Ijumaa, Mei 7, 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 24 Ramadhani mwaka 1442 Hijria sawa na tarehe 7 Mei mwaka 2021
Siku kama ya leo miaka 73 i2liyopita alifariki dunia Qutbuddin Shirazi, tabibu, mwanahesabati, mwanafikizia na mwanafalsafa wa Kiirani katika mji wa Tabrizi huko kaskazini magharibi mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi. Alibobea pia katika elimu za mantiki na irfani. Alifanya hima kubwa kutafuta elimu ya tiba na alihudumu kwa miaka mingi kama tabibu katika hospitali ya Shiraz, kusini mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa mtu wa kwanza kufanya uchunguzi kuhusu upinde wa mvua na kupata tafsiri ya kisayansi kuhusu suala hilo. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika taaluma mbalimbali.
Miaka 213 iliyopita katika siku kama ya leo wananchi wa Uhispania walianzisha harakati dhidi ya vikosi vya jeshi la Mfalme Napoleon wa Ufaransa, vilivyokuwa vinakalia kwa mabavu nchi yao. Wakati huo Uhispania pia ilikuwa ikihesabiwa kuwa moja ya makoloni makubwa ya Ulaya na ilikuwa ikikalia kwa mabavu ardhi nyingi nje ya bara hilo. Lakini wananchi wa Uhispania walikuwa wameonja uchungu wa nchi yao kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya kigeni. Baada ya miaka mitano ya mapambano dhidi ya vikosi vamizi vya Ufaransa, walifanikiwa kuvifukuza vikosi hivyo mwezi Disemba mwaka 1813 kutoka nchini kwao. Wakati huo huo kutokana na kushindwa katika Amerika ya Kusini, Uhispania ililazimika kuziacha huru nchi kadhaa ilizokuwa ikizikoloni.
Siku kama ya leo miaka 209 iliyopita, alizaliwa Robert Browning, malenga na mwanafikra wa nchini Uingereza. Akiwa kijana mdogo Browning alikuwa na maandalizi ya kuwa malenga ambapo alitoa shairi lake la kwanza akiwa na umri wa miaka 12. Taratibu akaanza kupata umashuhuri katika jamii ya Uingereza kama malenga mkubwa. Robert Browning alikuwa akiwasilisha itikadi yake juu ya umoja wa Mungu duniani kupitia mashairi yake. Ameacha athari nyingi katika uwanja huo. Robert Browning alifariki dunia mwaka 1889.
Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mei 1888, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilianzisha uvamizi katika ardhi ya Zimbabwe ya sasa. Mipango ya kuikalia kwa mabavu Zimbabwe ilibuniwa na mwanasiasa na mfanyabiashara aliyejulikana kwa jina la Cecile Rhodes, ambaye aliasisi shirika la Afrika Kusini la Kiingereza nchini humo. Kwa kusaidiwa na jeshi la Uingereza, Rhodes aliuwa kwa umati maelfu ya raia wazalendo na kuwakamata mateka wengine wengi, na hivyo kuweza kuidhibiti ardhi yote ya Zimbabwe na kuipachika jina lake la Rhodesia.