Jumanne, Desemba 08, 2020
Leo ni Jumanne tarehe 22 Mfunguo Saba Rabiuthani 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 8 Desemba mwaka 2020 Miladia
Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, yaani tarehe 8 Desemba 1949 Chian Kai-shek kiongozi wa wapigania uhuru wa China alikimbilia Taiwan akiandamana na baadhi ya wafuasi wake baada ya kushindwa na wapiganaji wa chama cha Kikomonisti wakiongozwa na Mao Tse Tung na kuunda serikali ya kitaifa ya Uchina. Uungaji mkono wa Marekani kwa kiongozi huyo wakati huo ulipelekea Taiwan kujitenga na Uchina na kiti cha nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama ikapatiwa Taiwan. Hata hivyo mnamo mwaka 1971 na baada ya mazungumzo kati ya China na Marekani, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liitambua kwa wingi mkubwa wa kura Jamhuri ya Watu wa China na kuipatia nchi hiyo kiti katika Baraza la Usalama. Kwa utaratibu huo Taiwan ikavuliwa uanachama wa Umoja wa Mataifa.
Siku kama ya leo 180 iliyopita, yaani tarehe 22 Mfunguo Saba Rabiutahni 1262 hijria, alizaliwa katika mji wa Esfahan nchini Iran Sheikh Muhammad Taqi Razi, maarufu kama Agha Najafi, alimu mkubwa wa Kiislamu. Alijifunza elimu za msingi za dini kwa baba yake, kisha akaelekea chuo cha kidini cha Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo yake. Alipokuwa huko, alichota lulu za elimu kwa maulamaa wakubwa wa chuo hicho kama Mirza Muhammad Hassan shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful-Ghit’aa. Baada ya kurudi Esfahan, Agha Najafi alifikia daraja ya juu kabisa ya elimu ya dini ya Umarajaa-Taqlidi. Alimu huyo alikuwa na ushawishi mkubwa kwa watu kiasi kwamba walimtambua kama mwanazuoni aliyekamilisha elimu za mantiki na mapokezi. Mfalme wa wakati huo Nasiruddin Shah na maafisa wa dola la kikoloni la Uingereza nchini Iran walihofu satua na ushawishi wake wa kijamii wakawa wanafanya juu chini ili kudhoofisha nafasi na hadhi yake. Agha Najafi ni miongoni mwa shakhsia waliokuwa na mchango mkubwa katika harakati ya Tumbaku. Miongoni mwa athari za alimu huyo mkubwa ni Al-Ijtihad wat-Taqliid, Asraarul-Aayaat na Anwaarul-Aarifin.
Miaka 152 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 8 Desemba 1868 ulianguka utawala wa Washugani au kwa jina jingine watawala wa kijeshi nchini Japan. Kuanguka kwa utawala huo kulipelekea kuanza kwa marekebisho ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni nchini humo. Washugani walikuwa moja kati ya makumi ya silsila zenye nguvu nchini Japan, walioanzisha utawala wao wa kidikteta tangu karne ya 12 Miladia.
Miaka 117 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Herbert Spencer mwanafikra na mwanafalsafa wa Kiingereza. Spencer alizaliwa mwaka 1820 Miladia na alijifunza elimu mbalimbali kwa baba yake. Baadaye alijiongezea ujuzi wa kielimu kutokana kwa kujisomea na kujiendeleza yeye mwenyewe. Herbert Spencer alikuwa akiamini kuwa, mtu inampasa ajifunze elimu kwa njia ya ushuhudiaji mambo na jarabati. Miongoni mwa athari za mwanafalsafa huyo wa Uingereza ni “Misingi ya Saikolojia”, “Misingi ya Sayansi za Jamii” ambacho ni kitabu cha juzuu tatu na “Misingi ya Biolojia” ambacho ni cha juzuu mbili.
Na siku kama ya leo miaka 106 iliyopita yalijiri mapigano ya baharini ya Falklands pambizoni mwa visiwa vya Falklands katika bahari ya Atlantiki na karibu na ardhi ya Argentina kati ya Uingereza na Ujerumani. Vikosi vya wanamaji vya Ujerumani vilipigwa vibaya na vile vya Uingereza na kupelekea visiwa hivyo kwa mara nyingine tena kuwa chini ya himaya ya Waingereza. Inafaa kuashiria hapa kuwa visiwa vya Falklands viligunduliwa mwishoni mwa karne ya 16 miladia.