May 02, 2021 22:04 UTC
  • Jumatatu, Mei 3, 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 20 Ramadhani 1442 Hijria sawa na tarehe 3 Mei mwaka 2021 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka wa 8 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, jeshi la Kiislamu lililokuwa na wapiganaji elfu kumi chini ya uongozi wa Mtume Muhammad (saw) liliukomboa mji wa Makka. Mtume Mtukufu alichukua hatua hiyo baada ya makafiri kukiuka makubaliano ya amani ya Hudaibiya ambayo yalisainiwa mwaka wa Sita Hijria kati yake na wakuu wa Makuraishi. Mtume Muhammad (saw) alitoa msamaha kwa wakazi wote wa Makka baada ya kukombolewa mji huo katika hali ambayo huko nyuma watu hao walikuwa wakipinga na kupiga vita Uislamu na pia walimuudhi mno Mtume na kuwatesa Waislamu. Muamala huo wa huruma na upendo wa Mtume (saw) uliwavutia watu wa kabila la Kuraishi na kuwafanya waingie kwa wingi katika dini tukufu ya Uislamu. Kwa msingi huo mji wa Makka ulikombolewa pasina kuwepo umwagaji damu.

Siku kama ya leo miaka 900 iliyopita, yaani sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka 542 Hijiria, alifariki dunia Ibn Shajari Baghdadi, fasihi na mtaalamu wa elimu ya nahau wa Kiislamu. Abu Sa'adat Hibatullah Ibn Ali Alawi Hassani, mtaalamu wa nahau, lugha ya Kiarabu, fasihi na malenga wa Kishia, alizaliwa mwaka 450 Hijiria. Nasaba ya msomi huyo inarejea hadi kwa Imam Hassan (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) na ni kwa ajili hiyo ndio maana akaitwa Alawi, Hassani. Akiwa kijana alianza kusomea fasihi, nahau, hadithi na elimu mbalimbali za zama zake na kamwe hakuwahi kuacha kusoma, kama ambavyo hata alipokuwa mzee, bado aliendelea kujifunza kwa wasomi wa zama zake. Aidha alifundisha lugha ya nahau kwa kipindi cha miaka 70 ambapo alitokea kupata wanafunzi mashuhuri katika uwanja huo. Miongoni kwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Al-Aamaal' 'Al-Hamaasah' na 'Mandhumat Ibn Shajarah.' Hatimaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 92 mjini Baghdad Iraq na kuzikwa mjini hapo.

Siku kama ya leo miaka 816 iliyopita, sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka 626 Hijiria, alifariki dunia Yaqut Hamawi mmoja wa waandishi na wasomi tajika wa Kiislamu wa karne ya Saba Hijria na alikuwa mtaalamu mashuhuri wa jiografia. Alizaliwa mwaka 539 Hijria huko Baghdad ambapo ujanani mwake alikamatwa mateka na kufanywa mtumwa. Hata hivyo baada ya kupita muda mfanyabiashara mmoja wa Baghdad alimnunua Hamawi na baadaye akamuachia huru. Miongoni mwa athari za uandishi za Yaqut Hamawi tunazoweza kuziashiria ni vitabu vyake viwili alivyovipa majina ya "Mu'jamul-Buldan" na Mu'jamul- Udabaa."

Siku kama ya leo miaka 768 iliyopita, sawa na tarehe 20 Ramadhani mwaka 674 Hijiria, alifariki dunia Ibn Saai Baghdadi, fasihi na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu. Sheikh Tajud-Din Abu Twalib Ali Ibn Anjub Ibn Uthman Baghdadi, Maarufu kwa jina la Ibn Saai, alizaliwa mwaka 593 mjini Baghdad, Iraq. Awali alianza kujifunza elimu za zama zake kwa walimu mbalimbali na kuibukia kielimu. Kwa miaka kadhaa Ibn Saai alisimamia maktaba ya utawala wa wakati huo mjini Baghdad na ambayo ilitumiwa kwa ajili ya kutwalii. Na baada ya Baghdad kudhibitiwa na silsila ya utawala wa Wamongolia, hatimaye Ibn Saai Baghdadi aliteuliwa na Nasir al-Din al-Tusi kwa ajili ya kusimamia maktaba mbalimbali za mji huo. Ni katika kipindi hicho ndipo akatokea kuwa mwandishi mkubwa, jambo ambalo lilimuingizia kiasi kikubwa cha fedha. Kitabu cha 'al-Khulafaau' ni miongoni mwa athari mashuhuri za Ibn Saai. Aidha ameandika kitabu cha 'Akhbaarul-Udabaa' 'Akhbaarul-Hallaj' na 'Akhbaaru Qudhaatu Baghdad.' Abin Saai, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 na kuzikwa mjini Baghdad.

Siku kama ya leo miaka 592 iliyopita, Jeanne d'Arc alianzisha harakati ya kihistoria ya kuzikomboa baadhi ya ardhi za Ufaransa zilizokuwa zikikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Jeanne d'Arc alikuwa kamanda wa jeshi ambaye alipewa jukumu na Mfalme wa Ufaransa la kuongoza mapambano dhidi ya majeshi ya Uingereza yaliyolikalia kwa mabavu eneo la kaskazini mwa Ufaransa. Hatimaye Kamanda huyo alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kimaonyesho nchini Uingereza kwa tuhuma za kuritadi na kuacha dini na mwaka 1431 aliuawa kwa kuchomwa moto akiwa hai.

Jeanne d'Arc

Siku kama ya leo miaka 552 iliyopita alizaliwa Niccolò di Bernardo dei Machiavelli, mwanahistoria na mwanasiasa wa Italia katika mji wa Florence. Sambamba na shughuli zake za kisiasa, Machiavelli aliandika pia kuhusu historia ya Florence. Katika mtazamo wa kisiasa, Machiavelli alikuwa akiamini kwamba inawezekana kutumia wenzo wowote ule kwa ajili ya kupata madaraka na kwa ajili ya kuyalinda, na kwamba hakuna udharura wowote wa kuheshimiwa misingi ya maadili katika masuala kama hayo. Miongoni mwa kazi za mwanahistoria na mwanasiasa huyo wa Italia ni "The Art of War" na "The Prince."

Niccolò di Bernardo dei Machiavelli

Siku kama ya leo miaka 527 iliyopita, sawa na tarehe 3 Mei 1494 Miladia, Christopher Columbus, baharia wa Uhispania aligundua nchi ya Jamaica, huko Amerika ya Kati katika safari yake ya pili ya uvumbuzi ndani ya bara la Amerika. Licha ya tabia ya upendo na maridhiano ya wakazi asilia wa Jamaica na nchi nyingine zilizogunduliwa, lakini Christopher Columbus na watu wengine waliotumwa na Uhispania, waliwafanyia ukatili wenyeji hao wakazi. Kwa utaratibu huo Jamaica ambayo kutokana na nafasi yake muhimu ya kijografia na kwa kuwa na dhahabu nyingi zilizokuwa zikikodolewa macho na Uhispania, ilikoloniwa kuanzia mwaka 1509 Miladia hadi muda unaokaribia karne mbili. Baada ya Uhispiania nchi hiyo pia ilikoloniwa na Uingereza ambapo katika kipindi hicho akthari ya wakazi wake asilia walifukuzwa au kuuawa. Hatimaye nchi hiyo iliweza kujipatia uhuru wake mwaka 1962 Miladia.

Jamaica

Siku kama ya leo miaka 174 iliyopita, yaani tarehe Tatu Mei 1847, alizaliwa Alexander Graham Bell mbunifu wa simu nchini Marekani. Bell alikuwa na shauku kubwa ya kuwa fundi na mhandisi tokea zama za ujana wake. Baada ya kufanya utafiti na uchunguzi kwa muda wa miaka 10, hatimaye alifanikiwa kutengeneza chombo chenye uwezo wa kuhamisha sauti, ambacho kinafanana na simu zinazotumika leo hii. Hali kadhalika mtaalamu huyo wa Kimarekani alifanikiwa kutengeneza chombo kinachonasa sauti au phonograph. Alexander Graham Bell alifariki dunia mwaka 1922.