May 16, 2021 03:56 UTC
  • Jumapili, 16 Mei, 2021

Leo ni Jumapili tarehe 4 Mfunguo Mosi Shawwal 1442 Hijria sawa na tarehe 16 Mei, 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1091 iliyopita, sawa na tarehe 4 Shawwal mwaka 351 Hijiria, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Dar Ghotni mmoja wa maulamaa na wataalamu wa lugha wa karne ya Nne Hijria. Dar Ghotni alikuwa mmoja wa maqari na wafasiri watajika wa Qu'rani Tukufu katika zama zake hizo, ambaye alitumia umri wake mwingi kuandika vitabu vya kielimu.

Miaka 519 iliyopita katika siku kama ya leo, ardhi ya Honduras inayopatikana leo huko Amerika Kusini iliunganishwa na makoloni ya Muhispania. Kabla ya hapo Honduras ilikuwa kituo cha utamaduni wa kaumu ya Maya. Hata hivyo baada ya Honduras kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Uhispania, kabila hilo liliangamizwa na kupotea. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia na kutokana na kuvurugika hali ya ndani ya Uhispania, Honduras kama ilivyokuwa kwa makoloni mengine, ilitumia fursa hiyo kuweza kujipatia uhuru wake.

 

Katika siku kama ya leo miaka 233 iliyopita, alizaliwa mjini Hamburg Friedrich Ruckert, malenga na mtaalamu wa masuala ya mashariki ya dunia wa nchini Ujerumani. Alikuwa mtafiti mkubwa wa masuala ya mashariki, aliyefundisha katika vyuo vikuu vya Ujerumani. Alifanya juhudi ya kutafsiri mashairi kwa lugha ya Kifarsi, Kiarabu na Kichina. Kadhalika alijifunza fasihi na tamaduni za eneo hilo na kuzitumia katika kusoma mashairi. Aidha Friedrich Ruckert  alikuwa mmoja wa malenga wa Kijerumani aliyefanikiwa kutarjumu diwani ya mashairi ya Hafez (malenga mkubwa wa Kiirani) katika lugha ya Kijerumani ambapo tarjama yake imechapishwa mara kadhaa nchini humo. Miongoni mwa athari ya Friedrich Ruckert ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Msimu wa Machipuko wa Upendo' na 'Sharqiyat.

Friedrich Ruckert

Miaka 33 iliyopita Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti lilianza kuondoka nchini Afghanistan. Baada ya Nur Muhammad Taraki kupinduliwa, serikali ya kwanza ya kikomunsti iliyokuwa ikipata himaya ya moja kwa moja ya Urusi ya zamani ilianzishwa nchini Afghanistan. Utawala wa Taraki uliondolewa madarakani mwanzoni mwa mwaka 1979 kupitia mapinduzi mengine yaliyoongozwa na Hafidhullah Amin mmoja wa watu wake wa karibu. Lakini Warusi hawakumpenda Hafidhullah ambaye alikuwa akitaka kujikurubisha kwa Marekani na kuanzisha uhusiano kati ya Afghanistan na Mashariki na vilevile Magharibi na hivyo wakaipindua serikali yake. 

Askari wa Sovieti wakiondoka Afghanistan

Katika siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, Jenerali Mobutu Sese Seko rais na dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zaire ya zamani, aliikimbia nchi hiyo baada ya vikosi vya majeshi ya waasi vilivyokuwa vikiongozwa na Laurent Kabila kukaribia mji wa Kinshasa. Mobutu alichukua madaraka ya nchi hiyo mnamo mwaka 1965 kupitia mapinduzi ya kijeshi na kisha kutawala kwa muda wa miaka 32. Licha ya kiongozi huyo kuwa dikteta asiye na huruma, lakini alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi hasa Marekani na Ufaransa. Kutokana na Congo DR kuwa katika eneo nyeti na muhimu kijiografia katikati mwa bara la Afrika na kuwa na utajiri mkubwa wa madini ikiwemo almasi, imekuwa ikizingatiwa sana na kumezewa mate na nchi za Magharibi. Siku moja baada ya Mobutu kuikimbia nchi hiyo, vikosi vya waasi viliuteka mji wa Kinshasa na kiongozi wao yaani Laurent Kabila, akashika hatamu za uongozi wa nchi.

Mobutu Sese Seko