Jun 13, 2021 02:48 UTC
  • Jumapili, Juni 13, 2021

Leo ni Jumapili tarehe Pili Dhul Qaada 1442 Hijria Qamaria sawa na Juni 9 mwaka 2021 inayosadifiana na 23 Khordad mwaka 1400 Hijria Shamshiya

Miaka 1131 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ibn Khuzaima, mpokeaji wa hadithi na faqih mashuhuri wa karne ya nne Hijria. Ibn Khuzaima alizaliwa mwaka 223 Hijria na alifanya safari katika pembe mbalimbali duniani wakati wa ujana wake kwa lengo la kujipatia elimu mbalimbali za kidini. Faqih huyo wa Kiislamu  ameandika vitabu vingi vya thamani na muhimu zaidi ni kile alichokipa jina la al Tahid wa Ithbati Swifati al Rabb".

 

Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, inayosadifiana na 23 Khordad 1359 Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwa na lengo la kufanya mabadiliko katika vyuo vikuu hapa nchini, alitoa amri ya kuasisiwa Baraza la Mapinduzi la Kiutamaduni. Katika ujumbe wake, Imam Khomeini MA aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuratibu na kuandaa mipango na mitalaa katika kozi mbalimbali za vyuo vikuu inayokwenda sambamba na mafunzo ya utamaduni tajiri wa Kiislamu.

Imam Ruhullah Khomeini

 

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita muwafaka na tarehe 13 Juni 1921 katika miaka ya mwanzo ya usimamizi wa Uingereza huko Palestina, ilianza harakati kubwa ya kwanza ya wananchi katika ardhi yote ya Palestina dhidi ya Wazayuni. Harakati ya wananchi hao wa Palestina ilibainisha upinzani wao dhidi ya siasa za kikoloni za Uingereza pamoja na uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Wazayuni waliokuwa wakiishi Palestina. Katika fremu ya sera hizo za Uingereza mwaka 1923 kulikuwa na Wazayuni 35 elfu huko Palestina na kabla ya kuundwa utawala bandia wa Israel mwaka 1948 idadi hiyo ilikuwa zaidi ya laki sita.

Utawala wa Kizayuni

 

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita sawa na tarehe 13 Juni mwaka 1944, kombora la kwanza la ardhi kwa ardhi la Ujerumani ya Kinazi lililojulikana kwa jina la V-1 lilishambulia ardhi ya Uingereza, katika Vita vya Pili vya Dunia. Kabla ya hapo Ujerumani ilikuwa ikiishambulia ardhi ya Uingereza kwa njia ya anga. Baada ya vita hivyo, nchi nyingine duniani zilitengeneza makombora ya aina hiyo kwa teknolojia ya kisasa zaidi.

Vita Vikuu vya Pili vya Dunia

 

Na katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, yaani tarehe 23 Khordad 1362 Hijria Shamsia, Bi. Nusrat Amin faqihi na mfasiri mkubwa wa Qurani Tukufu alifariki dunia katika mji wa Esfahan ulioko katikati mwa Iran. Bi. Nusrat Amin aliutumia muda wake wote katika kuishughulikia Qurani Tukufu, na amefanikiwa kufasiri juzuu 15 za Qur'ani na kuandika vitabu kadhaa.

Bi. Nusrat Amin