimu ya fasihi na utungaji mashairi. Alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufanya uchunguzi kuhusu maisha ya Nabii Muhammad (saw). Umashuhuri mkubwa wa Ibn Hisham unatokana na kitabu chake cha al Sira al Nabawiyya ambacho ni miongoni mwa marejeo muhimu kuhusu maisha ya Mtume Muhammad (saw). ***
Miaka 77 iliyopita sawa na tarehe 29 Novemba 1943 harakati ya Ukombozi ya kupambana na ufashisti iliundwa nchini Yugoslavia chini ya uongozi wa Marshal Tito. Wapiganaji wa harakati hiyo walitoa pigo kubwa kwa wanajeshi wa Ujerumani wakati Yugoslavia ilipokuwa ikikaliwa kwa mabavu na jeshi la Ujerumani. Mwaka 1944 wapiganaji wa harakati ya kupambana na ufashisti nchini Yugoslavia waliwafukuza nchini mwao wanajeshi vamizi wa Ujerumani kwa kusaidiwa na Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani. ***
Katika siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, mwafaka na tarehe 29 Novemba 1947, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha kwa wingi dhaifu wa kura suala la kugawanywa ardhi za Palestina baina ya serikali mbili yaani ya Palestina na ya Kiyahudi. Uamuzi huo usio wa kiadilifu na usio wa kimantiki ulichukuliwa chini ya ushawishi wa serikali za Magharibi hususan Marekani na Uingereza. Siku ya leo ya Novemba 29 inafahamika kama Siku ya Kimataifa ya Kufungamana na Wananchi wa Palestina. Siku hii iliainishwa ili kuonyesha mshikamano na Wapalestina ambao wametendewa dhulma ya kihistoria na madola ya Magharibi yanayodai kuwa vinara wa demokrasia. ***
Siku ya leo inayosadifiana na tarehe 9 Azar kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsiya huadhimiwa hapa nchini Iran kama siku ya kumbukumbu ya Sheikh Mufid, alimu, msomi na mwanafikra mkubwa wa Kishia. Alimu huyu ambaye ni mashuhuri zaidi kwa jina la Sheikh Mufid, jina lake kamili ni Muhammad bin Nu'man na alizaliwa huko Baghdad mwaka 336 Hijria. Alionyesha kipaji kikubwa cha masomo na ufahamu tangu akiwa katika rika la utoto na ni katika kipindi hicho pia alipoanza kusoma masomo ya Kiislamu. Sheikh Mufid ameandika vitabu vingi ambavyo vinakadiriwa kufikia 200. Al'Alam, Amali na Irshad ni baadhi ya vitabu mashuhuri kwa Sheikh Mufid. Alimu huyu amezikwa huko Kadhmein Iraq. ***